Home Mchanganyiko RC TABORA AWAHIMIZI  WATUMISHI WA OFISI YAKE  NA TAASISI NYINGINE ZA SERIKALI KUTUMIA LUGHA...

RC TABORA AWAHIMIZI  WATUMISHI WA OFISI YAKE  NA TAASISI NYINGINE ZA SERIKALI KUTUMIA LUGHA YENYE STAHA KWA WATEJA

0

Mkuu wa Mkoa wa Tabora Balozi Dkt. Batilda Buriani (kulia)akitoa maelekezo leo wakati wa kikao kazi na watumishi wa Ofisi yake na wale wa Taasisi za umma ambazo ziko katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.Kushoto ni Katibu Tawala Mkoa wa Tabora Msalika Makungu.

Mkuu wa Mkoa wa Tabora Balozi Dkt. Batilda Buriani (kulia)akitoa maelekezo leo wakati wa kikao kazi na watumishi wa Ofisi yake na wale wa Taasisi za umma ambazo ziko katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa

 

Picha na Tiganya Vincent

******************************

NA TIGANYA VINCENT

 

MKUU wa Mkoa wa Tabora Balozi Dkt. Batilda Buriani amewataka watumishi wa Ofisi yake na Taasisi za umma kutumia lugha yenye staha baina yao wenyewe  na Wananchi wanapokuja kupata huduma.

Alisema lugha nzuri ni mojawapo ya tiba na suluhisho la matatizo yanayowakabili Wananchi na inasaidia kutoa huduma bora.

Balozi Dkt. Batilda ametoa kauli hiyo leo wakati wa kikao kazi na watumishi wa Ofisi yake na wale wa Taasisi za umma ambazo ziko katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa. 

Alisema lazima Ofisi ya Mkuu wa Mkoa iwe kitovu cha utoaji wa huduma bora kwa Wateja na Taasisi nyingine zijifunze toka kwao.

Aidha Balozi Dkt. Batilda amesisitiza nidhamu na uadilifu katika mazingira ya kazi na nje ya kazi ,  ubunifu kwenye kazi, bidii . umoja na mshikamano na weledi ili kuacha alama, na kuacha kufanya kazi kwa mazoea.

Aliongeza kila mtumishi lazima awe na Mpango kazi unaoonesha majukumu yake  namna atakavyotekeleza kila siku.

Balozi Dkt. Batilda amewataka Watumishi wa Ofisi yake kuzisimamia kwa karibu na kuzishauri Halmashauri za Mkoa wa Tabora katika Mipango yao ya Maendeleo na kuongeza ukusanyaji wa mapato. 

Aliongeza Dawati la Malalamiko liendelee kusikiliza na kutatua kero na malalamiko ya Wananchi kwa mujibu wa Sheria na taratibu.

Katika hatua nyingine amewataka Watumishi wa Umma na wakazi wa Mkoa wa Tabora kuendelea kuchukua tahadhari za Ugonjwa wa COVID 19 kama inavyoshauriwa na Wataalamu wa Afya.

Alisema kwa sasa Dunia inakabiliwa na Wimbi la Tatu la ugonjwa huo ambapo kila mmoja anafahamu hilo kinachotakiwa ni kuchukua tahadhari zote kwa kuvaa barakoa kwenye maeneo yenye mikusanyiko ya watu, kunawa mikono kwa sabuni na kwa kutumia maji tililika na kupeana nafasi.