Kutoka Kushoto , Bw. Benedict Nkwao (Afisa Uhusiano-ISW) Bi. Sarah Mbasha Msaidizi wa Mhadhiri kutoka idara ya Taaluma za kazi(-Labour Relations) na Bw. Reid Kabongo afisa Udahili wakitoa huduma katika Banda la Taasisi ya Ustawi wa Jamii kwenye maonesho ya 16 ya Elimu ya Juu viwanja vya Mnazi mmoja Dar es Salaam.
…………………………………
Taasisi ya Ustawi wa Jamii katika kipindi cha mwaka wa masomo 2021-2022 inatarajia kuongeza idadi ya wataalam wa kada mbali mbali inazotoa kwani uhitaji wao katika jamii ni mkubwa sana.
Akiongea na Blogu ya Fullshgwe Mkuu wa Taasisi hiyo Dkt Joyce Nyoni katika maonyesho ya 16 ya Vyuo vikuu vya Sayansi na Teknolojia (TCU) yanayofanyika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam, amesema “Taasisi hiyo inatarajia kuongeza idadi ya wataalam wa malezi na makuzi ya Watoto wadogo na wataalam wa kazi ya jamii kwa vijana na Watoto walio katika kundi rika”.
Taasisi kupitia kozi yake ya mafunzo ya elimu ya malezi na makuzi ya awali ya mtoto na kozi ya cheti cha msingi cha kazi ya jamii kwa vijana na watoto walio katika kundi rika inatarajia kuongeza zaidi wahitimu hawa.
Kampasi ya Taasisi ya Ustawi wa Jamii Kisangara Mwanga Mkoani Kilimanjaro Pamoja na kutoa kozi za ustawi wa jamii ngazi ya cheti cha msingi na ngazi ya stashahada itakuwa ni kitovu cha kutoa kozi hii maalum na yenye uhitaji mkubwa kwa shule nyingi za kulea Watoto yaani Day Care Centers na wazazi na walezi wa Watoto katika mazingira mbali mbali ya jami yetu ya kitanzania.
Kwa upande wake. Mhadhiri Msaidizi wa Taasisi ya Ustawi wa Jamii idara ya taaluma ya Mahusiano ya kazi na menejimenti ya umma kwenye Bi. Sarah Mbasha amesema Taasisi inaendelea kuwa Taasisi pekee ya elimu ya Juu Tanzania kutoa wataalam wabobezi wa usuluhishi na uamuzi na wataalam wa sheria za kazi za kimataifa kuanzia ngazi ya cheti mpaka shahada ya kwanza.
Katika mwaka huu wa udahili 2021-2022 Taasisi imeanza kupokea wanafunzi wa shahada ya uzamili ya kozi ya sheria za kazi, usuluhishi na uamuzi na inategemea kuwa kwa kuzaliwa wataalam katika ngazi hii Taasisi itaandaa wasimamizi wakuu wa kutosha kwa uhitaji katika Nyanja ya sheria za kazi, usuluhishi na uamuzi nchini watakaosaidia kutatua migogoro ya kikazi, kuleta mahusiano mazuri baina ya waajiri na wafanyakazi kwa usimamizi mzuri wa sheria na viwango vya kazi hivyo kuongeza uzalishaji sehemu za kazi,na kupunguza idadi ya migogoro inayoenda tume ya usuluhishi na uamuzi (CMA).
Taasisi ya Ustawi wa Jamii inawakaribisha wahitimu wote kufika katika banda lake katika maonesho hayo ili kupata elimu na maelezo mengi na mazuri kuhusu kozi inazotoa na kuweza kusajiliwa ili kupata nafasi ya masomo katika kozi zake inazofundisha.