………………………………………………………………
Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Serikali imeliomba Shirika la Muungano wa Mapinduzi ya Kijani Afrika (AGRA) ambalo linafadhili miradi ya kilimo cha mazao, mifugo na Uvuvi katika halmashauri 30 nchini, kuongeza ufadhili wake kwa halmashauri nyingine 154 ili nazo ziweze kunufaika na miradi inayotokana na ufadhili huo.
Ombi hilo limetolewa leo na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI Prof. Riziki Shemdoe wakati alipokutana na ujumbe wa shirika hilo ulioongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya shirika hilo ambaye ni Waziri Mkuu Mstaafu wa Ethiopia Mheshimiwa Hailemarian Dessalegn.
Prof. Shemdoe amesema kutokana na manufaa ambayo serikali imeyaona katika halmashauri 30 zinazotekeleza miradi hiyo ya kilimo cha mazao, mifugo na Uvuvi ambayo inalenga kuongeza uzalishaji na Usalama wa chakula na kuinua kipato, ipo haja kwa AGRA kuongeza ufadhili katika halmashauri nyingine 154 zilizobaki ili wakulima wa halmashauri hizo nao wanufaike na miradi hiyo.
Katibu Mkuu amesema tangu kuanza kutekelezwa kwa miradi ya kilimo nchini kupitia miradi iliyo chini ya ufadhili wa AGRA, wakulima kutoka halmashauri hizo 30 wamepata manufaa mbalimbali.
Amesema kupitia AGRA kila halmashauri kati ya hizo 30 iliweza kujikita katika kuongeza thamani ya mazao kwa kutoa kipaumbele kwa mazao matatu makuu yanayolimwa katika halmashauri husika.
“Kwa kufanya hivyo, wakulima katika halmashauri hizo siyo tu wataweza kuongeza uzalishaji wa chakula na kuinua kipato chao lakini pia wataweza kuunganishwa na masoko ya uhakika yatakayowawezesha kuuza ziada kwa faida na kuongeza kipato kwenye kaya zao,” amesema Prof. Shemdoe.
Aidha kupitia ufadhili wa AGRA, serikali iliweza kuandaa Mipango ya kuendeleza sekta ya kilimo ya Wilaya katika halmashauri zote 30 kutoka mikoa 12 inayotekeleza miradi hiyo.
Pia serikali imefanikiwa kuanzisha MAJUKWAA ya kuratibu Wadau wa sekta ya Kilimo katka ngazi ya Wilaya katika halmashauri 23 kati ya 30.
Ameongeza kuwa serikali imefanikiwa kuandaa mfumo wa ufuatiliaji na tathmini lakini pia kutafuta Rasilimali fedha kwa ajili ya kutekeleza Mipango hiyo ambapo halmashauri zote 30 kupitia mapato yake ya ndani zimechangia shilingi bilioni 5 katika mwaka huu wa fedha.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi hiyo ya AGRA Mhe. Dessalegn ameelezea kufurahishwa na taarifa ya utekelezaji wa miradi hiyo inayofadhiliwa na shirika lake ambapo amesifu ushirikiano walioupata hapa Tanzania na kwamba amepokea ombi hilo na kuahidi kulifanyia kazi.
Mkutano huo pia ulihudhuriwa na Rais Mstaafu wa Tanzania Mhe.Dkt Jakaya Kikwete, Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe na wataalamu mbalimbali wa serikali kutoka wizara za Kilimo na Ofisi ya Rais TAMISEMI.
Miradi ya kilimo cha mazao, mifugo na Uvuvi inayotekelezwa katika mikoa 12 na halmashauri 30 ina thamani ya Dola za Kimarekani 680,000 na umefadhiliwa na AGRA kwa miaka mitatu kuanzia Novemba 2018 hadi Decemba 2021.
Miradi hii inatekelezwa katika halmashauri za Kiteto, Hanang, Babati vijijini, Arusha dc, Meru dc, Karatu, Hai, Siha na Rombo.
Pia inatekelezwa katika halmashauri za Kilindi, Kilolo, Mufindi, Ludewa, Wanging’ombe, Madaba, Songea dc, Mbinga dc, Sumbawanga dc, Kalambo Nkasi, Mpimbwe, Nsimbo, Tanganyika, Kasulu, Kibondo, Kakonko, Biharamulo, Muleba, Misenyi na Maswa.