Waziri wa Afya Dkt. Dorothy Gwajima akionyesha Cheti cha Utumishi Bora alichokabidhiwa Mkurugenzi wa Kitengo Cha Sheria Bw. Merick Luvinga kwenye Banda lililopo ofisi za Wizara jengo la NHIF, Mjini Dodoma mapema leo 18 Juni.
Waziri wa Afya Dkt. Dorothy Gwajima akimkabidhi Cheti cha Utumishi Bora Mkurugenzi wa Kitengo Cha Sheria Bw. Merick Luvinga kwenye Banda lililopo ofisi za Wizara jengo la NHIF, Mjini Dodoma mapema leo 18 Juni.
Waziri wa Afya Dkt. Dorothy Gwajima akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya watumishi wa Wizara hiyo mara baada ya kumkabidhi Cheti cha Utumishi Bora Mkurugenzi wa Kitengo Cha Sheria Bw. Merick Luvinga kwenye Banda lililopo ofisi za Wizara jengo la NHIF, Mjini Dodoma mapema leo 18 Juni.
*****************
Na Catherine Sungura, Dodoma.
WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima kesho 19 Juni, Mwaka huu anatarajiwa kusikiliza kero na malalamiko ya watumishi wa Wizara Kwenye ukumbi wa Wizara mji wa Serikali Mtumba.
Akizungumza wakati wa kuzindua maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma mapema leo mjini hapa, alisema kuwa katika kuadhimisha wiki hiyo, atatumia wasaha huo wa kukutana na watumishi ili kusikiliza kero zao mbalimbali kwa lengo la kuzifanyia kazi.
Kauli mbiu ya maadhimisho hayo mwaka huu ni “Kujenga Afrika tunayoitaka, kupitia utamaduni wa uadilifu ambao unastawisha uongozi wenye maono hata Katika mazingira ya mgogoro.
Vilevile Dkt. Gwajima ameweza kumkabidhi Cheti Cha Utumishi Bora Mkurugenzi wa Kitengo Cha Sheria, Bw. Merick Luvinga Kwenye Banda lililopo ofisi za Wizara jengo la NHIF.
Dkt.Gwajima amesema Wizara imempatia Cheti hicho kilichosainiwa na yeye pamoja na Katibu Mkuu, Prof. Abel Makubi ikiwa ni kutambua kazi nzuri anayofanya wizarani pamoja na Taasisi zingine kwani wameshapokea barua mbalimbali kutoka Wizara na Taasisi nyingine ambazo amekua akifanya nao kazi za kumpongeza Mkurugenzi Luvinga .
Aidha,Dkt. Gwajima amesema wizara yake imejipanga kufanya mambo mbalimbali hivyo ikiwemo kusikiliza wananchi.
“Sisi Wizara ya Afya hapa na Idara na vitengo vyake vyote na ofisi zake mbalimbali kuanzia kule Itega, Area D, Kilimani, Jengo hili la hapa NHIF na maeneo yote zilipo ofisi zetu tutawasikiliza na kuwahudumia wadau wanaokuja kwenye ofisi zetu kufuata huduma wanazozihitaji,
Wananchi wote mnakaribishwa ikiwemo hapa hema la NHIF, mnakaribishwa maalum na mtasikilizwa na kutoa maoni yenu yatasikilizwa kwa kiwango cha hali ya juu wiki hii itakuwa ni maalum na maoni ya kipekee”. Alisema Waziri Dkt. Gwajima
Ameongeza kuwa, Viongozi wote akiwemo Mhe. Naibu Waziri na Naibu Waziri anayeshughulikia Maendeleo ya jamii, Makatibu wakuu na Wakurugenzi wote kuanzia kesho Juni 19 watapita na kutembelea Taasisi ili kukagua huduma zinazotolewa katika maeno mbalimbali katika ofisi zinazohusiana na masuala ya afya katika wiki yote.
