Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato (wa pili kushoto) akikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa usambazaji wa umeme Vijijini Awamu ya Tatu mzunguko wa pili kwa Mkoa wa Kagera uliofanyika katika Kijiji Omurunazi wilayani Muleba Mkoani humo, Juni 19, 2021.
Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato, akizungumza na wakazi wa Kijiji cha Omurunazi wakati wa uzinduzi rasmi wa Usambazaji wa Umeme Vijijini Awamu ya Tatu mzunguko wa pili kwa Mkoa wa Kagera uliofanyika katika Kijiji hicho wilayani Muleba Mkoani humo, Juni 19, 2021.
Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato (kulia) akizungumza na Mbunge wa Jimbo la Muleba Kaskazini, Charles Mwijage wakati wa uzinduzi rasmi wa Usambazaji wa Umeme Vijijini Awamu ya Tatu mzunguko wa pili kwa Mkoa wa Kagera uliofanyika katika Kijiji Omurunazi wilayani Muleba Mkoani humo, Juni 19, 2021.
Mjumbe wa Bodi ya Wakala wa Nishati Vijijini, Mhandisi Styden Rwebangira (kulia) kwa niaba ya Mwenyekiti wa bodi hiyo na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Romanus Lwena (kushoto) wakimsikiliza Naibu Waziri wa Nishati( hayupo pichani) wakati wa uzinduzi rasmi wa Usambazaji wa Umeme Vijijini Awamu ya Tatu mzunguko wa pili kwa Mkoa wa Kagera uliofanyika katika Kijiji Omurunazi wilayani Muleba Mkoani humo, Juni 19, 2021.
Baadhi ya wakazi wa Kijiji Omurunazi pamoja na Wanafunzi wakiwa katika uzinduzi rasmi wa Usambazaji wa Umeme Vijijini Awamu ya Tatu mzunguko wa pili kwa Mkoa wa Kagera uliofanyika katika Kijiji hicho wilayani Muleba Mkoani humo, Juni 19, 2021.
Mbunge wa Jimbo la Muleba Kaskazini, Charles Mwijage (katikati) akishiri moja ya ngoma za asili katika Mkoa wa Kagera wakati wa uzinduzi rasmi wa Usambazaji wa Umeme Vijijini Awamu ya Tatu mzunguko wa pili kwa mkoa huo, uliofanyika katika Kijiji Omurunazi wilayani Muleba, Juni 19, 2021.
Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato (kushoto) akihesabu fedha ili kumkabidhi Mbunge wa Jimbo la Muleba Kaskazini, Charles Mwijage kwa ajili ya kuwalipia wateja 10 wa mwanzo watakaounganishiwa umeme wakati wa uzinduzi rasmi wa Usambazaji wa Umeme Vijijini Awamu ya Tatu mzunguko wa pili kwa Mkoa wa Kagera uliofanyika katika Kijiji Omurunazi wilayani Muleba Mkoani humo, Juni 19, 2021.
…………………………………………………………………….
Na Zuena Msuya, Kagera
Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato, amesema Serikali imetenga shilingi Bilioni 34 zitakazotumika katika Mradi wa kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu mzunguko wa Pili kwa Vijiji 166 ambavyo bado havijafikiwa na Umeme katika Mkoa wa Kagera.
Wakili Byabato, alisema hayo wakati akizindua rasmi mradi huo katika Kijiji cha Omurunazi Wilayani Muleba mkoani humo, uliofanyika Juni 19, 2021.
Alisema kuwa katika kuhakikisha kuwa vijijini vyote vinaunganishwa na Umeme nchini, Mkoa wa Kagera umetengewa fedha hizo ambazo zitatumika katika mradi wa kusambaza umeme kwenye vijiji vyote vilivyosalia katika wilaya Saba za mkoa huo ambao unaotekelezwa kwa kipindi cha miezi 18.
Alifafanua kuwa, kwa Wilaya ya Muleba, ambapo mradi huo umezinduliwa, serikali imetenga shilingi Bilioni 6 ambazo zitatumika kusambaza Umeme katika Vijiji 30, ambapo pia Mkandarasi ametakiwa kuwaunganishia Umeme wateja 400 kwa kuanzia.
