Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Brigadia Jenerali Wilbert Ibuge katikati, akiwa katika picha ya pamoja na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Hamad Chande wa pili kulia, katibu tawala wa mkoa huo Mashauri Ndaki,Mkuu wa wilaya ya Songea Pololet Mgema wa pili kulia na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Songea Michael Mbano.
Picha na Muhidin Amri
………………………………………………………………………….
Na Muhidin Amri,Songea
MKOA wa Ruvuma umefanikiwa kupanda miti milioni 13,989,636 kati ya lengo la kupanda miti milioni 17 sawa na asilimia 82 katika kipindi cha mwaka 2020/2021.
Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Brigadia Jenerali Wilbert Ibuge, amesema hayo wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa shughuli za mazingira kwa Naibu waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Hamad Chande ofisini kwake mjini Songea.
Brigadia Jenerali Ibuge amesema, miti 10,247,000 sawa na asilimia 73.2 imepona na Serikali ya mkoa inaendelea kuhamasisha kampeni ya kitaifa ya upandaji miti inayofanyika kila mwaka kwenye Halmashauri zote.
Aidha amesema, mkoa umekuwa ukiratibu masuala mbalimbali ya usimamizi wa sheria na utunzaji mazingira ikiwa ni pamoja na shughuli za usafi,uhifadhi na utunzaji mazingira,lengo ni kuyafanya mazingira yawe katika hali ya usalama ili kuboresha afya za binadamu na ustawi wa viumbe hai.
Akizungumzia suala la uzalishaji wa taka ngumu katika wilaya zote za mkoa huo amesema,takribani tani 39,596 kwa mwaka zinazalishwa na asilimia kubwa ni za majumbani na sehemu za biashara hasa za masoko.
Kwa mujibu wa Mkuu wa mkoa, taka zinazozalishwa majumbani udhibitiwa kwa njia za mashimo pamoja na utekelezaji kwa moto na Halmashauri zote zimeendelea kutenga maeneo kwa ajili ya uanzishwaji wa madampo ya kutupa taka.
Brigadia Jenerali Ibuge ameongeza kuwa, hata hivyo kutokana na ongezeko la viwango vya maisha na ukuaji wa haraka wa shughuli za maendeleo pamoja na ongezeko la watu,kumesababisha kuongezeka sana kwa uzalishaji wa taka ngumu na maji taka kutoka kwenye makazi ya watu hasa katika Manispaa ya Songea.
Mkuu wa mkoa amesema,ongezeko hilo limesababisha kuwa na uzalishaji mkubwa wa taka ambao hauendani na uwezo wa Manispaa ya Songea kuweza kukusanya taka hizo ambapo kiwango cha taka zinazozalishwa ni tani 71.5 kwa siku.
Kwa upande wake Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Hamad Chande, amepongeza juhudi za Serikali ya mkoa wa Ruvuma ya kupanda miti kwa asilimia 70, na ametaka utaratibu huo uendelee mwaka hadi mwaka.
Aidha, ameagiza Halmashauri zote za mkoa wa Ruvuma kuhakikisha zinapanda miti takribani elfu mbili kwa mwaka ili kukabiliana na uharibifu wa mazingira unaotokana na kuongezeka kwa shughuli mbalimbali za kibinadamu.
Ametaka,suala la kutunza mazingira liwe kama wimbo wa kila siku kwani itasaidia sana wananchi kutambua wajibu na amewataka watendaji wa serikali, kushirikiana na jamii kudhibiti uharibifu wa mazingira na vyanzo vyote vya maji ili viwe endelevu kwa maisha ya binadamu na viumbe wengine.