Home Siasa UVCCM LUDEWA WATAKIWA KUTUMIA FURSA ZA KIUCHUMI ZILIZOPO NDANI YA WILAYA HIYO.

UVCCM LUDEWA WATAKIWA KUTUMIA FURSA ZA KIUCHUMI ZILIZOPO NDANI YA WILAYA HIYO.

0

…………………………………………………………………………..

Na Damian Kunambi, Njombe

Vijana wilayani Ludewa mkoani Njombe wametakiwa kuzitumia fursa mbalimbali za kiuchumi zilizopo Katika wilaya hiyo ili kuweza kukuza uchumi wao binafsi na wilaya kwa ujumla.

Hayo ameyasema mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi wilayani humo Theopista Mhagama katika kikao cha kamati ya utekelezaji Baraza Kuu la Umoja wa Vijana Wilaya.

Amesema vijana wanapaswa kuwa na miradi ya kutosha ambapo kwa kufanya hivyo itawasaidia kutotumika kisiasa na viongozi mbalimbali.

Aliongeza kwa kuwahimiza kufanya shughuli mbalimbali za kilimo cha biashara kama kilimo cha parachichi ambapo umoja huo wa vijana tayari wanamiliki shamba la hekari 300 ambalo wanaweza kupanda mazao mbalimbali.

“Tunapaswa kulima mazao ya kimkakati ili tuweze kuinuka kiuchumi, napendekeza tuanze na kilimo cha parachichi hivyo tutakubaliana tulime hekari ngapi na mimi kiongozi wenu nitajitolea miche itakayotosha hekari mbili na miche mingine tutaona namna ya kuipata”, Alisema Mhagama.

Sanjari na suala hilo la kilimo pia amewataka vijana kujipanga katika kutumia fursa mbalimbali zitakazojitokeza ndani ya mradi mkubwa wa Liganga na Mchuchuma pindi utakapoanza ikiwemo kuanzisha miradi ya biashara.

Aidha kwa upande wa katibu wa vijana wilayani humo Baraka Kalinga aliwataka vijana hao kuwatambua vijana wa maeneo yao na kushirikiana nao Katika shughuli za maendeleo.

Amesema endapo watakua karibu na vijana wenzao itawasaidia kujenga ushirikiano ikiwemo kuongeza idadi ya wanachama.

Bakari Mfaume ni katibu wa chama hicho wilayani humo amewaasa vijana hao kutumia kanuni ya KKK ambapo ni Kuwatambua vijana, Kuwaelimisha pamoja na Kuwasikiliza ili kuweza kuleta mshikamano.

Aliongeza kuwa kila mmoja anapaswa kutambua wajibu wake katika chama ili kuleta ufanisi katika kukijenga chama kwani kuna baadhi ya viongozi wanagombea nafasi mbalimbali za uongozi pasipo kujua majukumu anayopaswa kuyatekeleza.

 Mkutano huo ulihudhuliwa na wakuu wa idara mbalimbali za serikali ikiwemo ya kilimo, mifugo, maendeleo ya jamii kwa lengo la kutoa elimu ya ufugaji, kilimo na mikopo ili vijana waweze kunufaika.