Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako,akizungumza wakati akifungua Kikao cha wadau kuhusu Bodi ya Kitaalamu ya Walimu kilichofanyika jijini Dar es salaam.
Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Leonard Akwilapo,akizungumza wakati akifungua Kikao cha wadau kuhusu Bodi ya Kitaalamu ya Walimu kilichofanyika jijini Dar es salaam.
Baadhi ya wadau wa Elimu wakifatili hotuba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako,(hayupo pichani) wakati akifungua Kikao cha wadau kuhusu Bodi ya Kitaalamu ya Walimu kilichofanyika jijini Dar es salaam.
…………………………………………………………………………
Na WyEST,Dar es Salaam
Serikali iko tayari kupokea maoni na mapendekezo yanayotolewa na wadau juu ya nini kifanyike ili kuboresha sheria na kanuni zinazounda Bodi ya Kitaalamu ya Walimu Tanzania.
Hayo yamesemwa Jijini Dar es Salaam na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako wakati akifungua Kikao cha wadau kuhusu Bodi ya Kitaalamu ya Walimu ambapo amesema lengo ni kuhakikisha utekelezaji wa sheria na kanuni uweze kuleta tija pande zote.
Prof. Ndalichako amesema kuwa mwaka 2018 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipitisha muswada wa sheria ya kuunda Bodi ya Kitaalamu ya Walimu ya Tanzania, ambapo Wizara ya Elimu ilitunga kanuni za kuwezesha utekelezaji wa majukumu ya Bodi hiyo baada ya kusainiwa kwa sheria hiyo.
Kiongozi huyo amesema kuwa baada ya kutungwa kanuni hizo, Chama cha Walimu Tanzania kilielezea kutoridhishwa na baadhi ya vipengele vya kanuni hizo, hivyo Wizara imeona ni vema kuwashirikisha wadau na kuamua kuitisha kikao ambacho kitasikiliza maeneo ya Kanuni na Sheria za Bodi hiyo yanayoonekana yataleta changamoto katika utekelezaji.
“Wizara iko tayari kupokea maoni na mapendekezo yenu kuhusu namna ambavyo kanuni na sheria za Bodi hiyo zinaweza kuboreshwa ili lengo la kuanzishwa kwa Bodi ya Kitaalamu ya Walimu liweze kufanikiwa,” amesisitiza Ndalichako.
Naye rais wa Chama cha Walimu Tanzania(CWT), Leah Ulaya akizungumza katika kikao hicho ameishukuru Serikali kwa kuitisha kikao hicho muhimu na kwamba uanzishwaji wa Bodi hiyo ni mzuri ila wao kama wadau wanaona utekelezaji wa Bodi hiyo umeanza mapema kwani walimu ambao ndio wahusika wakuu bado hawajapata uelewa wa kutosha kuhusu Bodi hiyo.
Akizungumza katika kikao hicho, mmoja wa walimu, Mohamed Mbonde amesema kuwa walimu hawaikatai Bodi ila wanachoomba Serikali iweke kipindi cha mpito kabla ya kuanza rasmi kwa utekelezaji wa kanuni za Bodi. Aidha amesema walimu pia wana wasiwasi wa kuanzishwa kwa Bodi hiyo kwa kuwa wana vyama vingi vinavyowasimamia na vyote vinawakata pesa.