Katibu Mkuu Wizara ya Afya- Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii, Dkt. John Jingu akizungumza na wajumbe wa mtandao wa kutokomeza Ndoa za Utotoni (TECMN)katika kikao cha kujadili namna bora ya kutokomeza ukatili dhidi ya watoto nchini.
Mratibu wa Mtandao wa kutokomeza mimba za utotoni nchini, Euphemia Edward akichangia jambo katika kikao cha kujadili namna bora ya kutokomeza ukatili dhidi ya watoto, Kikao kitafanyika katika Ofisi ya Katibu Mkuu Wizara ya Afya- Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii, Dodoma.
Mjumbe wa TECMN kutoka Shirika la Save the Children Dickson Megera akieleza jambo katika kikao cha kujadili namna bora ya kutokomeza ukatili dhidi ya watoto kulichofanyika leo Jijini Dodoma na kuwakutanisha wajumbe wa Mtandao huo na Katibu Mkuu Wizara ya Afya- Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii, Dkt. John Jingu.
Washiriki wa kikao cha pamoja cha kujadili namna bora ya kutokomeza ukatili dhidi ya watoto kilichofanyika leo katika ofisi ya Katibu Mkuu Wizara ya Afya- Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii.
Picha ya pamoja ya Katibu Mkuu Wizara ya Afya- Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu na wadau wa Mtandao wa kutokomeza mimba za utotoni Tanzania (TECMN) baada ya kujadili namna bora ya kutokomeza ukatili dhidi ya watoto, katika ofisi ya Katibu Mkuu kilichofanyika leo, Dodoma
……………………………………………………………………..
Na Mwandishi wetu, Dodoma
Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii, Dkt. John Jingu amesema zinahitajika mbinu shirikishi kuanzia ngazi ya Familia za kukabiliana na vitendo vya ukatili ikiwemo mimba za utotoni.
Dkt. Jingu ameyasema hayo Jijini Dodoma katika kikao chake na Wajumbe wa Mtandao wa kutokomeza Ndoa za Utotoni Tanzania TECMN ikiwa ni njia ya kupambana na vitendo vya ukatili.
Amesema mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia zikiwemo ndoa za utotoni yanatakiwa kuanza katika ngazi ya familia na hatimaye mifumo yake kuendelea hadi taifa.
Akitoa mifano katika baadhi ya mikoa, Katibu Mkuu Jingu amesema pamoja na jitihada zinazochukuliwa na serikali katika kusimamia sheria za kuharamisha vitendo hivyo, bado vitendo hivyo vinaendelea kutokana na mila na desturi za jamii husika.
Amesema baadhi ya ndugu na wanafamilia wanachelea kutoa ushahidi wa unyanyasaji kutokana na ukali wa sheria zilizopo ili kuwanusuru wanafamilia wanaohusika katika vitendo hivyo vya ukatili ikiwa ni pamoja na kuwakatili watoto kwa kuwapa mimba.
Akizungumzia njia za mapambano dhidi ya ukatili huo, Katibu Mkuu amesema mkakati wa kuboresha uchumi wa kaya kwa kuwawezesha wanawake kushiriki katika uzalishaji mazao ya kimkakati hivyo kuimarika kiuchumi na kushiriki kuzitunza familia zao.
Ameshauri kampeni za kukomesha ukatili zifanyike kwa kushirikisha vyombo vya habari na watu wenye ushawishi katika jamii husika wakiwemo viongozi wa dini ili kuwezesha jamii kutambua tatizo na kuchukua hatua za kulikataa.
Amefafanua kuwa kuna hatua zilizochukuliwa kupitia Mpango kazi wa taifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto MTAKUWWA kuanzia ngazi za chini lakini bado jitihada zaidi zinahitajika kuhakikisha kamati hizo zinafanya kazi kwa ufanisi.
Ameongeza kuwa ni muhimu kuwa na vituo vya malezi na makuzi ya awali ya watoto katika jamii ili waweze kujihusisha na mambo yanayoweza kuwakuza kiakili badala ya kuachwa bila uangalizi na hatimaye kujikuta katika mazingira hatarishi.
Kwa upande wake mtaalamu wa masuala ya haki za watoto kutoka Shirika la Save the Children Dickson Megera amependeleza uwepo wa mfumo wa ufuatiliaji wa matukio ya ukatili wa kijinsia zikiwemo ndoa za utotoni ili kuwezesha jamii kujua na kuchukua hatua dhidi ya vitendo hivyo.
Mratibu wa Mtandao wa TECMN Euphomia Edward ameipongeza Serikali kwa jitihada zake za kuwaunganisha wadau katika mapambano ya kutokomeza vitendo vya ukatili nchini.
“Ni mara chache kukuta viongozi wa ngazi za juu wakiwa na uelewa wa matatizo ya jamii katika ngazi za chini, lakini kwako ni kinyume kabisa na hii inadhihirisha kwamba wewe ni Mzee wa field hivyo na kupongeza sana.” Alisema.
Mtandao wa TECMN unajumuisha Mashirika 64 Yasiyo ya kiserikali ambao unafanya kazi katika ngazi ya kitaifa na kikanda.