**************************
Na Mwandishi Wetu
KAMISHNA wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania(TFS) Profesa Dos Santos Silayo amewataka wananchi wa mkoa wa Ruvuma kujivunia na kuhifadhi chanzo cha maji cha Mto Ruvuma kilichopo katika milima ya Matogoro Manispaa ya Songea.
Hayo ameyasema Julai 26, 2021 mkoani Ruvuma wakati alipoongoza msafara wa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Mary Masanja kupanda msitu wa milima ya Matogoro kwenda kujionea Mapango na Chanzo cha Maji cha Mto Ruvuma ikiwa ni sehemu ya maazimisho ya Tamasha la Majimaji Selebuka linalofanyika wilayani Songea.
“Mto Ruvuma umeubeba Mkoa wa Ruvuma kwa kuwa umepita katika wilaya zote tano ambazo ni Songea, Mbinga, Nyasa, Namtumbo na Tunduru na ni kwa sababu hii wananchi kwa kushirikiana nasi TFS tunapaswa kuuheshimu na kuulinda msitu huu wa Matogoro, machifu wote Kusini huku wanafanya hivyo,” alisema Kamishna Prof. Silayo.
Mhifadhi Mkuu Kanda ya kusini na Kamanda wa Kanda, Manyisye Mpokigwa anasema chanzo cha Mto Ruvuma licha ya kuwa ni muhimu kwa wakazi wa mkoa wa Ruvuma ni kivutio cha utalii kutokana na chanzo hicho kuwa katika mfano wa kisima kidogo ambacho kimetoa mfereji mdogo wenye kazi kubwa ambayo huwezi kuongelea katika hali ya kawaida na kueleweka kwa jamii.
Anasema licha ya udogo wa kisima hicho kidogo ndicho kinachounda mto maarufu duniani unaoitwa Ruvuma ukiwa na urefu za kilometa zaidi ya 800 na upana wa kati ya meta 300 hadi 500 kutegemea na eneo lililopo kwa sababu kuna baadhi ya maeneo mto huo una upana mkubwa zaidi.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Mary Masanja ni miongoni mwa waliokwenda kutalii milima ya Matogolo: “Hii ni safari yangu ya kwanza kufika hapa, ila nimefurahi sana kuona mazingira ya hivi. Mazingira yanavutia, kuna upepo mzuri kileleni na pia kuona chanzo cha mto mkubwa (Ruvuma), inapendeza kwa kweli, tuitunze misitu yetu na tujenge utamaduni wa kutalii, kuna raha sana kupanda milima kama hii, mimi nitaendelea kutumia milima ya TFS kama sehemu ya maandalizi yangu ya kupanda Mlima Kilimanjaro na niwaase wengine kufanya hivyo.”
.