Mkuu wa wilaya ya Ilemela Mhe Hassan Masala akihutubia wafanyabiashara wa soko la samaki la kimataifa la Mwaloni Kirumba,
Mkuu wa wilaya ya Ilemela Mhe Hassan Masala akionyeshwa eneo korofi ndani ya soko la samaki Mwaloni Kirumba na viongozi wa soko hilo
Mkuu wa wilaya ya Ilemela Mhe Hassan Masala akikagua jengo la wafanyabiashara was soko la samaki Mwaloni Kirumba,
********************************
Mkuu wa wilaya ya Ilemela Mhe Hassan Masala ametoa siku ishirini na moja kwa wataalam wa manispaa ya Ilemela kuhakikisha wanatafuta ufumbuzi wa kero na changamoto zinazowakabili wafanyabiashara wa soko la kimataifa la samaki na mazao yake Mwaloni Kirumba
Hayo yamekuja baada ya mkuu huyo wa wilaya kutembelea soko hilo na kuzungumza na wafanyabiashara wa sokoni hapo juu ya kero na changamoto zinazowakabili ili aweze kuzipatia ufumbuzi ambapo kero mbalimbali ziliwasilishwa kwa mkuu huyo wa wilaya ikiwemo uongozi usiofuata sheria na taratibu walizojiwekea, ubadhirifu wa fedha za umma, ulinzi na usalama ambapo akataka kushugulikiwa kwa haraka juu ya kero hizo kwani Mwaloni Kirumba ni soko la kimataifa na chanzo kikubwa cha mapato kwa wilaya ya Ilemela hivyo kuchelewa kushughulikia kero hizo ni kujicheleweshea maendeleo kwani fedha zinazopatikana sokoni hapo ndizo zinazotekeleza miradi ya maendeleo ikiwemo miundombinu ya barabara, huduma za afya na maji
‘.. Mmeomba siku 14, Mie nawaongezea siku 7 jumla ziwe 21 baada ya hapo Mimi nitakuja kuzungumza na wafanyabiashara hawa, Waiteni, Washirikisheni, Zungumzeni nao tujue kipi ni kipi, Asionewe mtu ..’ Alisema
Aidha Mhe Masala akasisitiza wananchi wanaofanya shughuli zao katika soko hilo na viongozi wake kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa Covid-19 kama inavyoshauriwa na wataalam wa afya sanjari na kuwataka kuendelea kumuombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hasan na viongozi wote wa Serikali ya awamu ya sita
Kwa upande wake kaimu mkurugenzi wa manispaa ya Ilemela Ndugu Shukrani Kyando mbali na kuahidi kuyafanyia kazi maelekezo yote yaliyotolewa na mkuu huyo wa wilaya akawataka wananchi kuendelea kuiunga mkono Serikali na kushirikiana nayo katika kumaliza kero zinazowakabili
Nae Meneja wa soko la Mwaloni Kirumba Ndugu Anthony Ndaba akamhakikishia mkuu huyo wa wilaya na wananchi kwa ujumla juu ya utatuzi wa haraka wa kero zilizowasilishwa ambazo ziko ndani ya mamlaka yake ikiwemo suala la usafi wa soko na upatikanaji wa eneo la hifadhi kwaajili ya wanawake wanaofanya shughuli zao ndani ya soko hilo
Mfanya biashara kutoka nchi jirani ya Jamhuri ya watu wa Kongo Ndugu Amani Kabayu akalalamikia uwepo wa baadhi ya wafanyabiashara wasiokuwa waaminifu wanaofanya utapeli kwa wageni kutoka nje ya nchi huku Abubakar Abdallah akilalamikia uendeshwaji usio na weredi wa soko hilo unaofanywa na viongozi wa soko wa sasa ikiwemo kutowasilishwa kwa taarifa za mapato na matumizi, kukaa madarakani muda mrefu, majungu na matumizi mabaya ya rasilimali za soko.