“Azma ya Serikali ni kuhakikisha kuwa ifikapo mwakani 2022, vijiji vyote nchini viwe vimeungamishiwa Umeme, hivyo imetoa muongozo kuwa gharama za kuunganisha Umeme mdogo kuwa ni shilingi 27,000 na kwa Umeme mkubwa ni shilingi 139, 500 kwa vijijini ili wananchi wote waweze kumudu gharama za kuunganishiwa umeme, tofauti na ilivyokuwa hapo awali, ni jukumu lenu wananchi kutumia fursa hiyo kuunga mkono juhudi za serikali kwa kulipia gharama hizo”, Alisema Wakili Byabato.
Aidha alizungumzia hali ya kukatika kwa Umeme katika mkoa huo wa Kagera, ambapo alisema kuwa sababu kubwa ni Jiografia ya mkoa huo kuwa na Radi wakati wote ambazo zimekuwa zikisababisha uharibu miundombinu ya umeme.
Hali kadhalika umeme unaohudumia mkoa huo unasafiri umbali mrefu ikiwemo kutoka nchini Uganda na hivyo kupunguza nguvu yake na pia uchakavu wa miundombinu.
Aliweka wazi kuwa ili kukabiliana na changamoto hiyo, vifaa maalumu vinakufungwa katika miundombinu hiyo kupunguza ashari za Radi, na pia vifaa hivyo vitazuia tatizo likitokea eneo moja lisiathiri eneo jingine.
Aliendelea kusema kuwa, suluhisho la kudumu litapatikana hivi karibuni kwa kuwa mkoa huo utaanza kutumia Umeme wa Gridi ya Taifa kwa kutumia umeme utakaozalishwa katika mradi wa kufua umeme wa Rusumo ambao unatarajiwa kukamilika hivi karibuni.
Sambasamba la hilo pia utatumia umeme utakaozalishwa katika mradi wa kufua umeme wa Maragarasi utakaoanza kutekelezwa hivi karibuni na kuufanya mkoa huo kuwa na ziada ya umeme katika matumizi yake.
“Wanakagera endeleeni kuvuta subira, changamoto hii ya umeme inaenda kuisha hivi karibuni, mradi wa Rusumo unakamilika hivi karibuni na kuanza kuzalisha umeme, ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme kutoka katika mradi huo kufika hapa Kagera umeanza kutekelezwa na TANESCO na fedha zipo tayari, tatizo hili muda si mrefu itakuwa historia”, alisisitiza Wakili Byabato.
Vilevile aliliagiza Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) kuweka utaratibu mzuri utakaowawezesha wananchi kulipia gharama za kuunganishiwa umeme kidogokigodo ili kila mmoja aunganishwe, pia aliwataka kuanzisha madawati maalum vijijini ya kulipia gharama hizo ili wananchi wasitembee umbali mrefu kufuata huduma hiyo.
Sambamba na hilo, aliwataka wafanyakazi wa TANESCO kutekeleza majukumu yao kwa weledi pasipo kuathiri mali za watu hasa wanapopita kusafisha njia ya kusafirisha Umeme kwa kuwa kuna baadhi yao wamekuwa wakifyeka na kukata mazao ya wananchi kwa madai kuwa yahaharibu miundombinu ya Umeme.
Aliwaeleza kuwa wanapofanya kazi ya kusafisha njia za kusafirisha umeme ni vyema kuwashirikisha wananchi wa eneo husika ili kupunguza malalamiko ya mara kwa mara kutoka kwa wananchi hao.
Kampuni mbili za wazawa zimepewa dhamana ya kutekeleza mradi huo kwa Mkoa wa Kagera ambazo ni JV Pomy na Qwihaya.
Katika hatua nyingine alizungumzia mradi wa Bomba la mafuta ambapo aliwataka wananchi kuanza kujiandaa kupokea mradi huo na kuchangamkia fursa za kufanya kazi katika maeneo ambayo mradi wa bomba hilo utakapotekelezwa.
Ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi katika Chongoliani mkoani Tanga utaanza hivi karibuni mara baada ya kukamilika kwa taratibu mbalimbali za ujenzi huo, ambapo mradi huo utapita katika mikoa mbalimbali nchini ukiwemo Mkoa wa Kagera.