Waziri wa Kilimo Mhe. Prof Adolf Mkenda akikagua skimu ya Umwagiliaji ya Mkombozi iliyopo tarafa ya Pawaga katika Wilaya ya Iringa, leo tarehe 2 Agosti 2021 mara baada ya kufanya ziara ya kikazi ya siku moja Mkoani Iringa.
Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Iringa
Serikali imebainisha kuwa suluhisho pekee la sekta ya Kilimo cha Umwagiliaji ni kuongeza uwezo wa kiuhandisi katika Tume ya Taifa ya Umwagiliaji.
Waziri wa Kilimo Mhe. Prof Adolf Mkenda ameyasema hayo leo tarehe 2 Agosti 2021 mara baada ya kutembelea na kukagua Skimu za Umwagiliaji za Magozi na Mkombozi zilizopo katika Tarafa ya Pawaga katika Wilaya ya Iringa Mkoani Iringa.
Amesema kuwa Serikali imekusudia kufanya hivyo ili kuongeza ufanisi wa kazi katika Tume hiyo ya Taifa ya Umwagiliaji jambo litakaloimarisha kilimo cha Umwagiliaji ili wakulima waachane na Kilimo cha kutegemea mvua za msimu.
Kadhalika ili kutatua changamoto mbalimbali kwenye Skimu za Umwagiliji, Waziri Mkenda amesema kuwa serikali imekuja na suluhisho ambalo ni mpango shirikishi kwa watumia maji.
Amebainisha kuwa mpango huo itakuwa ni kutoza tozo kwa watumia maji ili kukiwa na matatizo ya uharibifu wa miundombinu Mfuko huo maalumu uweze kutumika kwa ajili ya marekebisho hayo.
Pamoja na mambo mengine Waziri Mkenda ametoa rai kwa wakulima kote nchini kuhakikisha kuwa wanaendelea na shughuli za uzalishaji mali ikiwemo Kilimo lakini wanapaswa kuchukua tahadhali zote zinazoelekezwa na serikali ili kujiepusha na maambukizi ya UVIKO 19.
Waziri wa Kilimo Mhe. Prof Adolf Mkenda ameanza zira ya kikazi katika mikoa ya Nyanda za juu kusini Iringa, Njombe, Songwe na Rukwa ambapo atakagua hali ya upatikanaji wa mbolea, ununuzi wa mahindi pamoja na kukagua skimu za umwagiliaji.