Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Mwanaidi Ali Khamis akikagua bidhaa za wajane katika maadhimisho ya siku ya wajane na duniani yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Mwanaidi Ali Khamis akikagua bidhaa za wajane katika maadhimisho ya siku ya wajane na duniani yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya wajane wakiwa katika maandamano siku ya wajane Dunia yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.
***********
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM.
Serikali imesema imejipanga kuendelea kutatua kero kwa wajasiriamali wakiwemo wajane, mama lishe na wauza mbogamboga kwa kupatiwa maeneo rasmi ya kufanyia biashara yenye ukubwa wa hekta 15,822.64 katika Halmashauri 150 nchini.
Akizungumza jijini Dar es Salaam katika maadhimisho ya siku ya wajane duniani, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na watoto, Mhe. Mwanaidi Ali Khamis, amesema kuwa serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan inawatambua na kuwaenzi wajane katika jamii.
Amesema kuwa juhudi mbalimbali zimefanywa na Serikali ikiwa ni pamoja na kuitambua siku ya Wajane kitaifa na kuhamasisha wadau wote kuiadhimisha na hivyo kuweza kusikiliza na kutatua changamoto zinazowakabili wajane.
Ameeleza kuwa serikali imekuwa ikitoa mikopo ya masharti nafuu kwa wanawake na wajane kupitia vyanzo mbalimbali ikiwemo mikopo yenye thamani ya Shilingi Trilioni 2.22 iliyotolewa kwa vikundi 490,000 vya Wanawake wajasiriamali vyenye wanawake milioni 4.9 kupitia asilimia 4 ya mapato ya ndani ya Halmashauri kwa kipindi cha mwaka 2015 mpaka mwaka 2020.
“Jumla ya kodi, ada na tozo 108 kati ya 139 zimefutwa ili kupunguza kero kwa wanawake wajasiriamali wakiwemo wajane” amesema Mhe. Bi. Khamis.
Amefafanua kuwa benki ya Posta Tanzania imesaidia wanawake kupitia dirisha maalum kwa ajili ya kuhudumia Wanawake.
Kupitia dirisha hilo mikopo yenye thamani ya shilingi Bilioni 22.3 imetolewa kwa Wanawake wajasiriamali wapatao 6,326 kwa kipindi cha kuanzia Julai, 2020 hadi Aprili, 2021 katika Mikoa 26 ya Tanzania Bara.
Ameeleza kuwa kumekuwa na fursa kwa wanawake kuongeza ubora wa bidhaa zao na masoko kwa bidhaa hizo kwa kupata Mafunzo kuhusu urasimishaji na uboreshaji wa bidhaa kwa wanawake wajasiriamali 7,713.
Aidha, wanawake 13,566 wakiwemo Wajane wamewezeshwa kushiriki katika Maonesho ya Biashara ya Kitaifa na Kimataifa yakiwemo maonesho ya Sabasaba, Juakali, Nanenane na VICOBA.
Amesema serikali imeimarisha mifumo ya kulinda haki za Wanawake wakiwemo Wajane kwa Kuanzisha madawati ya jinsia na watoto 427 katika vituo vya polisi; na vituo 153 katika Jeshi la Magereza kwa lengo la kutokomeza ukatili wa Kijinsia kwa Wahanga wakiwemo Wajane.
Pia kumeongezeka kwa huduma za msaada wa sheria kutokana na kutungwa kwa Sheria ya Msaada wa Kisheria Na. 1 ya mwaka 2017, ambapo imewezesha makundi maalum ikiwemo Wajane na watoto kupata haki zao katika vyombo vya usimamizi wa sheria.
Aidha, taasisi 125 za kutoa huduma za msaada wa kisheria zimetambuliwa na wasaidizi wa Kisheria 3,721 wamesajiliwa kote nchini.
“Wanufaika wakubwa wa huduma hizo ni wanawake wakiwemo wajane, kwa mwaka 2018/2019 Serikali ilitoa msaada wa kisheria kwa wajane na hivyo kesi 277 za mirathi ziliweza kutolewa hukumu ya ushindi, hii ni pamoja na uendeshaji wa mashauri na hukumu katika utetezi wa mali” amesema Mhe. Bi Khamis.
Maadhimisho ya mwaka huu 2021 yanafanyika kwa mara ya tatu hapa nchini tangu tulipoanza kuadhimisha siku hii mwaka 2019, ambapo yalifanyika Kitaifa Mkoani Dodoma.
Kwa mwaka huu Maadhimisho haya yanafanyika katika ngazi ya mikoa kwa kuzingatia mazingira ya eneo husika, kama tunavyofahamu Maadhimisho haya hufanyika Kitaifa kila baada ya miaka mitano ili kuwa na muda wa kutosha kutathmini utekelezaji uliofikiwa.
Tanzania huadhimisha Siku ya Wajane kwa lengo la kujenga hamasa, mshikamano na uelewa ndani ya Jamii kuhusu haki na Ustawi wa Wajane. Aidha, maadhimisho haya yanatoa fursa ya pamoja katika kubaini changamoto za wajane na namna ya kukabiliana nazo.
Mwaka huu Maadhimisho ya Siku ya Wajane Duniani yataongozwa na Kaulimbiu “Mapambano Dhidi ya COVID-19: Wajane Washiriki Kikamilifu”. Kaulimbiu hii inahimiza umuhimu wa makundi yote katika Jamii wakiwemo wajane kushiriki katika mapambano dhidi ya COVID-19.