.
NA FARIDA SAIDY,MOROGORO.
Jamii imetakiwa kutumia nishati mbadala ili kutunza mizingira kwa kupanda miti kufuatia kuwepo kwa uharibifu wa mazingira unaotokana na shughuli za kibinadamu ikiwemo kilimo cha kuhama hama, kuchoma mkaa, na ufugaji usiozingatia utaalam, ambapo hali hiyo imepelekea kuwepo kwa majanga ya asili yanayotokana na mabadiliko ya tabia nchi.
Rai hiyo imetolewa na Msimamizi wa kampeni ya KESHO TUTACHELEWA Elibarick Simon yenye lengo la kuhamasisha upandaji wa miti na utunzaji wa mazingira hususani kwa vijana, inayosimamiwa na shirika lisilo la kiserikali la Raleigh Tanzania.
Akizungumza kwenye mkutano uliowakutanisha vijana kutoka Raleigh Tanzania walioshiriki katika kampeni tofauti za uhamasishaji utunzaji wa mazingira hapa nchini Elibarick Simon amesema shirika hilo kwa kushirikiana na serikali imeweza kutoa elimu ya utunzaji wa mazingira kwenye jamii.’
Kwa upande wake mwakilishi kutoka wakala wa huduma za misitu nchini Christopher Assenga amesema TFS inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo Raleigh Tanzania katika upandaji wa miti ili kuweza kurudisha uoto wa asili ambao umeharibiwa katika maeneo mbalimbali hapa nchini.
Aidha amewataka vijana kushiriki katika kampeni mbalimbali za upandaji miti hususani katika vyanzo vya maji hali itakayosaidia kuongeza upatikanaji wa maji safi na salama katika maeneo mjini na vijijini hapa nchini.
Nae kiongozi wa maradi wa “Kesho Tutachelewa” Saidi Swalehe amesema mpaka sasa Raleigh Tanzania imepanda miti zaidi ya 85,394 ndani ya mikoa sita na kuwafikia vijana 9,345 ambao walifanikisha zoezi la upandaji miti hiyo katika maeneo mbalimbali hapa nchini.
Pia ameongeza kuwa kupitia matamasha ambayo yalikuwa yanaendeshwa na Raleigh Tanzania wameweza kuwafikia zaidi ya watu 2, 000 wakiwemo wanawake ambao wamekuwa waathirika wakubwa wa mabadiliko ya tabia nchi yatokanayo na uharibifu wa mazingira.