Mchambuzi wa Bajeti ya Serikali katika sekta ya elimu (TYVA) Bw.Arif Fazel akizungumza na waandishi wa habari wakati akitoa matokeo ya uchambuzi wa bajeti ya Serikali katika sekta ya elimu leo Jijini Dar es Salaam. Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Vijana TYVA, Bw.Yusuph Bwango akizungumza na waandishi wa habari wakati wa utoaji wa matokeo ya uchambuzi wa bajeti ya Serikali leo Jijini Dar es salaam. Afisa Miradi wa Friedrich Eiberd Shiftung FES, Bw.Amon Petro akizungumza na waandishi wa habari wakati wakati wa utoaji wa matokeo ya uchambuzi wa bajeti ya Serikali leo Jijini Dar es salaam.
Afisa Miradi wa Shirika la Vijana la TYVA Bw.Luth Kitentya akizungumza na waandishi wa habari wakati akitoa matokeo ya uchambuzi wa bajeti ya Serikali katika sekta ya afya leo Jijini Dar es Salaam.
(PICHA ZOTE NA EMMANUEL MBATILO)
**************************
NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
Katika uchambuzi wa bajeti ya Serikali katika Sekta ya Elimu uliofanywa na Shirika la Vijana la TYVA wamebaini, juhudi za Serikali kuandikisha watoto kwenye shule za awali na shule za msingi zinaridhisha, isipokuwa malengo ya uandikishwaji hayafikiwi kwa ukamilifu kulingana na malengo.
Hayo yamesemwa na Mchambuzi (TYVA) Elimu, Bw.Arif Fazel akiwasilisha uchambuzi huo kwa waandishi wa habari lkeo Jijini Dar es Salaam ambapo amesema hadi February 2021 uandikishaji wa wanafunzi wa elimu ya awali ulifikia wanafunzi 1,057,919 sawa na asilimia 83.14 ya lengo kuandikisha wanafunzi 1,272,503 ikilinganishwa na mwaka 2020 ambapo wanafunzi 1,278,016 sawa na asilimia 92.48 waliandikishwa kati ya lengo la kuandikisha wanafunzi 1,382,761.
“Mwaka 2021 jumla ya wanafunzi 214,594 hawakuandikishwa. Mwaka 2020 jumla ya wanafunzi 104,745 hawakuandikishwa kulingana na malengo ya uandikishwaji”. Amesema Bw.Arif.
Aidha amesema katika elimu ya shule za msingi, hadi February 2021, jumla ya wanafunzi wa darasa la kwanza 1,400,145 sawa na asilimia 92.32 ya lengo la uandikishaji wa wanafunzi 1,516,598 ulifanikiwa ikilinganishwa na mwaka 2020 ambapo wanafunzi 1,526,474 waliandikishwa sawa na asilimia 96 ya lengo la uandikishaji wa wanafunzi 1,597,612.
Amesema katika uandikishaji wa wanafunzi wa darasa la kwanza mwaka 2021 wanafunzi 116,453 hawa kufanikiwa kuandikishwa pia mwaka 2020 wanafunzi 71,138 hawakufanikiwa kuandikishwa sawa na mpango wa Serikali.
Pamoja na hayo, Bw.Arif amesema katika uchambuzi wao wamebaini kuwa kuna upungufu wa miundombinu ya shule za msingi hususan vyumba vya madarasa, madawati, matundu ya vyoo na nyumba za walimu. Kwa mfano hadi Februari 2021 jumla ya vyumba vya madarasa 3,049 vya shule ya msingi vimejengwa na kuongeza idadi ya vyumba vya madarasa kutoka idadi ya vyumba vya madarasa kutoka 125,719 vilivyokuepo Februari 2020 hadi vyumba vya madarasa 128,768.
“Kutokana na idadi ya wanafunzi wa shule ya msingi ambao ni 12,233,628 na idadi ya madarasa ambayo ni 128,768 inapelekea darasa moja kubeba wanafunzi 91”.Ameeeleza Bw.Arif.
Sambamba na hayo amesema kuwa jumla ya matundu ya vyoo 14,581 yamejengwa katika shule za msingi na kuongeza matundu ya vyoo kutoka 205,663 vilivyokuepo Februari 2020 hadi kufikia matundu ya vyoo 220,244 mwezi Februari 2021. Hivyo idadi ya matundu 205 tu ndio yaliongezeka.
Kwa upande wake Mchambuzi TYVA Sekta ya afya , Bw.Luth Kitentya amesema kuwa licha ya serikali kuonyesha juhudi katika mwaka wa fedha 2019/2020 kuweka huduma bora za kinga kwa kutoa chanjo, bado uchambuzi ulibaini kuwa katika bajeti za mwaka wa fedha 2020/2021 na 2021/2022 hakukuwepo na mkazo juu ya utoaji endelevu wa elimu ya umuhimu wa kuzingatia chanjo kwa watoto, wasichana na wajawazito.
Amesema wamebaini kuwa kuna ongezeko dogo zaidi kwa wajawazito kuhudhuria kliniki. Bajeti ya mwaka wa fedha 2021/2022 haijaakisi mahitaji halisi ya juhudi za Serikali kufanikisha zoezi la kuhamasisha wajawazito kuhudhuria kliniki.
“Katika kuimarisha huduma za afya wakati wa ujauzito (Antenatal Care), kwa kipindi cha Julai 2019 hadi Machi 2020, jumla ya wajawazito 1,744,668 walihudhuria kliniki wakati wa ujauzito, kati ya wajawazito 1,822,500 waliotegemewa, ambapo wajawazito 1,343,228 walitimiza mahudhurio manne au zaidi (ANC4+) sawa na asilimia 77 ikilinganishwa na asilimia 41 kwa kipindi kama hicho mwaka 2015/2016”. Amesema Bw.Kitentya.
Nae Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Vijana TYVA, Bw.Yusuph Bwango amesema Shirika hilo limekuwa likifanya uchambuzi wa bajeti za afya na elimu ili kufanikisha uwepo wa bajeti inayoitikia matakwa ya vijana.
Amesema uchambuzi huo ulizingatia mbinu ya mapitio ya nyaraka mbalimbali kama vile vitabu vya bajeti, mpango wa Taifa wa maendeleo wa miaka 5 na kila mwaka, Takwimu za BEST (Basic Education Statistics Tanzania, 2018-2019) na Hotuba za Bajeti za kila mwaka husika.
“Takwimu zinaonesha kuwa idadi ya watu nchini Tanzania imesheheni vijana. Mfumo wa elimu nchini umeumbwa kuwaandaa watoto na vijana kupitia elimu ya awali, msingi, sekondari, vyuo vya ufundi na vyuo vya elimu ya juu”. Amesema Bw.Bwango.