Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Omary Kipanga (mwenye kofia ya kijani) akipokea maelekezo ya ujenzi wa jengo la kliniki kutoka kwa Meneja Uzalishaji na Usimamizi wa Miradi, Injinia Faraji Magania wakati alipokuwa akikagua ujenzi wa jengo hilo linalojengwa katika Chuo cha Ufundi Arusha.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Omary Kipanga (mwenye kofia ya kijani) akifafanua jambo mara baada ya kukagua ujenzi wa jengo la madarasa na maabara linalojengwa katika Chuo cha Ufundi Arusha.
Mchoro unaoonesha jengo la bweni la wasichana linalojengwa katika Chuo cha Ufundi Arusha litakavyokuwa baada ya kukamilika.
Baadhi ya bidhaa zinazotengenezwa na karakana ya uashi ya Chuo cha Ufundi Arusha.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Omary Kipanga akiangalia mmoja wa wanafunzi wa ufundi magari katika Chuo cha Ufundi Arusha akiinua gari kwa kutumia jeki ya umeme.
*****************************
Na WyEST
# Utekelezaji wake wafikia asilimia 49
# Bweni la wanafunzi 420 na kliniki ya matibabu pia kujengwa
Serikali inatarajia kutumia zaidi ya Shilingi bilioni 4.2 katika mwaka wa fedha 2021/22 kukamilisha ujenzi wa jengo la madarasa na maabara katika Chuo cha Ufundi Arusha (ATC).
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Omary Kipanga akiwa ziarani Jijini Arusha ambapo amesema jengo hilo litakuwa na ghorofa tatu lenye maabara, madarasa, ofisi na stoo.
Amesema mpaka sasa ujenzi wa jengo hilo umegharimu zaidi ya Shilingi bilioni 2.6 na kwamba hadi kukamilika litatumia jumla ya Shilingi bilioni 6.8.
“Lengo la Serikali ni kuhakikisha inaboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia ili kuweza kuzalisha wataalamu watakaokuwa na umahiri unaohitajika katika soko la sasa la ajira,” amesisitiza Mhe. Kipanga.
Awali akitoa taarifa ya miradi mbalimbali ya ujenzi inayotekelezwa chuoni hapo, Kaimu Mkuu wa Chuo hicho, Dkt. Musa Chacha amesema chuo kimepokea jumla ya Shilingi bilioni 1.499 kutoka Serikalini kwa ajili ya ujenzi wa bweni la wasichana litakalokuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 420 likikamilika na kwamba ujenzi wake umefikia asilimia 15.
Amesema chuo pia kina mradi wa ujenzi wa kliniki itakayogharimu takribani Shilingi bilioni moja ambazo zitatokana na mapato ya ndani na kwamba ujenzi wake umefikia asilimia 30.
Aidha Dkt. Chacha amesema chuo kupitia maabara zake kimetafiti na kutengeneza bidhaa mbalimbali kwa matumizi ya jamii ikiwemo vipukuswa vyenye ubora, barakoa na dawa ya kunywa kwa waathirika wa UVIKO-19 ili kupambana na janga la ugonjwa huo.
Naibu Waziri Kipanga yupo Jijini Arusha kwa ziara ya kukagua miradi mbalimbali ya ujenzi katika vyuo na taasisi zilizo chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.