Nteghenjwa Hosseah, OR-TAMISEMI
Katibu Mkuu Prof. Riziki Shemdoe ametangaza ajira za Elimu 6,749 kwa shule za Msingi na Sekondari na Wataalamu wa Afya 2,726.
Akitoa Taarifa hiyo Jijini Dodoma mapema leo hii Prof. Shemdoe amesema waombaji wa kada ya Ualimu walikua 99,583 na Wataalam 37,437 wa kada ya afya, wakiwemo wenye ulemavu 1,099 waliomba nafasi hizo.
“Baada ya kukamilisha taratibu zote za uchakataji wa maombi Walimu 6,949 (3,949 wa shule za Msingi na 3000 wa shule za sekondari) na Wataalam wa kada za afya 2,726 wamepangiwa vituo vya kazi” amesema Prof. Shemdoe
Ametaja vigezo vilivyotumika kuwapata watumishi waliokidhi sifa kuwa ni pamoja na Mwaka wa kuhitimu chuo ambapo waombaji waliomaliza mapema zaidi (mwaka 2012 hadi 2019) kulingana na mahitaji yaliyopo katika kada husika wamepewa kipaumbele.
Aidha, Umri wa mwombaji umezingatiwa kwa kutoa kipaumbele kwa waombaji wenye miaka zaidi ya 40 ambao wamemaliza miaka ya mwanzoni kama ilivyobainishwa kwenye kipaumbele cha awali.
“Sababu ni kuwa kama hawataajiriwa mapema wakifikisha miaka 45 ambapo hawataweza kuajiriwa tena Serikalini kwa ajira ya masharti ya kudumu” amesema Prof. Shemdoe.
Pia waombaji waliofungana kwa sifa zilizobainishwa awali yaani mwaka wa kuhitimu na umri amepewa kipaumbele msichana/mwanamke, bila kuathiri uwiano wa asilimia 50 amefafanua.
Vile vile, Prof Shemdoe amebainisha kuwa endapo waombaji wamefungana kwenye sifa ya Mwaka wa kuhitimu, Umri na Jinsi basi amepewa kipaumbele mwenye umri mkubwa zaidi kwa kuangalia tarehe ya kuzaliwa.
Akitaja changamoto zilizojitokeza wakati wa uchambuzi na kusababisha baadhi ya waombaji kupoteza sifa amesema ni pamoja na Waombaji kutoweka kwa usahihi viambatisho vyote vinavyohitajika kwa mujibu wa tangazo la ajira, waombaji kutofuata maelekezo ya mfumo wa maombi ya ajira, Kutofautiana kwa taarifa za mwombaji alizojaza kwenye mfumo wa maombi ya ajira na taarifa zilizopo kwenye viambatisho pamoja na Waombaji kuandika taarifa zisizo sahihi kuhusu masomo anayoomba kufundisha na yaliyopo kwenye vyeti mafunzo au hati za matokeo.
Prof. Shemdoe ametumia fursa hiyo pia kutoa maelekezo kwa waajiriwa wapya kuwa wanatakiwa kuripoti kwa Wakurugenzi na kufanya kazi kwenye vituo walivyopangiwa na sio katika Makao Makuu ya Halmashauri.
‘Mwajiriwa mpya atakayechukua posho ya kujikimu na baadaye asiripoti katika kituo chake cha kazi alichopangiwa atachukuliwa hatua stahiki kwa mujibu wa sharia na taratibu’ amesema.
Ameongeza kuwa Wajiriwa wapya hawatabadilishiwa vituo vya kazi walivyopangiwa kwa kipindi cha miaka (3) na
wanatakiwa kuripoti katika vituo walivyopangiwa ndani ya siku 14 kuanzia tarehe 1 hadi tarehe 14 Julai, 2021 na ambao hawataripoti kwa muda huo watakuwa wamepoteza nafasi zao na zitajazwa na waombaji wengine wenye sifa waliopo kwenye Kanzi data (Database) ya Ofisi ya Rais – TAMISEMI.
Prof. Shemdoe amewataka waajiriwa wapya kuripoti katika vituo vyao vya kazi wakiwa na Vyeti halisi vya Kidato cha Nne na Sita, Vyeti halisi vya kitaaluma vya kuhitimu mafunzo katika kada husika, Kitambulisho cha Taifa au namba ya utambulisho ya NIDA pamoja na
(Cheti halisi cha kuzaliwa.
Halkadhalika amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri ambazo zimepangiwa waajiriwa wapya kuwapokea na kuwawezesha kwa kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo ya Utumishi wa Umma na baadaye kutoa taarifa ya uripoti wao katika Ofisi ya Rais TAMISEMI.
“Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa wanaelekezwa kukamilisha taratibu za ajira haraka ili watumishi wapya waingizwe kwenye mfumo wa malipo ya mshahara (Payroll) mapema iwezekanavyo” alisisitiza Prof. Shemdoe
Majina ya walimu waliopangiwa vituo vya kazi yanapatikana katika Tovuti ya Ofisi ya Rais-TAMISEMI ya www.tamisemi.go.tz.
Tarehe 6 Aprili, 2021 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan alitoa kibali cha ajira kwa kada za Ualimu na Afya kwa ajili ya kuajiri walimu 6,949 wa Shule za Msingi na Sekondari na wataalam wa Afya 2,726 na kibali hicho kilifuatiwa na tangazo la ajira la tarehe 9 Mei, 2021.