Mkuu wa Kitengo cha Masoko na Mawasiliano cha benki ya Stanbic Tanzania, Desideria Mwegelo (Kulia)akikabidhi jezi kwa mwenyekiti wa klabu ya Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (Taswa SC) Majuto Omary.
*********************************
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam. Timu ya waandishi wa habari za michezo nchini, Taswa SC inaondoka leo kuelekea Dodoma kwa ajili ya mechi ya kirafiki dhidi ya timu ya wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (Bunge SC).
Mechi hiyo imepangwa kufanyika kesho kwenye uwanja wa Jamhuri ambapo kila timu imetamba kushinda.
Taswa SC ambayo imedhaminiwa na benki ya Stanbic Tanzania, imepania vilivyo na hasa baada ya ushindi wao wa mabao 3-2 dhidi ya timu ya Umoja Road Veterans ya Tabata.
Mwenyekiti wa Taswa SC, Majuto Omary aliema kuwa wamejiandaa vilivyo kwa ajili ya mechi hiyo ambayo itanguliwa na mechi ya netiboli kati ya Bunge Queens dhidi ya Taswa Queens.
“Tumejiandaa vilivyo na tunaishukuru benki ya Stanbic Tanzania ambayo imedhamini safari yetu pamoja na kutupatia vifaa vye michezo,” alisema Majuto.
Alisema kuwa wanatarajia kuendeleza ushindi dhidi ya Bunge SC katika mechi hiyo ambayo inasubiriwa kwa hamu na mashabiki wa soka wa mkoa wa Dodoma na mikoa ya jirani.
Kwa upande wake, timu meneja wa timu ya Bunge SC, Seif Gulamali alisema kuwa maandalizi ya mechi hiyo yamekamilika na wanatarajia kupata ushindi mnono.
Gulamali alisema kuwa wachezaji wake wamejiandaa vilivyo kwa ajili ya mechi hiyo na lengo lao ni kuendeleza wimbi la ushindi.
“Tumejiandaa kupata ushindi katika mechi zote, mpira wa miguu na netiboli, tuna kikosi kipana sana na wachezaji wote wapo katika morali ya hali ya juu,” alisema Gulamali.
Mmoja wa wachezaji wa timu hiyo, Cosato Chumi aka Gaza alisema kuwa wameandaa dozi nene kwa Taswa SC katika mchezo huo. Mbali ya Chumi, pia wachezaji wengine wa timu hiyo ni Ridhwani Kikwete na Festo Sanga.