****************************
Na Gift Thadey, Babati
TIMU 10 za soka za Tarafa ya Mbungwe Wilayani Babati Mkoani Manayara, zinatimua vumbi kwa ajili ya michuano ya Trump Cup inayofanyika kwenye Kata ya Magugu.
Mdhamini wa mashindano hayo Gabriel Lucas Nyange Trump amesema lengo la mashindano hayo ni kuibua, kukuza na kuendeleza vipaji vya vijana wa eneo hilo.
Trump amesema vijana wa eneo hilo kipindi cha jioni wanashiriki michuano hiyo ambayo itasababisha umoja, upendo na mshikamano.
Dwani wa Kata ya Magugu, Filbert Modamba amemshukuru Trump kwa kuwezesha michuano hiyo ambayo ni chachu kwa vijana.
Modamba amempongeza Gabriel Nyange Trump kwa kuanzisha mashindano hayo ya Trump Cup ambayo yamesababisha hamasa kwa vijana kupenda michezo.
Mkuu wa kikosi cha kutuliza ghasia FFU wa Mkoa wa Manyara, Thomas Mbilinyi anasema michuano hiyo itasaidia kupunguza uhalifu kwenye eneo hilo.
Mbilinyi amesema wadau wengine wa michezo wamuige Gabriel Nyange katika kuanzisha mashindano mbalimbali kwenye maeneo tofauti ya mkoa wa Manyara.
“Wadau wengine wa miji midogo ya Galapo, Mirerani, Orkesumet, Kibaya, Katesh na kwingineko waige mfano huu kwa kuwakutanisha vijana pamoja kwenye michezo,” amesema Mbilinyi.
Mwenyekiti wa mashindano hayo ya Trump Cup, Mohamed Kulanjiti amesema timu hizo 10 zimetokea kwenye Kata saba za Tarafa ya Mbungwe.
“Katika timu hizo 10 kila kata imetoa timu moja na nyingine zimetoa timu mbili hadi kufanikisha kuwepo kwa timu hizo zinazoshiriki Trump Cup,” amesema Kulanjiti.