Mbunge wa Jimbo la Babati Vijijini Mkoani Manyara, Daniel Sillo akizungumza na wananchi wa Kata ya Ufana, kwenye ziara yake ya kutembelea Kata zote 25 na kusikiliza kero na changamoto zao na kuzungumza nao.
*************************
Na Mwandishi wetu, Babati
MBUNGE wa Jimbo la Babati Vijijini Mkoani Manyara, Daniel Sillo ameahidi kutoa mabati 110 ili kukamilisha ujenzi wa shule shikizi ya msingi Datar iliyopo kata ya Ufana.
Sillo amesema mabati hayo atayatoa kutoka kwenye fedha za mfuko wa jimbo 2021/2022 ili kuwaondolea wanafunzi adha ya kutembea umbali mrefu na kuwapunguzia msongamano.
Sillo ametembelea shule hiyo ambayo ujenzi wake unaendelea ikiwa ni mwendelezo wa kuzitembelea shule mbalimbali na kutoa misaada ambapo ameshatoa mifuko ya saruji kwenye shule zilizopo jimboni kwake pamoja na mashine za kutolea nakala (photo copy) kwa baadhi ya shule za Sekondari.
Amefanya ziara kwa kata ya Secheda na Ufana ikiwa ni muendeleo wa ziara yake kwa kata zote 25 zilizomo ndani ya Jimbo hilo katika kuwashukuru, kuwasikiliza wananchi, kutatua kero zinazowakabili sambamba na kuwahamasiha juu ya utendaji wa shughuli za kimaendeleo.
Katika ziara hiyo Sillo ameambatana na viongozi wa CCM na wataalamu kutoka idara mbalimbali ili kuweza kubainisha changamoto zinazowakabili wananchi na kuzipatia majawabu ya papo kwa hapo.
Amewahimiza wananchi wa kata hizo juu ya kuwa wamoja na kushirikiana katika kutatua changamoto za kata hiyo na kuwataka kupokea fedha za maendeleo zinazotolewa na serikali ili kuruhusu huduma za kijamii kuendelea.
“Maendeleo yanatokana na ushirikiano wa viongozi na wananchi kwani yanaletwa kwa pamoja na siyo vinginevyo hivyo wananchi wa jimbo la Babati Vijijini tunapaswa kutambua hilo,” amesema Sillo.
Katibu wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Babati Vijijini, George Sanka amewataka viongozi wa vijiji kuwa sehemu ya utatuzi wa migogoro mbalimbali katika maeneo yao.
Sanka amesema viongozi wa vitongoji na vijiji wanapaswa kuwa mstari wa mbele katika kuleta maendeleo huku akisisitiza kuwepo na upendo, shirikiano, amani na umoja Katika kuwatumikia wananchi.