Ili kukidhi Mahitaji ya kitoweo cha nyama inayotokana na wanyamapori na kuendelea na uhifadhi wa wanyama nchini Mamlaka ya Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) tayari imeruhusu kuanzishwa kwa Ranchi zipatazo 5 katika mikoa mbalimbali ili kufuga wanyamapori kwa ajili ya kitoweo.
Hayo yamesemwa katika banda la Maliasili kwenye maonesho ya 45 ya Biashara ya Kimataifa ya Sabasaba yanayoendelea kwenye viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere Barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam
Akizungumza katika maonesho hayo Bw. Alphonce Ambroce Mung’ong’o Kaimu Kamishna Msaidizi Mwandamizi, Huduma za Biashara TAWA amesema Ranchi zilizoanzishwa kwa ajili ya kufuga wanyamapori ni Mwiba Ranch Meatu mkoani Simiyu, Singu Farm mkoani Morogoro, Ilaroi Ranch mkoani Manyara, TPC Moshi, Mkoani Kilimanjaro na ranchi ya Ruhoi River Rufiji mkoani Pwani.
“TAWA imeamua kuanzisha utaratibu wa kufuga wanyamapori kwa ajili ya kitoweo hapa nchini kama ilivyo katika baadhi ya nchi za wenzetu ambao wanafuga wanyamapori kwa ajili ya kujipatia kitoweo,”.
Bw. Alphonce amesema Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) imeamua kuruhusu ranchi hizo za ufugaji wa wanyamapori kuanzishwa ili kukidhi soko la nyamapori, lakini pia kuhakikisha uhifadhi wa wanyamapori nchini unaendelezwa na kuwa katika viwango vinavyotakiwa ili tuendelee kuwa na wanyama wa kutosha katika hifadhi.
Amesema ranchi hizo zitasaidia sana kupata nyama ya kutosha kwa wanohitaji kitoweo kama ilivyo katika nchi kadhaa hapa Afrika kama vile Afrika Kusini ambayo nyamapori inauzwa katika maduka makubwa ya SuperMarket nchi nzima na watu wanaweza kupata kitoweo hicho bila kukosa, lakini uhifadhi wa wanyamapori katika hifadhi zao unaendelea vizuri kabisa.
Ameongeza kuwa nyamapori pia inaweza kupatikana kupitia kwa wawindaji wa vitalu ambao wanapowimnda lengo lao kubwa linakuwa siyo kupata nyama wao mara nyingi wanakuwa wanawinda kwa ajili ya kupata ngozi za wanyama, mafuvu yake au viungo vingine hivyo nyama ile inaletwa kwenye mabucha na wananchi wanaweza kujipatia kitoweo.
Picha mbalimbali zikioneshwa wananchi wakitembelea banda la Maliasili kwenye maonesho ya 45 ya Biashara ya Kimataifa ya Sabasaba yanayoendelea kwenye viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere Barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam.
Simba Dume ambaye yuko katika maonesho ya 45 ya Biashara ya Kimataifa ya Sabasaba yanayoendelea kwenye viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere Barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam kwa ajili ya wananchi kujionea.
Ndege aina ya Tai pia yuko katika maonesho hayo.