MKUU wa wilaya ya Babati Lazaro Twange,akizungumza leo June 25,2021 wilayani Babati wakati akifungua mafunzo kwa watumishi wa Halmashauri za mkoa wa Manyara akimwakilisha Mkuu wa Manyara, Charles Makongoro Nyerere ambaye ndiye alikuwa mgeni rasmi.
Meneja wa Shirika la viwango Tanzania (TBS) Yona Afrika akisoma taarifa wakati wa mafunzo kwa watumishi wa Halmashauri za mkoa wa Manyara yliyofanyika leo June 25,2021 wialayani Bahati Mkoani Manyara.
MKUU wa wilaya ya Babati Lazaro Twange,akiwa katika picha ya pamoja na washiriki baada ya kufungua mafunzo kwa watumishi wa Halmashauri za mkoa wa Manyara akimwakilisha Mkuu wa Manyara, Charles Makongoro Nyerere ambaye ndiye alikuwa mgeni rasmi.
……………………………………………………………………………….
Na Gift Thadey, Babati
MKUU wa wilaya ya Babati Lazaro Twange amewapongeza Shirika la viwango Tanzania (TBS) kwa kuendelea kuwa walinzi wa afya za watanzania kwa kusimamia ubora wa bidhaa zinazozalishwa.
Twange amewapongeza TBS Mjini Babati wakati akifungua mafunzo kwa watumishi wa Halmashauri za mkoa wa Manyara akimwakilisha mkuu wa Manyara, Charles Makongoro Nyerere ambaye ndiye alikuwa mgeni rasmi.
Twange amesema watumishi hao walioshiriki mafunzo hayo ndio wanasimamia wananchi wengi katika maeneo yao kwa niaba ya TBS.
Aidha amesema wananchi wengi ambao wanawasimamia wanafanyabiashara za aina tofauti.
“Biashara tunafahamu ni maisha ya watanzania hivyo nawashukru TBS kwa kuwa wao ndio walinzi wa afya zetu na shughuli hii iko Duniani kote,” amesema Twange.
Amewataka watumishi ambao wamepata mafunzo hayo kuhakikisha wanasimamia viwango kweli kweli katika maeneo yao ya kazi ili kudhibiti uingizwaji wa bidhaa bandia.
Meneja wa Shirika la viwango Tanzania (TBS) Yona Afrika akisoma hotuba kwa mgeni rasmi alisema mafunzo hayo yameandaliwa na TBS kwa lengo la kutoa mafunzo ili kuwapa walengwa uelewa kuhusu shirika hilo, majukumu yake ikiwemo taratibu za uandaaji wa viwango, matumizi ya viwango na faida zake.
Majukumu mengine ameyataja kuwa ni taratibu za uthibitishaji ubora na usalama wa bidhaa na mifumo yake, vifungashio na usajili wa majengo yanayotumika kwa bidhaa za vyakula na vipodozi.
Meneja huyo amesema shughuli hiyo ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya viwango barani Afrika ambayo hapo awali ilijumuisha kutoa zawadi kwa washindi wa insha.
Afrika amesema zoezi hilo la utoaji wa zawadi lilifanyika katika makao makuu ya Shirika kule jijini Dar es salaam Mei 6, mwaka huu ambapo shindano liliwahusu wanafunzi wa vyuo vikuu nchini.
Meneja huyo amesema maadhimisho hayo ya siku ya viwango barani Afrika hufanyika kila mwaka kwa lengo la kuamsha uelewa miongoni mwa Mamlaka za udhibiti ubora, wazalishaji katika viwanda vikubwa na vidogo, wajasiriamali, taasisi za elimu ya juu na utafiti, walaji na wadau mbalimbali wa viwango kuhusiana na manufaa ya viwango na ubora kwa uchumi endelevu wa nchi yetu na bara la Afrika kwa ujumla.
Kauli Mbiu mwaka huu ni “Nafasi ya uandaaji wa viwango katika kutangaza na kukuza sanaa, utamaduni na urithi,”
Awali ameeleza maana ya viwango kuwa ni nyaraka ambazo hutayarishwa kwa kuzingatia mfumo wa uwazi na ushirikishaji wa wadau mbalimbali wa sekta husika.