Namwandishi
wetu
MFUKO
wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) umepongezwa kwa kuibuka mshindi wa pili katika
kundi la Taasisi za Bima na Hifadhi ya Jamii zilizoshiriki kwenye Maonesho ya
45 ya Kimataifa ya Biashara maarufu kama Sabasaba yaliyofanyika katika viwanja
vya Mwl. Nyerere jijini Dar es Salaam.
Akizungumza
baada ya hafla ya ufungaji wa maonesho hayo, mmoja wa wadau ameeleza kuwa
ushindi huo ni chachu kwa Mfuko kuendelea kutoa huduma nzuri kwa wadau wake
ikiwemo kujitangaza kupitia maonesho na makongamano yanayohusisha wadau tofauti
nchini.
“Nawapongeza
sana WCF kwa kuibuka washindi wa pili, binafsi niliposikia wapo sabasaba
nilisema ni lazima niwatembelee, na kwa kweli wamenihudumia vizuri sana.
Ninashauri wasiishie kushiriki sabasaba tu, waendelee kujitangaza kupitia
makongamano ya wadau, alisema Athuman Saidi, mmoja ya waliotembelea banda la
WCF.
Naye
Mkurugenzi Mkuu wa WCF Dkt. John Mduma,
baada ya kukabidhiwa tuzo hiyo amesema ushindi huo umezidi kuwapa motisha zaidi
kuendelea kutoa huduma za fidia stahiki na kwa wakati pamoja na elimu ya
taratibu za madai ili kuepukana na vikwazo vinavyochangia Mfanyakazi kukosa
sifa ya kulipwa fidia yake.
Pia
ameahidi kufanyia kazi maoni yaliyowasilishwa na wadau waliotembelea banda la
Mfuko huo kwa lengo la kuendelea kuwa mfano wa kuigwa barani Afrika katika
utoaji wa huduma za fidia.
“Katika
maonesho haya tumekuwa washindi wa pili
kwetu ni wajibu mkubwa tumepewa katika kuonesha tofauti kati ya mshindi na
asiyeshinda lakini zaidi ushindi huu unapaswa kuwa na tija katika utoaji wa
huduma za fidia ili kuendelea kuwa mfano wa kuigwa,” amefafanua.
Tuzo
hiyo ilitolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar,
Mhe. Hemed Suleiman Abdulla wakati wa sherehe za kufunga maonesho hayo
zilizoenda sanjari na utoaji wa zawadi kwa washindi wa makundi mbalimbali.
Katika
Maonesho ya 45 kundi la Bima na Taasisi za Hifadhi ya jamii lilijumuisha taasisi za Bima na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii
ambapo maboresho makubwa yaliyochangia WCF kupata ushindi kwa mwaka huu ilikuwa ni pamoja na kutekeleza
mapendekezo ya wadau wa sekta binafsi ya punguzo la viwango vya uchangiaji
pamoja na kuimarisha matumizi ya huduma za kimtandao katika utoaji wa huduma
za Fidia.
Maonesho
haya yaliyobeba kauli mbiu isemayo “Uchumi
wa Viwanda, Ajira na Biashara Endelevu”yalifunguliwa na
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango mnamo
Julai 5, 2021 ambapo nchi mbalimbali zilishiriki maonesho ya mwaka huu ikiwemo
China, Umoja wa Falme za Nchi za Kiarabu (UAE), Marekani na Uturuki.
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dkt. John Mduma (Katikati) akiwasikiliza wananchi waliotembelea kwenye band a la Mfuko huo ili kupata elimu ya fidia wakati wa maonesho ya 45 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam yaliyofikia kilele jana. Mfuko huo umeibuka mshindi wa pili katika kundi la Taasisi za Bima na Hifadhi ya Jamii.