Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa mwaka 2021 Luteni Josephine Mwambashi akikata utepe kuweka jiwe la msingi la kituo cha mafunzo ya kilimo cha Mwendakulima wilayani Kahama
Meneja anayesimamia mradi wa ujenzi wa kituo cha Mafunzo ya Kilimo kinachofadhiliwa na Barrick, Elibariki Jambau akisona risala kwa kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru na viongozi wa mkoa wa Shinyanga
Baadhi ya wafanyakazi wa Barrick katika hafla hiyo
Wafanyakazi wa Barrick na wafanyakazi kutoka sekta mbalimbali za Serikali wakati wa hafla hiyo
***
Mradi wa ujenzi wa kituo cha mafunzo ya kilimo na ufugaji katika kata za Mwendakulima na Mondo unaofadhiliwa na kampuni ya madini ya Barrick,mgodi wa Buzwagi, umeanza kunufaisha wakulima na iwapo watatumia ujuzi wanaopata kituoni hapo watafanikiwa zaidi kwa kuongeza uzalishaji wa mazao na ufugaji wa kisasa.
Hadi sasa mradi huo ambao ulianzishwa mwaka 2018 umeishanufaisha wakulima zaidi ya 3,924 kutoka vijiji 9 katika eneo la Mondo na Mwendakulima katika wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga.
Akiongea wakati wa hafla ya uwekaji wa kuweka jiwe la msingi wa kituo cha Mwendakulima jana uliofanywa na Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2021, Luteni Josephine Mwambashi, Meneja wa mradi huo kutoka Barrick, Bw. Elibariki Jambau, alisema kuwa mradi huo unatekelezwa kwa kipindi cha miaka 5 kuanzia mwaka 2018 na utamalizika mwaka 2023.
Alisema lengo la mradi huo ni kuongeza tija kwa mazao ya kilimo na mifugo vilevile kituo kuwa ni kitovu cha upatikanaji maarifa ya kilimo na taarifa za masoko ya mazao kutoka kwa wataalamu mbalimbali wa Serikali.
Jambau alisema mpaka mradi huu kukamilika utagharimu kiasi cha shilingi milioni 529 na hadi sasa kazi ambazo zimekamilika katika mradi zimegharimu kiasi cha shilingi milioni 138,763,285,00.
“Mpaka sasa kazi zilizokamilika ni upandaji miti ya mbao, ubebeshaji wa miche ya matunda, ujenzi wa kitalu nyumba, ujenzi wa kisima cha maji, ununuzi wa Trekta, Mashine ya kupukuchua mahindi, mpunga, kununua mashine ya kupima unyevu, uzito, pamoja na kutoa mafunzo kupitia mashamba ya mfano kwa wakulima 1,801, sawa na asilimia 46.8 na wakulima waliolengwa.
Mafanikio ambayo yamepatikana hadi sasa alisema ni kuongezeka kwa mavuno ya wakulima kutoka magunia 15 hadi 28 ya mahindi kwa kila ekari na magunia 18 hadi 32 za mpunga, kuwaunganisha wakulima na wadau 17 wa pembejeo na zana za kilimo na masoko 14 ndani na nje ya Kahama, kusambaza miche 69,000 ya miti mbalimbali kwa wakulima pamoja na shule 14.Vilevile vyama 2 vya Ushirika wa mazao (AMCOS) pamoja na uanzishwaji wa vikundi 29 vya uzalishaji”, alisema Jambau.
Aliongeza kuwa shughuli nyingine inayotarajiwa kufanyika katika kituo hiki ni uboreshaji wa koosafu za mifugo kwa kutumia njia ya chupa katika uzalishaji (Uhamilishaji) ili kuboresha ng’ombe wa kienyeji na kupata ng’ombe chotara kwa ajili ya kuongeza tija ya uzalishaji wa maziwa na nyama.
Akiongea baada ya kuweka jiwe la msingi la kituo hicho, Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Luteni Josephine Mwambashi,aliipongeza kampuni ya Barrick kwa kuanzisha mradi huo ambao utanufaisha wakulima wengi na kuwataka wakulima wausimamie uwe endelevu.
Ametoa wito kwa wakulima kuchangamkia fursa ya mafunzo yanayopatikana kituoni hapo ili waweze kupata maarifa yatakayowawezesha kuendesha kilimo cha kisasa na ufugaji wa kisasa ili wapate mavuno mengi.
Akiongea kwa niaba ya wakulima ,Tembo Mihango, mkulima kutoka kijiji cha Penzi kata ya Mondo ,alisema Barrick kwa kuanzisha mradi huu imetekeleza msemo wa “kama unataka kusaidia mtu usimpe samaki bali mfundishe kuvua” kwa kuwa wakulima kwa kupatiwa maarifa wanaweza kujitegemea kutokana na shughuli zao sambamba na kuboresha maisha yao.