Home Michezo MASHINDANO YA RIADHA KURINDIMA MTWARA KUANZIA KESHO

MASHINDANO YA RIADHA KURINDIMA MTWARA KUANZIA KESHO

0

**************************

Na Mathew Kwembe, Mtwara

Mashindano ya riadha ya Umoja wa Shule za Sekondari Tanzania (UMISSETA) inatarajia kuanza kesho katika uwanja wa Chuo cha Ualimu Mtwara huku mojawapo ya wanariadha wanaosubiriwa kwa hamu kushiriki mbio hizo ni Beatrice Innocent Kigulu, ambaye ana mguu mmoja na mkono mmoja.

Kwa mujibu wa Mratibu Msaidizi wa mchezo wa riadha kutoka kamati ya kitaifa inayosimamia mashindano ya UMITASHUMTA na UMISSETA Neema Chongolo, maandalizi yote muhimu kwa ajili ya mashindano ya riadha yamekamilika ambapo mikoa mbalimbali itashiriki michezo hiyo kwa siku 5 kuanzia kesho hadi tarehe 30 juni, 2021.

Chongolo amesema mwanariadha Beatrice atashiriki katika hit no 3 (kundi la 3) la wasichana wenye ulemavu wa viungo ambapo atakimbia na wenzake katika mbio za fainali maalum za mita 100.

Mbali na kundi hilo namba tatu, Chongolo amesema kutakuwa na makundi mengine mawili ya fainali za riadha maalum ambapo wasichana na wavulana watashiriki mbio hizo za mita 100.

Ukiacha fainali maalum, kesho pia kutakuwa na mbio za mita 100 kwa wavulana na wasichana kawaida hatua ya mchuano, kurusha tufe wasichana na wavulana na hiyo itakuwa fainali.

Mratibu huyo msaidizi ameongeza kuwa kesho pia kutakuwa na mashindano yam bio za mita 100 kwa wavulana na wasichana hatua ya nusu fainali, na pia mikoa itakimbia katika relay 4 x 400, mbio za kupokezana kijiti hatua ya mchuano.

Akizungumzia zaidi fainali za mbio maalum kwa wanariadha wenye mahitaji maalum, Chongolo amesema fainali hiyo itaanza saa 12.30 asubuhi katika uwanja wa Chuo cha Ualimu Mtwara ambapo wanariadha wenye uono hafifu watashiriki tofauti na wenzao wenye ulemavu wa viungo.

Naye Mratibu wa michezo ya wanafunzi wenye mahitaji maalum  ya UMISSETA  Mwalimu John Ndumbaro amesema jumla ya wanariadha 11 wenye mahitaji maalum akiwemo Beatrice Kigulu watashiriki fainali hizo.

Amesema washiriki wa riadha ni 11 ukilinganisha na mikoa 28 inayoshiriki UMISSETA mwaka huu, hivyo amewataka waratibu wa michezo kuwabaini wanafunzi wenye mahitaji maalum ambao wana vipaji katika michezo mbalimbali washiriki katika michezo ili waweze kufanya vizuri katika masomo yao.

“Ofisi ya Rais TAMISEMI imetoa nafasi 10 kwa kila mkoa kuleta wanamichezo wenye mahitaji maalum kushiriki mashindano ya UMISSETA ngazi ya taifa lakini mwamko wa mikoa bado upo chini,” amesema.

Mwalimu Ndumbaro anaamini wapo wanamichezo wenye mahitaji maalum wenye vipaji vya hali ya juu huko mikoani na hivyo ametoa wito kwa maafisa michezo wa kila mkoa kuwabaini wanafunzi hao wenye vipaji ili wapate fursa ya kushindana na wanafunzi wenzao kutoka mikoa mingine.

Kwa upande wake mwanafunzi Beatrice Kigulu (15) ambaye anasoma kidato cha pili katika shule ya sekondari makambako amesema anajisikia furaha sana kujumuika na wanafunzi wenzake kushiriki michezo ya UMISSETA na akaahidi kushinda medali hapo kesho.

Mwanariadha huyo mwenye ndoto ya kuwa daktari anaamini kuwa mtu mwenye changamoto kama za kwake anapaswa kujiamini na ndiyo maana muda wote amekuwa ni mtu mwenye uso wa tabasamu mbali ya changamoto kadhaa alizokabiliana nazo.

Beatrice mbali na kushiriki riadha pia ana kipaji kikubwa cha kuimba amesema kutokana na kushiriki UMISSETA amepata marafiki wengi kutoka mikoa mbalimbali na anaishukuru serikali ya awamu ya sita kwa kumpa fursa ya kuonyesha kipaji chake.

Amesema akipata fursa ya kukutana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan atamwambia azidi kuwapa nafasi wanafunzi wenye mahitaji kwani na wao wana nafasi na wana mchango katika jamii.

Mashindano ya riadha ya UMISSETA yatajumuisha mchezo wa kurusha tufe, kurusha kisahani, kurusha mkuki, miruko mitatu, kuruka juu, na kuruka chini 

Pia mbali na mbio za mita 100 na  200 maalum na kawaida, pia kutakuwa na mbio za mita 400 kawaida wavulana na wasichana, mita 800 kawaida wavulana na wasichana, mita 1500 wavulana na wasichana, mita 3000 wavulana na wasichana, pia relay 4x mita 400 wavulana na wasichana na  4x mita 100  kwa wavulana na wasichana.