Ofisa Maliasili wa Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro, John Mtimbanjayo akitoa ufafanuzi kwa maofisa habari kutoka serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali namna kijiji cha Kitunduweta na vingine vinavyonufaika na Isimamizi Shirikishi wa Misitu ya Jamii (USMJ)
Maofisa habari kutoka serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali wakioneshwa choo cha Mwalimu Mkuu Shule ya Msingi Kitunduweta wilayani Kilosa mkoani Morogoro kilichojengwa kupitia mpango wa Isimamizi Shirikishi wa Misitu ya Jamii (USMJ)
Maofisa habari kutoka serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali wakifuatilia kwa umakini maelezo kutoka kwa Mtendaji wa Kijiji cha Kitunduweta wilayani Kilosa mkoani Morogoro, Timothy Lukoo pichani hayupo kuhusu manufaa ya mpango wa Isimamizi Shirikishi wa Misitu ya Jamii (USMJ) kijijini hapo.
Mchoma Mkaa Kulangwa Ganda akitoa ushahidi wa namna amenufaika kamaisha na uhifadhi baada ya mpango wa Usimamizi Shirikishi wa Misitu Jamii (USMJ) kufika kijijini kwao Kitunduweta wilayani Kilosa mkoani Morogoro
…………………………………………………………………………….
Na Mwandishi Wetu
KIJIJI cha Kitunduweta wilayani Kilosa kinatarajia kujenga Zahanati yake kwa kutumia fedha zinazotokana na utekelezaji wa Dhana ya Usimamizi Shirikishi wa Misitu ya Jamii (USMJ).
Hayo yamesemwa na Mtendaji wa Kijiji hicho Thomas Lukoo wakati akitoa taarifa ya Mradi wa Kuhifadhi Misitu kwa Kuwezesha Biashara Endelevu ya Misitu (CoFoREST) kwa maofisa habari kutoka wizara na taasisi mbalimbali walikuwa kwenye ziara ya siku moja.
Mradi huo unatekelezwa na Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania (TFCG) na Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania (MJUMITA) chini ya ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Uswisi (SDC).
Lukoo amesema Kijiji cha Kitunduweta kimetenga shilingi milioni 11.5 za kuanzia ujenzi huo ambao utagharimu shilingi milioni 155.
Amesema ujenzi wa zahanati hiyo ni uendelevu wa kijiji kutekeleza miradi ya maendeleo na huduma za jamii ili kupunguzia wananchi gharama.
“Tumetenga shilingi milioni 11.5 kwa ajili ya ujenzi wa zahanati fedha kutoka kwenye msitu wetu ila ili kukamilika kwa ujenzi huo inahitajika shilingi milioni 155,” amesema.
Mtendaji huyo amesema wanatarajia kukamilisha ujenzi huo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo halmashauri na Hifadhi ya Taifa ya Mikumi (MINAPA).
Lukoo amesema wanatarajia wiki ijayo waanze kuchimba msingi ili kuhakikisha zahanati hiyo inakamilika kwa haraka ili kuhakikisha huduma za afya zinapatikana.
Amesema ujasiri wa kutekeleza miradi mbalimbali inatokana na TFCG na MJUMITA kuwajengea uwezo wanakijiji kutumia rasilimali misitu kwa njia endelevu.
“Tunajenga zahanati ya kisasa lakini huo ni mwendelezo wa ujenzi wa miradi ya maendeleo katika kijiji chetu.
Hadi sasa tumeshakamilisha ujenzi wa nyuma ya mwalimu iliyogharimu shilingi milioni 17, choo shilingi milioni 10 na darasa moja,” amesema.
Aidha, mtendaji huyo amewaomba maofisa habari hao kufikisha ujumbe chanya kwa wafanya maamuzi kuhusu CoFoREST kwani ni mradi ambao umeondoa utegemezi kwenye vijiji kuanzia ngazi ya familia.
Kwa upande wake Katibu wa Wachoma Mkaa kijiji cha Kitunduweta, Kulangwa Ganda amesema mradi huo wamefanikiwa kubadilisha maisha na kutunza mazingira.
Ganda amesema yeye binafsi amenufaika kwa kujenga nyumba, kufikia soko, kusomesha watoto, amefungua duka na kununua pikipiki.
Ofisa Maliasili wa Wilaya ya Kilosa, John Mtimbanjayo amesema mradi huo umefanikiwa kusaidia uboreshaji huduma za jamii katika vijiji huku misitu ikibaki salama.
“Mimi naomba maofisa wenzangu muwe mabalozi wazuri kuhusu mradi huu kwani ni mkombozi wa kiuchumi, kijamii na maendeleo kwa wanavijiji,” amesema.
Ofisa Maliasili wa Wilaya ya Kilosa, John Mtimbanjayo amesema mafanikio USMJ wilayani hapo ni ya kuigwa na kuendelezwa kwenye maeneo mengine.
Kwa upande wao maofisa habari kutoka wizara na taasisi mbalimbali zinahusiana na misitu na uhifadhi wameahidi kupigania USMJ kwa kuwa ina matokeo chanya.