………………………………………………………………
Na Mathew Kwembe, Arusha
Timu ya Netiboli ya TAMISEMI QUEENS ambayo inamilikiwa na Ofisi ya Rais TAMISEMI leo imeichakaza timu ya Eagles kutoka jijini Dar es salaam kwa magoli 92-26.
Katika mchezo huo wa kusisimua uliofanyika katika uwanja wa kisasa wa shule ya msingi Ngarenaro jijini Arusha, hadi robo ya kwanza ya mchezo inamalizika TAMISEMI QUEENS walikuwa wanaongoza kwa magoli 17-8.
Katika robo ya pili na tatu, timu ya TAMISEMI QUEENS iliongeza kasi ya mashambulizi katika goli la Eagles na kufanikiwa kujipatia magoli 41 dhidi ya 12 ya Eagles na hadi mwisho wa robo ya tatu ubao ulikuwa unasoma TAMISEMI QUEENS 63 huku Eagles walikuwa na magoli 18.
Nyota wa mchezo wa leo alikuwa ni mfungaji hodari wa TAMISEMI QUEENS Lilian Jovin ambaye alikuwa mwiba katika goli la Eagles.
Mapema kabla ya kufanyika kwa mchezo huo, timu ya JKT Mgulani ya Jijini Dar es salaam ilifanikiwa kuifunga timu ya Arusha Jiji magoli 63-29.
Hadi robo ya mchezo inamalizika JKT Mgulani walikuwa mbele kwa magoli 17-8, na katika robo ya pili JKT Mgulani 38 Arusha Jiji 13, na katika robo ya tatu JKT Mgulani walikuwa wanaongoza kwa magoli 54-19.
Katika mchezo mwingine kati ya uhamiaji na Polisi Arusha mchezo huo ulilazimika kuahirishwa hadi kesho saa 2.00 asubuhi kufuatia giza kutanda kiwanjani hapo katika robo ya pili ya mchezo huku Uhamiaji wakiongoza kwa magoli 23-19.
Mashindano ya Netiboli ligi daraja la kwanza inatarajiwa kuhitimishwa kesho kwa mchezo utakaoamua bingwa wa michuano hiyo mwaka huu kati ya TAMISEMI QUEENS dhidi ya JKT Mbweni katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.
Mgeni rasmi katika mchezo huo anatarajiwa kuwa Naibu Waziri Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe Pauline Gekul.
Jumla ya timu 9 za wanawake na timu 4 za wanaume zimeshiriki mashindano ya kutafuta klabu bingwa ya netiboli mwaka 2021.