*************************
Serikali za Mitaa, Mashirika ya Umma na binafsi nchini wameombwa kujitokeza kupata huduma ya Ushauri elekezi katika masuala yote ya kimaendeleo ili kuweza kupata majawabu kwa baadhi ya changamoto zinawakabili.
Kauli hiyo imetolewa na Prof. Fadhili Mgumia wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini wakati akizungumza katika Maonesho ya 45 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar Es Salaam maarufu Sabasaba yanayoendelea jijini Dar es salaam
Amesema kuwa Chuo hicho kimebobea kwenye masuala ya Utafiti; Mafunzo na Ushauri Elekezi hususani katika nyanja za mipango, mazingira, Biashara, uchumi, utawala, usimamizi wa miradi ya maendeleo, Idadi ya watu, mipango miji, n.k hivyo wahitaji wanakaribishwa kupata hudumu bora na zitakazokidhi mahitaji yao.
Kwa upande wake Afisa Udahili wa Chuo hicho, Bw. Chrisstopher Mdoe, amewakaribisha wahitimu wa nyuma na wale wa kidato cha sita ambao matokeo yao yametoka jana kujiunga na Chuo hicho.
Aidha amewakaribisha wahitaji wote kutembelea banda lao lililopo sabasaba kuweza kujionea programu wanazotoa na kwa watakaochelewa wajitokeza katika maonesho ya vyuo vikuu maarufu TCU yatakayofanyika viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Dar es salaam kuanzia tarehe 26 hadi tarehe 31Julai Mwaka huu.
“Tuna program mbalimbali za masomo tunazozitoa kuanzia ngazi ya cheti moja Diploma,Shahada ya kwanza mpaka ngazi ya Masters na sifa za kujiunga na chuo chetu zipo katika tovuti yetu ya www.irdp.ac.tz”alisema Mdoe