Mkufunzi Msaidizi wa Taasisi ya Uhasibu nchini (TIA)Tawi la Singida, Rebecca Sekei akieleza utaratibu na ratiba ya uzinduzi wa Chama cha Wanafunzi wa Uhasibu (ASA) unaotarajia kufanyika kesho kwenye maeneo ya Kampasi hiyo Singida.
Mhadhiri Msaidizi wa TIA Tawi la Singida,Mohamed Kaluse akizungumzia tukio hilo.
Na Godwin Myovela, Singida.
MKUU wa Mkoa wa Singida Dk. Binilith Mahenge kesho jumamosi Juni 19,2021 anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika hafla ya tukio kubwa la uzinduzi wa Chama Cha Wanafunzi wa Uhasibu (ASA) Tawi la Singida.
Uzinduzi huo unaotarajiwa kufanyika kuanzia majira ya saa 3 asubuhi na kusindikizwa na burudani na mada mbalimbali zitakazowasilishwa kutoka Bodi ya Uhasibu Tanzania (NBAA), Mamlaka ya Mapato (TRA), Benki ya NMB, Mkaguzi wa Hesabu za Serikali na wadau wengine.
Mkufunzi Msaidizi wa Taasisi ya Uhasibu nchini (TIA) Tawi la Singida, Rebecca Sekei amesema katika hafka hiyo pamoja na mambo mengine, NBAA watakuwa na jukumu la kutoa mada itakayojikita kuelimisha namna ya uandaaji wa vitabu vya biashara katika sekta binafsi.
Sekei alisema wengine wanaotarajia kutoa mada ni TRA ambao wao watajikita kuelimisha juu ya faida za kuandaa taarifa za biashara kwa wafanyabishara na ulipaji kodi.
Pia alisema katika uzinduzi huo, Benki ya NMB watapata fursa ya kufundisha mada juu ya uwekezaji na usimamizi wa fedha, huku maafisa kutoka Ofisi ya Mkaguzi wa Hesabu za Serikali wanatajiwa kufundisha umuhimu wa ukaguzi wa hesabu kwa taasisi za Serikali.
“Kutakuwa na mambo mengi sana ya kujifunza, bila kusahau masuala yanayohusiana na Bima ya Afya hivyo nawakaribisha wadau wote,” alisema Sekei.
Kwa upande wake, Mhadhiri Msaidizi wa TIA Kampasi ya Singida, Mohamed Kaluse alisema Jumuiya hiyo inayotarajiwa kuzinduliwa azma yake ni kutaka kuwaweka pamoja wanafunzi wa uhasibu ili kukuza na kuendeleza fani hiyo.
Kaluse alisema lengo lingine ni kujenga ukaribu wa mashirikiano baina yake na uongozi wa wanafunzi ndani ya Kampasi ya Singida, na pia kuunganisha na kujenga mahusiano na taasisi mbalimbali za nje katika kuendeleza fani ya uhasibu.
“Kuna faida nyingi za kuanzisha chama hiki kwanza ni kutaka kuendeleza fani yetu na kubadilisha ule mtazamo wa wanachuo kusoma uhasibu ili uajiriwe, badala yake tunataka fani ya uhasibu ijikite katika kutatua changamoto mbalimbali zinazoikumba jamii,” alisema Kaluse.
Pamoja na mambo mengine, imeelezwa, wanachama wa ASA watakuwa na fursa pana ya kuanza kufungua ‘firm’ za kihasibu kama ilivyo kwa mawakili na wanasheria ambazo zinaweza kutoa ushauri wa kitaalamu katika taasisi za umma na binafsi kwa ustawi wa Taifa.
Hata hivyo, Kaluse alibainisha faida nyingine za mwanachama ni kuwa na wepesi katika kutengeneza mazingira mazuri ya kujiajiri na kuajiriwa, kudhaminika,sambamba na kujenga mahusiano ndani ya mnyororo wa thamani kwenye fani hiyo ya uhasibu katika kuingiliana na kufanya kazi kwa pamoja kibiashara.