Home Mchanganyiko RC MKIRIKITI AAGIZA FORODHA KILANGAWANA SUMBAWANGA KUANZA KAZI

RC MKIRIKITI AAGIZA FORODHA KILANGAWANA SUMBAWANGA KUANZA KAZI

0

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe. Joseph Mkirikiti (kushoto) akiongea na vijana wa kijiji cha Kilangawana wilaya ya Sumbawanga waliozuia msafara wake ili wafikishe kero yao ya kuzuiwa kupita kwenye pori la akiba la Uwanda kwa kutokuwa na forodha l

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe. Joseph Joseph Mkirikiti akiongea na wananchi wa kijiji cha Ilambo  Kata ya Kilangawana Halmasahauri ya Wilaya ya Sumbawanga leo alipofanya ziara ya kikazi kukagua miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa zahanati na kusikiliza kero za mipaka na tatizo la forodha kwenye pori la akiba la Uwanda (TAWA).

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe. Joseph Joseph Mkirikiti (kushoto) akiwa pamoja na viongozi wa wilaya ya Sumbawanga wakibeba nondo maalum kwa ajili ya ujenzi wa nguzo za jengo la utawala la halmashauri ya wilaya ya Sumbawanga iliyopo Laela leo. Akiwa kwenye ziara ya ukaguzi wa mradi huo ,Mkuu wa Mkoa ameonyesha kutoridhishwa na kasi ya ndogo ya ujenzi wa mradi huo tangu mkataba uliposainiwa mwezi Juni mwaka huu ambao utagharimu shilingi Bilioni Moja

 Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe. Joseph Mkirikiti (kushoto) akiongea na wanafunzi wa shule ya Sekondari Lusaka leo (28.07.2021) wakati alipofika kukagua mradi wa ujenzi wa maabara ya shule hiyo iliyopo Wilaya ya Sumbawanga. Akiwa shuleni hapo Mkuu wa Mkoa amewaeleza wanafunzi waongeze bidii kusoma huku wakichukua tahadhari ya ugonjwa wa UVIKO -19

Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Mhe. Sebastian Waryuba (aliyesimama) akizungumza wakati wa kikao cha Mkuu wa Mkoa wa Rukwa  Mhe. Joseph  Mkirikiti (aliyekaa katikati) leo katika kijiji cha Mpona aliptembelea kukagua ujenzi wa zahanati ya kijiji hicho.
(Habari na Picha na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa)

………………………………………………………….

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Joseph Mkirikiti  ametatua mgogoro uliodumu kwa miaka 27 baina  ya wananchi na   pori la akiba Uwanda ambapo wananchi wamekuwa wakizuiwa kupita kwenye pori la akiba la hifadhi wanapokwenda kuvua samaki  Ziwa Rukwa.

Mkirikiti ametoa agizo hilo alipokuwa akiongea na mamia  ya vijana na wananchi wa  kijiji cha Kilangawana na Ilambo kata ya Kilangawana   ambapo ameiagiza halmashauri ya Sumbawanga na hifadhi ya pori la akiba la Uwanda (TAWA) kuanzisha kituo cha forodha kwa ajili ya kukata vibali na ushuru kwenye kijiji hicho hatua itakayoondoa usumbufu wa watu. 

“Kuanzia sasa awepo Afisa Uvuvi hapa Kilangawana atoe huduma ya forodha kwa wavuvi bila kikwazo, nataka TAWA msisumbue wananchi wenye vibali” alisema Mkirikiti

Kijiana Frank Solokoto wa kijiji cha Ilambo alisema kero ya ukosefu wa forodha inawafanya wasafiri umbali mrefu kilometa 40 hadi kijiji cha Legeza kufuata huduma ya forodha na  pia imesababisha askari wa pori la akiba Uwanda kuwakamata na kunyang’anya pikipiki na kudaiwa rushwa.

“Mhe. Mkuu wa mkoa mwaka Jana nilikuwa natoka kuvua samaki nikapita njia inayokatiza kwenye hifadhi ya Uwanda nikakamatwa wakaninyang’anya pikipiki, baada ya kuwapa kiasi  wakaniachia ila wakabaki na pikipiki, kwa kuwa kazi yangu ni kuvua samaki nikatafuta pikipiki ingine ambayo nayo walinikamata nayo, pikipiki hizo zimeuzwa na mahakama, sina kazi hapa sina pesa hata mia ya matumizi naomba msaada wako mkuu!!.” Alisema Frank.

Mkuu wa mkoa huyo baada ya kusikia kilio hicho alimuita Frank na kumpatia shilingi elfu kumi ya matumizi papo hapo huku wananchi wakishangilia kwenye mkutano wa hadhara.

Frank alimshukuru Mkuu wa mkoa na kukiri makosa ya kupita hifadhini kinyume cha Sheria na kuomba ili kuondoa tatizo la wananchi kukamatwa hifadhini serikali ifungue forodha ya Kilangawana.

“Mkuu wa mkoa ahsante sana, forodha ya Kilangawana ikifunguliwa tutaokoa mapato na kuwasaidia wananchi kuondokana na changamoto ya kukamatwa na wahifadhi wa Uwanda, naomba forodha ifunguliwe ya Kilangawana.” Alisema Frank.

Maombi hayo yalipata Baraka ya Kaimu Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Sumbawanga Apolinary Macheta ambaye alimueleza mkuu wa mkoa mkutanoni hapo kuwa hata halmashauri iliwahi kupokea malalamiko hayo na kuyawasilisha kwa maandishi katika ofisi ya maliasili lakini hawajajibu.

Mkuu huyo wa Mkoa yupo kwenye ziara ya kazi kukagua na kuhamasisha shughuli za maendeleo ikiwemo kutoa elimu ya kujikinga na UVIKO-19 kwenye Halmashauri za mkoa wa Rukwa.

Mwisho

Imeandaliwa na:

Afisa Habari

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Rukwa

SUMBAWANGA

28.07.2021