“Mimi nitaambatana na viongozi wenzangu kuona nini kinaendelea, wateja wangapi wamefika, wateja wanasema nini, kero ni ngapi, maoni yao, pongezi zao. Lakini pia Juni 22 tutafanya shughuli za usafi kwa wafanyakazi wote wa makao makuu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Dodoma.
“Ni kielelezo tu cha kuonyesha tuliopo makao makuu kama watumishi kuungana na wenzetu walio ‘field’ kufanya zile shughuli ambazo zinafanya maboresho katika kuwavutia na kufanya wateja waridhike pia tutakuwa na namba za simu za watu watatoa kero na pongezi. Alieleza.
Aidha, amewaagiza Wakuu wa vitengo kuwa na majarada ya kero kwani watapita kitengo kimoja baada ya kingine ili baadae waanze upya.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu Wizara hiyo, Prof. Abel Makubi ametaka menejimenti zote kuweza kukagua huduma kwenye hospitali, wodi na kliniki ili waweze kuzitatua kuanzia ngazi ya chini.
“Menejimenti kwenye taasisi zetu zote na Hospitali zifanye usimamizi shirikishi wa kukagua hizo taasisi ama hospitali, kama wewe una tibu basi ndani ya hizi siku tano utenge siku moja ya kutembelea hospitali kwenye wodi, kliniki na kuona kilichopo na baadae itatuliwe kama wanaweza kutatua na kinachoshindikana basi waweze kukiwasilisha juu.”. Alisema Prof. Makubi
Aidha, Amezitaka Bodi zisiwe zinasubiria vikao vya bodi pekee yake, hii ni nafasi sasa watumishi kuwa karibu na bodi, ambapo alisema kuna watumishi wengine hawawezi kuwaeleza menejimenti lakini wanaweza kuongea na wajumbe wa bodi na kuyafanyia kazi.
“Menejiment zisaidiane na ngazi zote kuanzia chini yaani kamati za afya za kijiji, Kata, Wilaya hadi juu.
Pia kutoa elimu kwa wananchi juu ya kupambana na magonjwa ya kuambukiza na yasiyo ya kuambukiza, kwa sasa kuhamasisha kufanya mazoezi, kuchukua hatua za kuepuka magonjwa na mengine.
“Nawaomba watumishi wote pamoja na Serikali tuzingatie kuchukua hatua ikiwemo tishio la COVID 19, ambayo imezikumba nchi za jirani. Hii haitupi wasiwasi kwa kuwa tumeweza kuchukua hatua za muda mrefu, kwa sasa tuendelee kuchukua hatua hasa kwa taasisi zote kuhakikisha wanaweka miundombinu ikiwemo maji, sabuni, na kama kuna uwezo hata vipukusi viwepo, hapo baadae tutaanza kupita kukagua. Hili ni agizo pia kwa Wakurugenzi wa Taasisi,Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya wote.
Prof. Makubi pia ametoa maelekezo hayo kwa Wakurugenzi ambao wapo chini ya Wizara ya afya, ikiwemo makao makuu, Wakuu wa tasisi za mafunzo, huduma, dawa na zingine na Wakurugeni wa hospitali zote kubwa za Taifa, Kanda, Mikoa na Halmashauri zinazotoa huduma, kuanzia kesho wawepo vituoni na kufanya mambo yafuatayo;
“Kuanzia kesho Junu 19, tutakuwa tunapokea kero na malalamiko ya watumishi ndani ya sekta ya afya.
Lakini sio hao tu na taasisi zetu zote ikiweo TMDA, NIMR na zingine kama watumishi watakuwa na shida zao ikiwemo kuhtaji promosheni ama wanaotaka kusoma tumekuwa tukipokea malalamiko mengi lakini mengine yanaweza kutatuliwa tu ngazi ya chini. Alisema.
Aliongeza: “Mnaweza kuyasikiliza huko huko na kuyatolea ufafauzi pasipo kuja Wizarani, kuanzia ngazi ya Zahanati, kituo cha Afya hadi juu, utaratibu huu utakuwa ni wa kila mwezi Afisa utumishi atenge angalau siku moja ya kutatua kero”. Alisema Prof. Makubi.