Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Mhandisi Robert Gabriel akikata utepe kuashiria kuzindua rasmi Boti mbili mpya kwa ajili ya kubeba wagonjwa (Ambulance Boat) pamoja na boti ya uokozi (Rescue Boat) katika hafla fupi iliyofanyika katika yadi ya Songoro Ilemela Mkoani Mwanza. Boti hizo mbili, MV. NZERA itakayotoa huduma ya kubeba wagonjwa Geita vijijini na MV. UKEREWE itakayokuwa ikitoa huduma ya kubeba wagonjwa katika Visiwa vya Ukerewe zimegharimu jumla ya shilingi Milioni 553, wakati boti ya uokozi ukarabati wake ukigharimu shilingi milioni 576.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Mhandisi Robert Gabriel, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Mhandisi Japhet Y. Maselle (wa pili kushoto), Meneja wa TEMESA mkoa wa Mwanza Mhandisi Hassan Karonda kushoto, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza Antony Diallo wakisubiri kukata utepe kuzindua boti za MV. NZERA, MV.SAR IV Pamoja na MV. UKEREWE II Kazi Iendelee. Hafla hiyo fupi imefanyika katika yadi ya Songoro Ilemela Mkoani Mwanza.
Pichani ni Boti tatu, MV. NZERA, MV.SAR IV Pamoja na MV. UKEREWE II Kazi Iendelee mara baada ya kuzinduliwa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Mhandisi Robert Gabriel. Boti mbili za kubeba wagonjwa zimegharimu jumla ya shilingi Milioni 553, wakati boti ya uokozi ukarabati wake ukigharimu shilingi milioni 576.
Picha ni (Ambulance Boat) Boti ya MV. NZERA itakayokuwa ikitoa huduma ya kubeba wagonjwa Geita vijijini. Boti hiyo iliyozinduliwa leo na Mkuu wa Mkoa Mwanza Mhe. Mhandisi Robert Gabriel imegharimu kiasi cha shilingi milioni 217.
Picha ni (Ambulance Boat) Boti ya MV. UKEREWE itakayokuwa ikitoa huduma ya kubeba wagonjwa katika visiwa vya Ukerewe. Boti hiyo iliyozinduliwa leo na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Mhandisi Robert Gabriel imegharimu kiasi cha shilingi milioni 217.
Picha ni (Rescue Boat) Boti ya Uokozi ya MV.SAR IV ambayo imefanyiwa ukarabati mkubwa uliogharimu kiasi cha shilingi milioni 576, Boti hiyo ya tani 3 itakua ikitoa huduma ya uokozi Mkoani Mwanza.
PICHA ZOTE NA ALFRED MGWENO (MWANZA)
**************************
ALFRED MGWENO (TEMESA MWANZA)
Serikali kupitia Wakala wa Ufundi na Umeme nchini (TEMESA) imeendelea kuboresha huduma za afya nchini baada ya leo kukabidhi boti mbili mpya za kubeba wagonjwa (Ambulance Boats) kwa wakazi wa visiwa vya Ukerewe Mkoani Mwanza na Geita vijijini. Boti hizo mbili, MV. NZERA itakayokuwa inatoa huduma Geita vijijini na MV. UKEREWE II itakayopelekwa visiwa vya Ukerewe, kila moja imegharimu shilingi milioni 276,600,000 za Kitanzania. Vilevile Serikali imepokea Boti ya uokozi, MV.SAR IV ambayo ilikuwa ikifanyiwa ukarabati mkubwa uliogharimu shilingi milioni 576,000,000/= (Bila ya ongezeko la kodi-VAT)
Akizungumza wakati wa kupokea Boti hizo mapema leo katika hafla fupi iliyofanyika katika Yadi ya Songoro iliyopo Ilemela Mkoani Mwanza, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel ameipongeza na kuishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kutekeleza ujenzi wa boti hizo.
‘’Ninafurahi kusikia kuwa kazi ya ukarabati wa boti ya uokozi imekamilika kwa gharama ya shilingi za Kitanzania TZS 576,000,000 na ununuzi wa boti hizi za kubeba wagonjwa umefanyika kwa gharama ya shilingi za Kitanzania 217,600,000 kila moja na fedha yote ikiwa imetolewa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania’’. Alisema Mhandisi Gabriel, ambapo ameipongeza kampuni ya kizalendo ya Songoro Marine Transport Boatyard ya Mwanza iliyojenga boti hizo na kuikarabati boti ya uokozi (Rescue Boat).
‘’Bila shaka kukamilika kwa boti hizi na kuanza kutumika kutaboresha huduma za afya za wananchi wa maeneo ambayo zinapelekwa kama alivyosema Mtendaji Mkuu wa TEMESA’’.
Mhandisi Gabriel pia ametoa maelekezo kwa halmashauri husika kuzisimamia na kuziendesha kwa weledi huku akiitaka TEMESA kushirikiana na Halmashauri kwa kutoa ushauri wa kitaalam mara kwa mara ili boti hizo ziweze kudumu na kuendelea kutoa huduma iliyokusudiwa ya kuwaondolea adha ya usafiri wagonjwa wa maeneo haya.
Awali, akizungumza katika hafla hiyo, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme
(TEMESA), Mhandisi Japhet Y. Maselle, amesema Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kupitia
Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) imetekeleza miradi mingine ya ujenzi wa boti za
kusafirisha wagonjwa tatu kwa ajili ya Mikoa ya Lindi, Geita na Mwanza ambapo Boti
nyingine moja tayari imekabidhiwa mkoa wa Lindi ili kuwahudumia wananchi wa Kilwa
Kisiwani.
‘‘Boti hizi mpya zina uwezo wa kubeba kilo elfu mbili (2000Kg) sawa na watu 12 kwa wakati mmoja. Aidha, zina sehemu ya muongozaji (Nahodha), sehemu ya kumhudumia mgonjwa na sehemu ya kukaa wauguzi. Pia boti hii ina vifaa maalum vya uokoaji (Special equipment for medical rescue) na Kitanda cha kubebea mgonjwa (Stretcher)‘‘. Alisema Mhandisi Maselle na kuongeza kuwa Boti hizo zinakabidhiwa kwa uongozi wa Halmashauri za Wilaya za Ukerewe na Geita Vijijini kila moja boti moja kwa ajili ya kuwahudumia wananchi wa maeneo hayo.
Mhandisi Maselle ameongeza kuwa Boti ya MV. SAR IV ina uwezo wa tani 3, urefu wa mita 11.5, upana wa mita 3.
‘’Boti hii ya uokozi ina vifaa vya kisasa vya kuiongoza kama GPS, na vifaa vya uokozi vya kutosha kwa idadi ya watu wanaoruhusiwa kubebwa, vifaa hivyo ni makoti ya kujiokoa (life jackets) na maboya (life rafts na life buoys).’’Alimaliza Mhandisi Maselle.
Gharama zote za ujenzi wa boti hizo zimegharamiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi.