MJUMBE wa Halmashauri kuu Taifa CCM (MNEC) na Mbunge wa Jimbo la Mvumi Mhe.Livingstone Lusinde ,akizungumza na waandishi wa habari leo Agosti 3,2021 jijini Dodoma.
………………………………………………………………
Na.Alex Sonna,Dodoma
MJUMBE wa Halmashauri kuu Taifa CCM (MNEC) na Mbunge wa Jimbo la Mvumi Mhe.Livingstone Lusinde amemtaka Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) John Mnyika kukaa kimya ili mahakama itende haki katika sakata la Mwenyekiti wao Freeman Mbowe.
Kauli hiyo ameitoa leo Agosti 3,2021 jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari Lusinde,amesema kuwa mahakama ni chombo huru hivyo hakiwezi kulazimishwa na watu au chombo chochote.
“Nashangazwa sana na matamshi ya Viongozi na wanachama wa CHADEMA wamekuwa na mambo ya ajabu sana , kesi ya Mwenyekiti wao Freeman Mbowe ipo kisheria na sio kisiasa,sasa wao wamekuwa wakihusisha kesi za mahakama na mambo ya kisiasa,” amesema Mhe.Lusinde
Aidha Lusinde amesema kuwa kitendo cha kuishinikiza mahakama ifanye wanachotaka wanasiasa ni ukiukwaji mkubwa wa Katiba ya nchi unaofanywa na watu wanaojiita ni walinda Katiba.
”CHADEMA wanachukulia katiba mpya ni hitaji lao peke yao wakati Rais Samia alishasema suala hilo lisubiri, hivyo hakuna haja ya kuendelea kumshinikiza Mkuu wa nchi”amesistiza
Aidha Lusinde amemshukia aliyewahikuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Ludovick Ottouh alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu kodi za mishahara ya wabunge kuwa wanatakiwa kukatwa kodi katika mishahara yao.
“Sisi tumetunga sheria sio kiwango,Mbona hata mwanzo makato yalikuwa kwenye simu, ndugu zangu tujifundishe kulipa kodi nani wa kutupa hela za bure?Mjadala uwe hapo tozo ni kubwa hivyo Waziri apunguze sio lilaumiwe Bunge,”amesema.
Lusinde amesema kuwa wao wanakatwa kodi ambazo zinaenda kwenye shughuli za kimaendeleo hapa nchini hivyo jamii iondokane na maneno kwamba wao hawakatwi kodi.
Pia Lusinde ametaja mshahara wake analipwa Sh milioni 4.6 na anakatwa kodi lakini hata wabunge wengine wanakatwa kodi kama ilivyo kwa watumishi wengine wa umma wanavyokatwa kodi.
“Ndugu zangu mimi nimeleta hapa Salary Sleep yangu mimi Livinstone Lusinde inaonyesha nalipwa shilingi milioni 4.6kwa mwezi huku makato ya mshahara yakiwa ni zaidi ya milioni 1.2 hivyo nashangaa kusikia kuwa Wabunge hatukatwi kodi”amesema
Hata hivyo Lusinde amemkaribisha Ottouh pamoja na wengine wanaodhani kuwa kazi ya Ubunge ni rahisi wajaribu kugombea kwani mwaka 2025 sio mbali.
Hata hivyo,Lusinde amewaomba wabunge kusimamia fedha walizopewa za kujenga barabara katika majimbo yao ambayo fedha hizo zimeelekezwa kwa wakala wa barabara za mijini na vijijini (TARURA) kwa lengo la kuwaletea wananchi maendeleo.
”Katika bajeti iliyopita kila Mbunge wa jimbo la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wamepatiwa kiasi cha fedha zaidi ya Bilion moja kwaajili ya barabara katika majimbo yote nchini”amesema
Aidha Lusinde amewataka watanzania nchini kuendelea kujikinga na ugonjwa wa Corona kwa kufuata taratibu na kanuni zote zilizotolewa na wataalamu wa afya ili kila mwananchi aendelee kulinda na afya yake.
”Nawaomba watanzania waendelee kujikinga huu ugonjwa ni hatari sana tunapoteza ndugu zetu wengi vijijini na mijini,ili tuendelee kuwa salama lazima tujikinge kwa kufuata maelekezo ya wataalamu.”