Mchezaji Judith Alphonce, wa Mtwara akifunga mojawapo ya pointi katika mchezo dhidi ya Tabora ambapo Mtwara ilishinda seti 3-0
Wachezaji wa timu ya mpira wa wavu Unguja wavulana wakiwa katika pilika pilika ya mchezo wa mpira wa wavu dhidi ya Mara ambapo Unguja ilishinda seti 3-0
Benchi la Ufundi la timu ya wasichana ya mpira wa Volleyball Mtwara likiongozwa na Kocha Gabriel Joshua kulia likifuatilia mchezo kati ya Mtwara dhidi ya Tabora
*****************************
Na Mathew Kwembe, Mtwara
Kama kuna timu ya wasichana ya mpira wa wavu inayoshiriki mashindano ya UMISSETA mwaka huu hapa Mtwara inadhani inaweza kuchukua kombe hilo mwaka huu basi iwaulize timu ya mkoa wa Tabora.
Katika mchezo huo uliochezwa leo asubuhi timu ya Mtwara ikiongozwa na kocha wao Gabriel Joshua iliweza kuisambaratishaTabora baada ya kuilaza kwa seti 3-0.
Jambo la kushangaza katika mchezo wa leo ni pale timu ya wasichana ya Tabora iliposhindwa kupata hata pointi moja katika seti ya pili kwa kukubali kupoteza pointi 25 kwa 0.
Kocha wa Tabora Mwalimu Masingija Muyanga kutoka sekondari ya Mwanzugi anakiri kuwa vijana wake walizidiwa kabisa katika mchezo wa leo licha ya timu yake kushinda michezo yake mitatu ya awali.
“Wenyeji Mtwara wamenizidi kwani wanacheza kwenye uwanja wao wa nyumbani lakini wachezaji wao pia wamekaa muda mrefu na wamekuwa exposed (uzoefu wa kucheza) katika mashindano makubwa,” alisema.
Kauli hiyo iliungwa mkono na nahodha wa timu ya wasichana ya Tabora Flora Frank ambaye anacheza kama ‘seta’ alisema kuwa wachezaji wake walijawa na hofu kutokana na wachezaji wenzao wa Mtwara kuwa na majina makubwa na kushiriki mashindano makubwa kama FEASSA.
Akizungumzia matokeo mazuri ya timu yake kocha wa timu ya wasichana ya Mtwara Gabriel Joshua alisema timu yake imejiandaa vizuri kulitetea kombe hilo na hakuna timu inayoweza kulichukua kombe hilo.
Amesema timu yake ambayo inaundwa na wanafunzi kutoka shule ya sekondari ya Mkalapa ambayo ipo kilometa 35 kutoka mji wa Masasi inafanya mazoezi kila siku kwa ajili ya kujiandaa na mashindano mbalimbali.
Joshua ambaye ni mtumishi wa halmashauri ya mji wa Masasi kama Mkuu wa Idara ya Ardhi na Maliasili katika halmashauri hiyo amesema timu yake inaundwa na wasichana ambao alianza kuwafundisha tangu wakiwa wadogo yaani darasa la nne.
“Baadhi ya wachezaji unaowaona hapa nilianza kuwafundisha volleyball tangu wakiwa darasa la nne na leo nipo nao katika mashindano haya ya UMISSETA na ndoto yangu ni kuwa na timu kali ya Volleyball ambayo haijapata kutokea nchini,” amesema.
Joshua ambaye pia hufundisha timu ya UMITASHUMTA ya wasichana ya mkoa wa Mtwara amesema mkoa wa Mtwara wamekuwa mabingwa wa UMITASHUMTA tangu waliposhiriki mashindano hayo mwaka 2013 huko Kibaha Pwani na amekuwa bingwa wa UMISSETA tangu mwaka 2019.
Amesema siri kubwa ya mafanikio ya timu yake ni mazoezi ya kila siku na kucheza michezo mbalimbali ya ligi kubwa ikiwemo kushiriki ligi ya muungano na mashindano mengine nchini.
Joshua ambaye anasaidiwa na walimu wawili mmoja kutoka shule ya msingi na mwingine sekondari ya Mkalapa anatamani kuiona timu anayoifundisha ikishiriki mashindano ya kimataifa kama Olimpiki na kurudi na medali ya dhahabu.
Kwa upande wao wanafunzi Proscovia Condrad mwenye miaka 15 ambaye anasoma kidato cha pili na mwenzake Lafia Hassan Matandika ambaye yupo kidato cha nne wanasifu uwezo wa Kocha Joshua kwani ameweza kuwafanya wapende mchezo huo na kufanya vizuri darasani katika masomo yao.
“Dada zetu ambao walisoma Mkalapa wamechukuliwa na timu ya JKT, nasi tunatamani kufika huko au zaidi,” amesema Lafia (Kulwa) ambaye pacha wake Lazia (Doto) pia anachezea timu hiyo.
Katika michezo mingine ya Volleyball iliyochezwa leo asubuhi Singida imeifunga Kigoma seti 3-0, Mara ikaifunga Songwe seti 3-0, na Dar es salaam ikaifunga Tanga seti 3-0
Kwa upande wa volleyball wavulana Manyara imeifunga Simiyu seti 3-0, Dar es salaam imeifunga Arusha seti 3-1, Dodoma imefungwa na Tabora seti 0-3, Kigoma imefunga Mbeya seti 3-1, Unguja imeifunga Mara seti 3-0 na Pwani imefungwa na Mwanza seti 0-3.
Katika soka wasichana Iringa na Arusha sare 1-1, Simiyu imeifunga Katavi 1-0, Lindi na Kilimanjaro sare 1-1, Morogoro na Ruvuma sare 1-1, Geita wasichana 3 Dar es salaam 1, Mwanza imewafunga wenyeji Mtwara magoli 3-0 na Rukwa na Lindi wametoka sare 2-2.
Michezo mingine Tabora imeifunga Kagera 2-0, Mara na Kilimanjaro wametoka sare 1-1, Iringa na Arusha sare 1-1, na Manyara imeifunga Dodoma 3-0.
Matokeo ya mchezo wa Netiboli Kagera 23 Manyara 19, Njombe 7 Mara 33, Shinyanga 22 Dar es salaam 29, Tabora 38 Dodoma 19, Rukwa 31 Lindi 15, Arusha 26 Kigoma 27.
Katika mpira wa kikapu wasichana Lindi dhidi ya Arusha magoli 7-73, Kilimanjaro dhidi ya Dodoma 51-23, na Mwana dhidi ya Songwe 47-16.
Matokeo ya mpira wa kikapu kwa wavulana Songwe dhidi ya Kagera 6-27, Dar es salaam dhidi ya Mwanza 28-18, Simiyu dhidi ya Morogoro 20-72 na Unguja dhidi ya Tabora 43-15.