TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imetoa vibali kwa taasisi na asasi za kiraia 10 kushiriki katika maandalizi ya Uchaguzi Mdogo wa Ubunge Jimbo la Chamwino na Uchaguzi wa Madiwani katika kata 11 za Tanzania Bara.

Kati ya asasi hizo, saba zimepewa vibali vya kutoa elimu ya mpiga kura, huku tatu zikiruhusiwa kushiriki katika uangalizi wa uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni.

Taarifa iliyotolewa leo Oktoba 6, 2026, jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa INEC, Ramadhani Kailima, ilisema uamuzi huo umefikiwa katika kikao cha Tume kilichofanyika siku hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, vibali vya kutoa elimu ya mpiga kura vimetolewa kwa kuzingatia kifungu cha 10(1)(h) cha Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 292, pamoja na Kanuni ya 22(4) ya Kanuni za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi za mwaka 2024.

Asasi zilizopata vibali vya kutoa elimu ya mpiga kura ni New Hope Community Development Organization, Save The Mother And Children Of Central Tanzania, Morogoro Saving The Poor Organization, Njombe Paralegals Centre, Patronage For Persons With Disabilities, Tanzania Child Welfare na The Mwalimu Nyerere Memorial Academy.

Kwa upande wa uangalizi wa uchaguzi, vibali vimetolewa kwa Njombe Paralegals Centre, Save The Mother And Children Of Central Tanzania na Tanzania Child Welfare.

INEC imesema vibali vya uangalizi vimetolewa kwa mujibu wa kifungu cha 85(4) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani, Sura ya 343, pamoja na Kanuni ya 13(4) ya Kanuni za Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani za mwaka 2025.

Tume imezipongeza taasisi na asasi zilizofanikiwa kupata vibali hivyo na kuwataka watekeleze majukumu yao kwa weledi na uadilifu, huku wakizingatia sheria, kanuni na miongozo inayosimamia uchaguzi.

Uchaguzi Mdogo wa Ubunge katika Jimbo la Chamwino, Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino, pamoja na Uchaguzi wa Madiwani katika kata 11 za Tanzania Bara, unatarajiwa kufanyika hivi karibuni kufuatia kuwepo kwa nafasi wazi.