Rais wa Namibia, Mhe. Hage Geingob akizungumza na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Damas Ndumbaro mara baada ya kufungua rasmi Mkutano wa Kimataifa wa Utalii wa Kanda ya Afrika ulioandaliwa na Shirika la Umoja wa Kimtaifa la Utalii (UNWTO) ulioanza Juni 14, 2021 Jijini Windhoek nchini Namibia, Mkutano huo una lengo la kukabiliana na athrai za UVIKO 19 na kuandaa mikakati madhubuti ya kurejesha sekta ya utalii katika hali ya awali.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Damas Ndumbaro akiwa na baadhi ya Mawaziri wa utalii kutoka nchi mbalimbali za a Afrika wakimfuatilia Rais wa Namibia, Mhe. Hage Geingob wakati akifungua rasmi Mkutano wa Kimataifa wa Utalii wa Kanda ya Afrika ulioandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii (UNWTO) ulioanza Juni 14, Jijini Windhoek nchini Namibia, Mkutano huo una lengo la kukabiliana na athari za UVIKO 19 na kuandaa mikakati madhubuti ya kurejesha sekta ya utalii katika hali ya awali.
Katibu Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii ( UNWTO), Zurab Pololikashvili akizungumza kabla ya kumkaribisha Rais wa Namibia, Mhe. Hage Geingob ambapo amesema moja ya kipaumbele chake ni kuhakikisha nchi za Kiafrika ikiwemo Tanzania ambazo zina vivutio vingi na vya kipekee zinajengewa uwezo katika suala la kutangaza vivutio vya utalii ilivyonavyo ili kuongeza idadi ya watalii na mapato yatokanayo na Watalii.
-Mkutano ujao wa UNWTO kwa Bara la afrika kufanyika Tanzania
Na Mwandishi Wetu, Windhoek, Namibia.
UJUMBE wa Tanzania ukiongozwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Damasi Ndumbaro ambao upo mjini hapa kuhudhuria mkutano wa siku tatu wa Umoja wa Mataifa unaoshughulikia masuala ya Utalii Duniani [UNWTO], ambao ni mahususi kwa nchi za Kiafrika kueweza kujadili na kufanya tafakuri kwa jinsi gani sekta ya Utalii itakavyorejea kwenye mstari wake baada ya kushambuliwa na madhara ya ugonjwa wa UVIKO 19, ambapo Tanzania mkutano ujao imekubaliwa kuwa mwenyeji wa mkutano huo.
Waziri Mhe. Ndumbaro amesema kuwa, ujumbe wa Tanzania umeweza kupata faida mbalimbali sambamba na kupata uzoefu mkubwa ikiwemo pia kutangaza fursa za utalii wa Tanzania katika mkutano huo ambao una aatalaamu Wabobezi Utalii Duniani
‘’Tumekutana nchi nyingi za Kiafrika, tumejadili mambo mengi, tumebadilishana uzoefu mkubwa tumepata mawasilisho mbalimbali kutoka kwenye makampuni ambayo yana uwezo wa juu kabisa wa kutangaza utalii Duniani.
Lakini pia tumepata fursa ya kufanya vikao vya ana kwa ana na wadau mbalimbali moja kati ya wadau hao ni Katibu Mkuu ambaye anayeshughulikia masuala ya Utalii wa umoja wa Mataifa, Zurab Pololikashvili, tumezungumza naye vizuri kabisa na pia amekubali mkutano ujao wa utalii Barani Afrika ufanyikie Tanzania’’. Alisema Mhe. Ndumbaro.
Mhe. Ndumbaro ameongeza kuwa, Katibu huyo pia amekubali yeye mwenyewe binafsi kutembelea Tanzania na kuonana na viongozi mbalimbali wa Kitaifa pamoja na wadau wa utalii kwa ajili ya kufanya maongezi juu ya mustakabali wa Utalii baada ya UVIKO 19.
‘’Lakini muhimu zaidi, tumeweza kuomba na kukubaliwa kuiingiza Tanzania kuwa moja kati ya nchi tatu barani afrika ambazo zitapata mradi wa Umoja wa Mataifa kwenye masuala ya Utalii. Nchi zingine zikiwa Namibia na Cape Vede ambazo zimeshaingizwa toka zamani kwa namna ya kipekee Tanzania tumepewa upendeleo huo baada ya kushiriki hapa na tayari tutaingizwa katika mradi huo mkubwa…’’. Alisema Mhe. Ndumbaro.
Aidha, amesema Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo umepata utaalam na uzoefu mkubwa kwa jinsi gani watakavyoweza kunasuka na ugonjwa huo wa UVIKO 19, amewapongeza watanzania kushiriki na kuweza kufanikiwa.
Katika mkutano huo, leo 16 Juni kutakuwa na Mawaziri 15 kutoka nchi 15 za Afrika ikiwemo Tanzania wapata nafasi ya kuziongelea nchi zao katika mkutano ambao utarushwa moja kwa moja na televisheni mbalimbali za ndani na nje ya Namibia ikiwemo mitandao ya Kijamii.