Home Mchanganyiko KWEZI APIGA MARUFUKU WANUNUZI WANAOIBIA WAKULIMA

KWEZI APIGA MARUFUKU WANUNUZI WANAOIBIA WAKULIMA

0
Mbunge wa Jimbo la Kaliua Mkoani Tabora Mheshimiwa Aloyce Kwezi akihutubia wakazi wa kijiji cha Ushokola wilayani humo na kusikiliza kero zao ambapo alilazimika kukaa hadi saa 3 usiku ili kuhakikisha kero zao zote zinapatiwa majibu.  
Na Lucas Raphael,Kaliua

MBUNGE wa Jimbo la Kaliua Mkoani Tabora Aloyce Kwezi (CCM) amepiga marufuku wafanyabiashara wanaoibia wakulima mazao yao kwa kutumia vipimio visivyoendana na uhalisia wa kilo.

Ametoa agizo hilo jana baada ya kusikiliza kero za wananchi katika mikutano ya hadhara aliyoifanya kwa nyakati tofauti katika vijiji vya Imala Upina, Usindi na Ushokola katika kata ya Ushokola wilayani humo.

Alisema kitendo cha baadhi ya wanunuzi wa mazao kulazimisha wakulima wawauzie ndoo ndogo za lita 10 mbili na kuwadanganya kuwa hicho ndiyo kipimo cha debe moja ni udanyanyifu na wizi mtupu.

Alibainisha kuwa mazao kama mahindi, maharage, mpunga au karanga kutumia kipimo cha namna hiyo ni kumwongopea mkulima kwani debe moja inaingia ndoo ndogo ya lita 10 moja na nusu tu.

Kwezi aliagiza Watendaji wote wa Vijiji na Kata na Wenyeviti wa Serikali za Vijiji kuhakikisha vitendo vya namna hiyo vinakomeshwa huku akiwataka kutoa taarifa punde wanapowaona wakijipitisha pitisha kwa wakulima. 

  

Aidha alionya kuwa kama kuna kiongozi yeyote anayeunga mkono au kutumia mwanya huo kuwaibia kwa kununua mazao yao kwa kipimo kama hicho huyo naye hafai kuwa kiongozi, akibainika atachukuliwa hatua za kinidhamu.

‘Mnunuzi anayekuja na vipimio vyake na kukutaka umwekee ndoo 2 kuwa ndiyo debe 1 huyo ni mwizi mkubwa toa taarifa haraka kwa Mtendaji wa Kijiji, Kata au Mwenyekiti, wasipo kusaidia nipigieni simu ili tuwakamate,’ alisema. 

Aliwataka Wenyeviti wa Serikali za Vijiji na Watendaji kuwa makini sana na wafanyabiashara wa namna hiyo kwa kuwa dhamira yao sio nzuri, wanataka kuwanyonya wakulima ili wasinufaike na jasho lao.

‘Sitaki wananchi wangu waibiwe jasho lao, wanatumia nguvu kubwa kulima mazao hayo, wanapaswa kunufaika, yeyote atakayebainika kuwaibia kwa kutumia kipimo hicho, akamatwe na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria’, alisema.

Awali mkazi wa kijiji cha Imala Upina Amos Alberto (45) alisema wakulima wengi wanaibiwa kwa kuwa hawajui uhalisia wa vipimo hivyo, aliomba elimu ya vipimo stahiki itolewa kwa wakulima ili kuepusha utapeli wa namna hiyo.