Home Mchanganyiko WAZIRI AWESO:”ATAKAYESHINDWA KASI YANGU AANDIKE BARUA YA KUACHA KAZI”

WAZIRI AWESO:”ATAKAYESHINDWA KASI YANGU AANDIKE BARUA YA KUACHA KAZI”

0

WAZIRI wa Maji Mhe.Jumaa Aweso ,akizungumza wakati akifungua mafunzo ya maadili kwa viongozi wa umma,kuzuia na Kupambana na Rushwa kwa Viongozi  wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) yaliyofanyika leo June 21,2021 jijini Dodoma.

WAZIRI wa Maji Mhe.Jumaa Aweso,akisisitiza jambo kwa washiriki wa mafunzo ya maadili kwa viongozi wa umma,kuzuia na Kupambana na Rushwa kwa Viongozi wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) yaliyofanyika leo June 21,2021 jijini Dodoma.

Baadhi ya washiriki wakifatilia hotuba ya Waziri wa Maji Mhe.Jumaa Aweso.(hayupo pichani) wakati akifungua mafunzo ya maadili kwa viongozi wa umma,kuzuia na Kupambana na Rushwa kwa Viongozi wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) yaliyofanyika leo June 21,2021 jijini Dodoma.

Mkurugenzi wa Utawala RUWASA Bi.Visensia Kagombora ,akizungumza wakati wa mafunzo ya maadili kwa viongozi wa umma,kuzuia na Kupambana na Rushwa kwa Viongozi wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) yaliyofanyika leo June 21,2021 jijini Dodoma.

Mkurugenzi Usambaji Maji RUWASA Mkama Bwire,akitoa neno la shukrani kwa niaba ya washiriki kwa Waziri  Maji Mhe.Jumaa Aweso mara baada ya kufungua mafunzo ya maadili kwa viongozi wa umma,kuzuia na Kupambana na Rushwa kwa Viongozi wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) yaliyofanyika leo June 21,2021 jijini Dodoma.

Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Mhandisi  Clement Kivegalo,akielezea umuhimu wa mafunzo ya maadili kwa viongozi wa umma,kuzuia na Kupambana na Rushwa kwa Viongozi wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) yaliyofanyika leo June 21,2021 jijini Dodoma.

……………………………………………………………………..

Na Alex Sonna,Dodoma

WAZIRI wa Maji Mhe.Jumaa Aweso amegeuka mbogo kwa Wahandisi ambao wamekuwa wakishindwa kutimiza wajibu wao hivyo amewaomba kama wameshindwa kwendana na kasi yake waandike barua ya kuacha kazi.

Kauli hiyo ameitoa leo June 21,2021 wakati  akifungua mafunzo ya maadili kwa viongozi wa umma,kuzuia na Kupambana na Rushwa kwa Viongozi  wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) yaliyofanyika jijini Dodoma.

 Waziri Aweso amewataka wahandisi kutimiza wajibu wao na kama wameshindwa kwendana na kasi yake waandike barua ya kuacha kazi.

“Unadanganya kwa faida ya nani? Lakini kama unaona wewe huwezi kufanya kazi kwa kasi hii hauwezi kwenda kwa mwenendo huu andika barua tutakusaidia, andika barua kwamba kwa kipindi hichi naomba nipishe lakini hatutagombana na mtu tunataka tukatatue miradi ya maji,”amesema Mhe.Aweso

Pia,amewaonya  Wahandisi hao  kuacha tabia ya uongo na kuwataka kuipa heshima taaluma yao kwa kutatua kero zinazowakabili wananchi.

“Nilichokiona kwa Wahandisi wa maji ni uongo, uongo, uongo, huwezi kuwa Mhandisi wa maji muongo, unaitwa mtaalamu maana yake umesomea kitu kile unatakiwa kujibu kitaalamu lazima uheshimishe taaluma yako.

Vilevile,Aweso amesema Mhandisi atakayekula fedha za maji ajiandae kwenda jela huku akiwataka kuwa wazalendo katika utekelezaji wa miradi.

Amesema Wizara ya Maji haijaajiri vibaka imeajiri wataalamu wenye uwezo hivyo fedha za maji  ukiamua kula jela inakuita,hivyo amewataka kufanya kazi.

“Hivi karibuni nitatoa mkeka sitamuonea mtu wala msiwe na wasiwasi nitawapa majukumu mazito mkafanye kazi, nimeona simu zimekuwa nyingi na wala hamna sababu ya kwenda kwa waganga kuliwa fedha zenu hivyo nitachanganya wahandisi nitatoa wengine wa RUWASA kwenda kwenye Mamlaka za Maji na wa Mamlaka nao watakuja Wakala lengo ni kuleta ufanisi”amesema Aweso

Waziri Aweso amewataka  kufanya kazi na kuachana na visingizio visivyo na ulazima na kusisitiza kuwa kipimo kilichopo kwenye utendaji kazi wao ni kuona matokeo.

Amesema  fahari yao ni kuona wananchi wanapata maji huku akiwataka viongozi hao kuzingatia mafunzo watakayopewa ili kuleta ufanisi na kujiepusha na vitendo vya rushwa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Mhandisi  Clement Kivegalo,amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwaongezea uwezo Wakurugenzi wa Mamlaka za Maji ili waweze kutimiza wajibu wao.

“Kwani Waziri,Naibu Waziri na Katibu Mkuu wanapoenda Mikoani wamekuwa wakikutana na changamoto ambazo watumishi wangefanya kazi kama viongozi matatizo hayo yasingejitokeza hivyo lengo letu la kwanza lilikuwa ni Kuwafundisha wafanye kazi kama viongozi,”amesema

Amesema lengo la pili lilikuwa ni kuwakumbusha kufanya kazi kwa maadili kama maelekezo yanavyomtaka mfanyakazi wa umma huku lengo la tatu likiwa ni kuwakumbusha kuhusu masuala ya rushwa kwani Wizara hiyo imekuwa ikipokea fedha nyingi.

“Na lengo la tatu ni suala la rushwa kwani bado ni tatizo tumeona ipo haya wapate mafunzo kuhusu masuala ya rushwa ili katika  shughuli zao  waepuke rushwa,”amesema

Vilevile,Mhandisi Kivegalo amewaomba  washiriki wa mafunzo hayo kuwa wasikivu  kwa kuwa lengo ni kuwaongezea uwezo kwenye utendaji kazi na kufikia malengo yaliyowekwa ya kufikia asilimia 85 ya wananchi vijijini wawe wanapata maji.