KATIBU Mkuu wa CCM Taifa Daniel Chongolo akizungumza na Wazee wa Chama Cha Mapinduzi Zanzibar katika Afisi Kuu ya CCM Zanzibar kisiwandui.
NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma Mabodi akizungumza kabla ya kumkaribisha Katibu Mkuu wa CCM katika Kikao cha Wazee wa CCM, kilichofanyika Kisiwandui.
BAADHI ya Wazee wa Chama Cha Mapinduzi wakiwa katika kikao hicho cha Katibu Mkuu wa CCM Taifa Daniel Chongolo.
********************
NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa Daniel Chongolo, amesema Chama kitaendelea kuenzi,kulinda na kuheshimu kundi la wazee kwani ndiyo chimbuko la maendeleo yaliyofikiwa hivi sasa ndani ya Chama.
Hayo ameyasema leo katika mwendelezo wa ziara yake visiwani Zanzibar wakati alipokutana na Wazee wa Baraza la Wazee Zanzibar pamoja na wawakilishi wa wazee kutoka katika Wilaya zote za chama cha mapinduzi.
Chongolo, amesema ziara yake hiyo ni ya kujitambulisha tangia ateuliwe kushika nafasi hiyo hivyo amefarijika kukutana na wazee hao kwa lengo la kusikiliza ushauri,maoni na mapendekezo yao ili yaweze kumsaidia katika utekelezaji wa majukumu yake.
Alifafanua kwamba mafanikio yaliyopo hivi sasa ndani ya chama yameasisiwa na wazee hao ambao walifanya kazi kubwa ya kuanzisha taasisi imara ya kisiasa ambayo ni CCM inayotokana na vyama viwili vya ASP na TANU.
‘’Wazee wetu enzi za ujana wenu mlianzisha chama hiki tena kwa kujitolea na mkatuwekea misingi na taratibu imara zinazosababisha leo hii CCM inaheshimika kutokana na nguzo muhimu za kiuongozi,kiutawala na kisiasa mliyoiweka nyinyi’’ alisema Katibu Mkuu huyo Chongolo.
Katika maelezo yake Katibu Mkuu huyo alifafanua kwamba kupitia kitabu cha taratibu za sehemu ya wazee wa CCM toleo la Juni 2019, kimeeleza mambo mbalimbali yakiwemo kurithisha kwa Taifa busara,hekima na ujasiri wao ndani ya jamii.
Alisema pia wana jukumu la kuendelea kuwa mfano bora wa tabia njema kwa Taifa na hivyo kuongoza mafanikio, imani,malengo na madhumuni ya Chama Cha Mapinduzi.
Katibu mkuu huyo, alisema pia wazee wana jukumu la kushauri viongozi wa Chama kwa hekima kuhusu njia bora za ujenzi wa CCM na Taifa.
Aliendelea kufafanua kwamba wazee hao wanatakiwa kuona nchi inaendeshwa kwa misingi ya kudumisha Amani,utulivu,Demokrasia na Uongozi bora.
Pamoja na hayo alisema wanatakiwa kuhifadhi, kukuza na kudumisha Umoja na uzalendo wa Kitaifa pamoja na kuwaunganisha Wazee wote wa CCM katika imani na mwelekeo wa kiitikadi wa Chama.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdulla Juma Mabodi, amesema Wazee hao wamekuwa wakifanya kazi kubwa ya kushauri masuala mbalimbali yenye tija ndani ya Chama na Serikali kwa ujumla.
Alisema ushindi wa CCM katika Chaguzi mbalimbali za Dola na ndogo za majimbo zimetokana na miongozo inayotolewa na Wazee hao kwani wana uzoefu na uwezo mkubwa katika masuala ya kisiasa,kiuchumi na kijamii.
Mapema akifungua kikao hicho Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa CCM Khadija Jabir, alisema wazee hao wapo imara na wanaendelea kushiriki masuala mbalimbali ya Chama Cha Mapinduzi.
Kupitia kikao hicho Mwenyekiti huyo aliahidi kwamba wataendelea kushauri viongozi mambo mbalimbali yatakayoongeza ufanisi zaidi wa kiutendaji na kiuongozi.
Ziara hiyo ya siku mbili ilianza Julai 4 na kuhitimishwa Julai 5,2021 alipokutana na wazee wa CCM,Watumishi wa Chama pamoja na kufanya mazungumzo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Dk. Hussein Ali Mwinyi.