Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) akizungumza na wananchi wa kijiji cha King’ombe alipofanya ziara ya kikazi ya kusikiliza kero za wananchi kuhusu mipaka ya Hifadhi ya Msitu ya mto Loasi katika Kata ya Kala Wilaya ya Nkasi leo. Kulia ni Mbunge wa Jimbo la Nkasi Kusini, Mhe. Vicent Mbogo na Mkuu wa Wilaya ya Nkasi, Mhe. Peter Lijuakali (kushoto).
Baadhi ya wananchi wa kijiji cha King’ombe wakimsikiliza Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao kuhusu mkakati wa Serikali wa kupima upya mipaka ya Hifadhi ya Msitu ya mto Loasi katika mkutano uliofanyika Kata ya Kala Wilaya ya Nkasi leo.
Mkuu wa Wilaya ya Nkasi, Mhe. Peter Lijuakali akizungumza na wananchi wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) (hayupo pichani) katika kijiji cha King’ombe Kata ya Kala Wilaya ya Nkasi leo.
Mbunge wa Jimbo la Nkasi Kusini, Mhe. Vicent Mbogo akimshukuru Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) wakati wa ziara ya kikazi katika kijiji cha King’ombe Kata ya Kala Wilaya ya Nkasi leo.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) akiteta jambo na Mbunge wa Jimbo la Nkasi Kusini, Mhe. Vicent Mbogo wakati wa ziara yake ya kikazi katika kijiji cha King’ombe Kata ya Kala Wilaya ya Nkasi leo.
***************************
Wananchi wa Kijiji cha King’ombe Kata ya Kala Wilayani Nkasi wameiomba Serikali kuangalia namna ya kuwaongezea ardhi ya kijiji ili waweze kufanya shughuli za maendeleo kama kilimo na ufugaji kwani wanashindwa kufanya shughuli hizo kutokana na kubanwa na Hifadhi ya Msitu wa Mto Loasi.
Hayo yamesemwa wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) alipokuwa akizungumza na wananchi hao leo.
“Shida tuliyonayo wananchi wa King’ombe ni ardhi kuwa finyu, tuna hekta zisizopungua hekta 6,260 na wakazi wa mahali hapa ni zaidi ya kaya elfu 10 na pia tuna Sekondari ya Kata hapa” amesema Titus Pius ambaye ni Mkazi wa Kijiji cha King’ombe.
Naye Mkazi mwingine wa kijiji hicho Maria Mpoli ameiomba Serikali iwasaidie kuongeza ardhi ili wanakijiji waweze kulima kwa nafasi.
Akijibu hoja hiyo, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) amesema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na wataalamu wa ardhi itaunda kamati itayoainisha mipaka mipya ya Hifadhi ya Msitu wa Mto Loasi.
“Hii kamati itapitia mipaka ya hifadhi upya na haitapita mwezi wa nane, tutarekebisha ramani yetu ya mwaka 1957 kwa kuviondoa hivo vijiji ambavyo viliingia mwaka 1974 na baada ya hapo tutaangalia uhitaji wa wananchi kama tunatakiwa kuwaongezea ardhi au kuwapunguzia” Mhe. Mary Masanja amefafanua.
Mhe. Masanja amewaasa wananchi wa kijiji hicho kuwa waangalifu kwa kuepuka kuvamia maeneo ya hifadhi ili kuepuka migogoro ya wanyamapori wakali na waharibifu kama tembo.
“Lengo la Serikali sio kun’gang’ania maeneo bali ni pamoja na kuwakinga wananchi wasikutane na wanyama wakali na waharibifu na changamoto ya tembo itaendelea kuwepo kama sisi tutayasogelea maeneo ya wanyama wakali na waharibifu ” Mhe. Masanja amesisitiza.
Amesema Serikali inayahifadhi baadhi ya maeneo kwa ajili ya kulinda maeneo ya wanyama kwa ajili ya kutangaza utalii ambao unaongeza mapato, kwa Serikai kwa ajili ya kujenga vituo vya afya, shule n.k.
“Unaweza ukaomba eneo lakini kumbe ni hatarishi ni mapito ya tembo, baada ya mwaka mmoja utaanza kuilalamikia Serikali kwamba tembo wamekula mazao yako hivyo, msisogelee maeneo ya wanyama hawa”Mhe. Masanja ameweka bayana.
Awali , Mkuu wa Wilaya ya Nkasi, Mhe. Peter Lijuakali amewaambia wananchi hao kuwa mkutano huo umefanyika ikiwa ni utekelezaji wa ilani ya CCM inayosema itatatua kero za wananchi na kuwapunguzia wananchi nafuu ya maisha.
Mkutano huo ni mwendelezo wa ziara za kikazi za Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja za kusikiliza changamoto za wananchi zinazohusiana na sekta ya maliasili na utalii katika maeneo mbalimbali nchini.