Home Mchanganyiko TACAIDS YATAKIWA KUONGEZA JUHUDI KATIKA UTENDAJIKAZI WAKE

TACAIDS YATAKIWA KUONGEZA JUHUDI KATIKA UTENDAJIKAZI WAKE

0

Naibu katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, uratibu, Bunge na watu wenye ulemavu, Mhe. Kaspar Mmuya akizungumza na watumishi wa TACAIDS mara baada ya kutembelea katika ofisi za Tume ya kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) leo. 

Baadhi ya watumishi wa tume ya kudhibiti UKIMWI (TACAIDS)wakijitambulisha kwa Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya waziri mkuu Mhe.Kaspar Mmuya alipotembelea leo katika ofisi za TACAIDS kwa lengo la kujitambulisha na kuzungumza na watumishi.

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu uratibu,sera,Bunge na watu wenye ulemavu Mhe.Kaspar Mmuya aliyekaa katikati ,kushoto Kwake ni Mkurugenzi wa rasilimali watu,utumishi na utawala bora wa ofisi ya waziri Mkuu Bw.Greyson Mwaigombe na kulia kwake ni Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TACAIDS Bw.Jumanne Issango waliosimama nyuma ni baadhi ya wajumbe wa Menejiment wa TACAIDS.

********************************

Tume ya kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) imetakiwa kutekeleza majukumu yake kimkakati ili kufikia malengo iliyojiwekea katika uratibu wa mwitikio wa UKIMWI nchini.

Kauli hiyo imebainishwa na Naibu katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, uratibu, Bunge na watu wenye ulemavu, Mhe. Kaspar Mmuya alipotembelea Tume ya kudhibiti UKIMWI na kuzungumza na menejiment pamoja na watumishi ambapo amewataka kuhakikisha wanaratibu vizuri miradi inayotekelezwa na wadau ili kuepusha wadau zaidi ya mmoja kutekeleza miradi yenye lengo la aina moja katika eneo moja.

Mhe. Mmuya amefafanua kuwa wadau wanahitaji kuratibiwa vizuri ili walengwa waweze kunufaika na miradi husika na iwe na mwendelezo ili kupata matokeo yenye tija.

Aidha ameagiza Tume kuhakikisha watu wenye ulemavu wanapewa kipaumbele kwani wanakabiliwa na changamoto mbalimbali zinazowakwamisha kupata huduma za VVU na UKIMWI “Katika taarifa zenu sijaona mahali mlipogusia watu wenye ulemavu namna mnavyo wahudumia hasa katika upataji wa taarifa kulingana na mahitaji yao, hivyo ni muhimu nao wakapewa kipaumbele kwani nao wanahitaji huduma stahili“alisema Mhe Mmuya.

Awali akiwasilisha taarifa ya TACAIDS Mkurugenzi wa utafiti na tathimini Dr Jerome Kamwela,alisema kuwa kwa sasa maambukuzi ya VVU yameshuka kutoka asilimia 5.1 ya mwaka 2011/12 hadi asilimia 4.7 mwaka 2016/17 ambapo maambukizi ya VVU kwa Vijana yanaonekana kuwa zaidi.

Amefafanua kuwa mwaka 2020 maambukizi mapya ya VVU kwa  Watu wazima miaka 15 na zaidi ni takribani 58,000 ambapo , Wanawake  ni 37,000 na Wanaume ni  21,000 Watoto chini ya miaka 15 walikuwa 10,000 wakati watu wazima na watoto walikuwa 68,000.

Aidha vifo vitokanavyo na UKIMWI kwa watu wazima miaka 15 na zaidi ni 24,000 wakati wanaume  ni 11,000 na wanawake  ni 13,000.  Kwa upande watoto chini ya miaka 15 ilikuwa 8,000 jumla ya vifo watu wazima na watoto ilikuwa 32,000

Dr Kamwela ameongeza kuwa Tangu Mpango wa Taifa wa Tiba za UKIMWI uanze mwaka 2004, WAVIU wanaopata huduma za tiba wameendelea kuongezeka.Hadi kufikia Disemba 2019, Asilimia 83 ya WAVIU milioni 1,700,000 walikuwa wanapata huduma za matibabu .Asilimia 92 ya WAVIU wanaopata huduma ya matibabu wamefubaza virusi.

Dr Kamwela ameongeza kuwa kwa sasa Tume inaendelea kukabiliana na makundi yaliyopo katika hatari ya kupata maambukizi ya VVU   hasa jamii za wavuvi,jamii za migodini, watu wanaofanya kazi za kuhama hama, wasichana wanaouza ngono.

Naye Kaimu Mkurugenzi mtendaji wa TACAIDS Bw.Jumanne Issango amemshukuru Naibu Katibu Mkuu kwa kuja kutembelea tume kwani maelekezo aliyoyatoa  yatawekwa kwenye mpango wa utekelezaji  na kuyafanyia kazi ikiwa ni pamoja na kuendeleza uchapaji kazi mzuri katika kuhakikisha  tunafikia malengo tuliyojiwekea.