Maafisa wa TBS wakitoa mada kuhusu masuala ya kuzingatia katika uzalishaji wa vifungashio na mifuko mbadala sambamba na utaratibu wa uthibitishaji ubora wa bidhaa wakati wa mafunzo kwa wazalishaji, waagizaji, wasambazaji na wauzaji wa vifungashio na mifuko mbadala yaliyofanyika katika ukumbi wa TMDA Mwanza.
Wazalishaji na wasambazaji wa vifungashio vya plastiki na mifuko wakifuatilia mafunzo kuhusu masuala ya kuzingatia katika uzalishaji wa vifungashio na mifuko mbadala sambamba na utaratibu wa uthibitishaji ubora wa bidhaa yaliyofanyika katika ukumbi wa TMDA Mwanza.
********************
NA MWANDISHI WETU
Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limekutana na wazalishaji, wasambazaji na Vifungashio vya plastiki na mifuko mbadala kwa ajili ya kujadili ni namna gani wanaweza kuzingatia matakwa ya viwango ili kulinda mazingira na mtumiaji wa bidhaa husika.
Lengo la semina ni kutoa elimu kuhusu matakwa ya kiwango husika pamoja na sheria na kanuni za kufuata wakati wa kuzalisha au kuagiza bidhaa hizo, ili kufanikisha lengo hilo TBS imeshirikiana na NEMC katika mafunzo hayo.
Akizungumza baada ya mafunzo hayo Meneja wa Kanda ya Ziwa (TBS) Bw. Joseph Ismail amesema kuwa changamoto iliyopo kwa sasa ni uelewa mdogo kuhusu matakwa ya viwango , sheria na kanuni zinazosimamia ualishaji na uagizaji wa bidhaa za vifungshio vya plastiki vilivyoruhusia na mifuko mbadala.
“Kama huelewi viwango vinataka nini kwa bidhaa husika na pia huelewi sheria na kanuni zinazotakiwa kufuata kabla ya uzalishaji ama uagizaji wa bidhaa husika kuna hatari kubwa ya kuzalisha na kuagiza na kuingiza sokoni bidhaa hafifu jambo litakalo ongeza malalamiko kwa watumiaji wa bidhaa hizo”.
Kwa upende wake Afisa Viwango (TBS) Bw. Johnson Kiwia amesema kuna waagizaji wameanza kuingiza mifuko mbadala isiyofuata matakwa ya viwango sokoni hali inayopelekea uwepo wa malalamiko mengi kutoka kwa watumiaji.
Ukweli ni kwamba sio wote wanaweza kushiriki katika sekta hii ya biashara , watumiaji hutegemea sana wasambazaji ili wawashauri juu ya aina ya ubora wanazozihitaji sokoni na iwapo wazalishaji sasa wamenza kuingiza sokoni mifuko myepesi ambayo haifiki GSM 70 kama matakwa ya kiwango yanavyosema hupelekea mtumiaji kupata bidhaa isiyoendana na mahitaji yake ni hii husababisha uwepo wa malalamiko juu ya thamani ya Maisha yao na fedha zao. Amesema Bw. Kiwia.
Pia Katibu wa Masoko mkoa wa Mwanza Bw. Kurwijila Makubi Athumani, amesema kupitia mafunzo hayo wametambua kanuni na taratibu zinazotakiwa kufuata kabla ya kuzalisha, kuagiza na kusambaza bidhaa za vifungashio vya plastiki vilivyoruhusiwa pamoja na mifumo mbala na ameahidi kuendelea kudumisha uhusiano na TBS ili kuisaidia nchi kuzalisha na kuingiza bidhaa bora na kulinda mazingira na watumiaji.
Pamoja na hayo Afisa Masoko (TBS) Bi. Rhoda Mayugu amewakaribisha wadau mbalimbali wenye maoni na changamoto wanazozipitia kuziwasilisha TBS ili kuzitatua na kuboresha utoaji huduma.