…………………………………………….
WANAKIKUNDI cha Wacha waseme kilichopo Shehia ya Mkungu Wilaya ya Mkoani Pemba wameiomba Serikali na wadau wa maendeleo kuwasaidia mashine ya kusaga mafuta ya mawese ili waweze kuzalisha mafuta hayo kwa wingi kupitia kikundi hicho.
Wamebainisha hayo wakati wa mafunzo ya kutengeneza mafuta ya mawese kwa kutumia njia za asili ambayo yaliandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, TAMWA Zanzibar kwa kuwashirikisha wanakikundi 20 katika kikundi hicho.
Walieleza kwamba kupitia mafunzo hayo waliweza kupata elimu zaidi ya jinsi ya kuvuna na kutengeneza mafuta ya mawese kwa kutumia njia za asili na kusaidia kikundi kujiendeleza zaidi kupitia shughuli hiyo.
Khadija Khamis Kombo ambaye ni mwenyekiti wa kikundi hicho alisema licha ya kikundi kupata elimu ya uzalishaji bora wa mafuta hayo lakini ukosefu wa mashine ya kisasa bado ni kikwazo kwao kuwezesha kukamua mafuta mengi kwa wakati.
“Elimu ya kukamua mafuta tayari tunayo lakini kinachotukwaza tusiweze kukamua mafuta megi zaidi ni kukosa mashine ya kukamulia kwani tunatumia njia za asili kukamua mafuta hayo ,” alisema.
Aidha alibainisha kwamba kutokana na uhitaji wa mafuta hayo kuwa mkubwa kisiwani Pemba inapelekea kushindwa kuwafikia wateja wengi wanayoyahitaji kwa wakati.
Alisema,“uhitaji wa mafuta ya mawese kwasasa hapa Pemba ni mkubwa na soko lipo lakini tunashindwa kulifikia soko hilo kutokana na uzalishaji wake bado haujawa vizuri kwa kukosa nyezo za kuzalishia.”
Katika hatua nyingine alisema kwamba gharama za usagaji wa chikichi ni kubwa kutokana na wamiliki wa mashine kutoza kiwango kikubwa cha pesa kwaajili ya kusaga jambo linalotatiza uendelevu wa kikundi hicho.
Alisema,“tunasagisha mafuta ya chikichi kwa bei kubwa kwani pishi moja tunasagia kwa shilingi elfu moja na ili uweze kupata mafuta lita tano unahitaji kusaga angalau pishi saba ambazo ni sawa na shilingi elfu saba.”
Naye Bashira Abdalla mwanakikundi, alisema bado kuna haja kwa serikali kupitia wizara ya kilimo kuweka mkakati maalumu wa kushajihisha upandaji wa michikichi kutokana na kuwa bado zao hilo halijapewa kipaumbele.
“Changamoto nyingine ambayo bado inatukwaza ni upatikanaji wa miche ya michikichi kwani upatikanaji wake ni shida jambo ambalo linatulazimu kuchukua muda mwingi kutafuta,” alisema.
Aliongeza, “tunaiomba serikali ifanye utafiti na itupatie miche ya kisasa ya michikichi ili tuweze kuzalisha kwa wingi.”
Mapema afisa uwezeshaji wanawake kiuchumi kutoka TAMWA ZNZ, Nairat Abdalla alilisisitiza wanawake Pemba kuendelea kujiingiza katika shughuli za uzalishaji ili kuondokana na utegemezi katika familia.
“Wanawake tuendelee kujikita zaidi katika uzalishaji wa mafuta kwani thamani ya mafuta inapanda kila siku kutokana na uhitaji wake kuongezeka katika jamii.”
Aidha aliomba jamii kuweka utaratibu wa kupanda miche ya mawese ili iweze kupatikana kwa wingi kwaajili ya kuongeza uzalishaji wa mafuta hayo.
Mafunzo hayo ni mwendelezo wa utekelezaji wa mradi wa kuwawezesha wananwake kiuchumi WEZA III unaotekelezwa na TAMWA Zanzibar kupitia ufadhili wa Milele Zanzibar Foundation.