Mratibu wa Mashindano ya UMITASHUMTA na UMISSETA Leonard Thadeo (kushoto mwenye tracksuit ya njano na nyeusi) akiwatambulisha wachezaji wa Netiboli kutoka Zanzibar kwa Mgeni rasmi Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia katika uwanja wa Nangwanda mara baada ya kuyafungua rasmi mashindano ya UMISSETA leo mjini Mtwara
Mgeni rasmi Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Caroline Nombo akizungumza na wachezaji wa Netiboli wa mkoa wa Mara katika uwanja wa Nangwanda mara baada ya kuyafungua rasmi mashindano ya UMISSETA leo mjini Mtwara
Mratibu wa Mashindano ya UMITASHUMTA na UMISSETA Leonard Thadeo (kushoto mwenye tracksuit ya njano na nyeusi) akiwatambulisha wachezaji wa Netiboli kutoka Zanzibar kwa Mgeni rasmi Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia katika uwanja wa Nangwanda mara baada ya kuyafungua rasmi mashindano ya UMISSETA leo mjini Mtwara
**************************
Na Mathew Kwembe, Mtwara
Michezo ya Umoja wa Shule za Sekondari Tanzania (UMISSETA) imefunguliwa leo katika uwanja wa Nangwanda Sijaona mkoani Mtwara ambapo Serikali imeziagiza shule kutenga maeneo maalum kwa ajili ya michezo na sanaa ili kuibua na kuendeleza vipaji vya wanafunzi.
Akifungua mashindano ya 41 ya UMISSETA mjini Mtwara, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Profesa Caroline Nombo amesema Wizara yake itahakikisha kila shule inakuwa na miundombinu yote muhimu kwa ajili ya michezo ikiwemo michezo kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum.
Amesema Wizara itaboresha ufundishaji wa michezo kama vitalu vya vipaji na msingi wa ushiriki endelevu katika michezo kwa afya, elimu, uchumi na ajira.
Amesema serikali imejidhatiti kuendeleza vipaji vya wanafunzi kupitia kufundisha somo la haiba na michezo kwa shule za Msingi, na Elimu kwa Michezo kwa vyuo vya ualimu.
Naibu Katibu Mkuu ameongeza pia kuwa kupitia wadhibiti ubora Wizara itahakikisha kunafanyika tathmini na ushauri wa kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji wa michezo, elimu kwa michezo na sanaa katika taasisi.
Naye Mratibu wa Mashindano ya UMITASHUMTA na UMISSETA Leonard Thadeo amesema michezo yote iliyoshindaniwa wakati wa mashindano ya UMITASHUMTA itakuwepo isipokuwa mchezo wa mpira wa goli ambao haujaanza kushindaniwa katika shule za sekondari.
Michezo itakayoshindaniwa katika UMISSETA ni pamoja na mchezo wa soka wavulana, na wasichana, netiboli, mpira wa mikono wavulana na wasichana, mpira wa wavu wavulana na wasichana, riadha wavulana na wasichana, mpira wa kikapu, na kwaya na ngoma katika sanaa za maonesho.
Jumla ya wanafunzi 3200 kutoka mikoa 28 ya Tanzania ikiwemo mikoa miwili ya Tanzania visiwani wanashiriki mashindano haya ambayo itafanyika kwa siku 11 katika viwanja vya shule ya Ufundi na Chuo cha Ualimu Mtwara.