Na Godwin Myovela, Singida
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa ameagiza sehemu zote zinazolima zao la alizeti ikiwemo mikoa ya Singida, Dodoma na Simiyu kutumia asilimia 10 ya mikopo inayotengwa kwa makundi ya vijana, wanawake na wenye ulemavu kwa kuwapatia mitaji ya mbegu za zao hilo badala ya fedha ili kupanua wigo wa uzalishaji wake, sanjari na kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja kupitia kilimo.
Waziri Mkuu aliyasema hayo juzi mkoani hapa wakati akizindua kampeni ya kitaifa ya kuhamasisha kilimo cha alizeti alipokutana na wadau mbalimbali wa mnyororo wa thamani ya zao hilo kutoka mikoa ya Singida, Dodoma na Simiyu.
“Toeni mitaji ya mbegu kwa makundi haya badala ya fedha. Mana hata wengine mnaowapatia mikopo ya fedha hizo hawarudishi, wapeni mbegu na wasimamieni hii italeta tija kubwa,” alisema.
Waziri Mkuu aliweka bayana faida kubwa ambayo mkulima atanufaika nayo endapo atajikita kwenye kilimo cha alizeti, kuwa pamoja na mambo mengine, mkulima atakayelima ekari moja atatumia wastani wa shilingi 250,000 lakini atakwenda kupata takribani shilingi 1,350,000.
“Mathalani ukilima zao hili Kwa ekari moja utatumia mbegu kilo 2 kwa gharama ya elfu 70, utavuna magunia 15 ya takribani kilo 65 na kwa kila gunia utapata lita 18 za mafuta, na kila Lita Kwa bei ya soko ni shilingi 5000…kwaiyo unakuta unakwenda kupata takribani 1,350,000 ukitoa 250,000 za maandalizi ya shamba hadi kuvuna unajikuta na faida kubwa,” Alisema Waziri Mkuu.
Alihamasisha wakulima kuchangamkia fursa hiyo ili kuinua hali ya vipato vyao lakini pia kutumia zao kama suluhisho la kukabiliana na uhaba wa mafuta ya kula nchini ambapo takribani tani 400,000 hulazimika kuagizwa nje ya nchi ili kutosheleza mahitaji.
Alisema uwezo wa nchi kwa sasa ni kuzalisha tani 290,000 pekee huku akisisitiza kiasi hicho ni sawa na asilimia 45 ya jumla ya tani zipatazo 650,000 zinazohitajika nchini.
“Nchi huagiza tani zipatazo 400,000 kufidia upungufu wa mafuta ya kula kwa gharama ya shilingi bilioni 474 kila mwaka kwa takwimu za sasa,” Alisema Waziri Mkuu.
Alisema mkakati wa Serikali uliopo ni kuongeza uzalishaji wa mazao ya mafuta yakiwemo alizeti, chikichi, pamba, karanga na ufuta ili kujitosheleza na kuondokana ya adha ya uagizaji wa mafuta ya kula kutoka nje.
Kuhusu mkakati uliopo wa kuinua tija ya kilimo cha alizeti, pamoja na mambo mengine, Waziri Mkuu amewataka Wakuu wa Mikoa kuandaa mpango mkakati ikiwemo kutenga maeneo mahususi kwa ajili ya kilimo cha zao hilo.
Aidha, aliwaagiza wakuu hao wa Mikoa kuhakikisha kila Taasisi na mashule wanaweka mara moja utaratibu wa kuanza kuzalisha alizeti, jambo ambalo anaamini litasaidia hata kuwajenga kiujuzi wanafunzi kuweza kutumia mafunzo hayo ili kujitegemea hapo baadaye.
Alisema mkulima, mwekezaji au yeyote kwenye mnyororo wa kilimo hicho anayehitaji kuwekeza kwenye alizeti serikali itamlinda na kumhakikishia kila aina ya ushirikiano.
Hata hivyo, aliwakumbusha Wizara ya Kilimo kuandaa kalenda ya kilimo cha zao hilo na kuisambaza kwa wakulima kabla ya msimu mwingine kuanza sambamba na kuongeza idadi ya maafisa ugani kwenye Vijiji na Kata ili kuongeza tija.
Waziri Mkuu pia aliwaagiza Wakuu wa Wilaya ambazo alizeti inalimwa kuandaa vitalu vya mashamba darasa ya mbegu bora kama mwendelezo wa uzalishaji wake baada ya Utafiti, ili kurahisisha upatikanaji wake.
Suala la mkoa husika kuwa na kanzi data (database) ya wakulima na hali halisi ya kilimo hicho ni miongoni mwa maagizo yaliyopewa mkazo lengo ni kufanya kilimo cha alizeti kuwa tegemeo, na hatimaye kuweza kusambaza uchumi wa mtu mmoja mmoja.
Agizo lingine ni kuanza kuunda vikundi vya ushirika ili kurahisisha usambazaji elimu ya mbinu bora za kilimo, lakini zaidi kupeleka huduma za kiugani kwa mkulima kwa wakati.
Pia aliwataka Wakuu wa Wilaya kuhakikisha kila Afisa Ugani anapimwa Kwa matokeo Kwa kupewa eneo na kulima yeye mwenyewe shamba lake la mfano kulingana na zao la mahali husika, ili wakulima wanaomzunguka waende kujifunza kwake, na endapo shamba hilo litashindwa kutoa matokeo mazuri basi aondolewe kwenye halmashauri husika.
Hata hivyo, Waziri Mkuu alizitaka Taasisi mbalimbali za Fedha, ikiwemo Benki ya Kilimo kujitambulisha kwa wakulima na kusambaza elimu ya namna ya kunufaika na mikopo ya kilimo suala ambalo wengi hawalifahamu.
Pia aliagiza Wizara ya Kilimo kuanza mkakati wa ujenzi wa maghala ya kuhifadhia alizeti sambamba na Wizara ya Viwanda kwenda mara moja kusikiliza kero mbalimbali zinazowakabili wenye viwanda vya ukamuaji mafuta ya zao hilo.
“Tutahakikisha mtandao wote wa wanaojihusisha na kilimo cha alizeti tunausimamia ipasavyo. Na naagiza kila kiongozi au taasisi itakayofanya mkutano wowote kwenye mikoa inayolima zao hili kuwe na ajenda ya kuhamasisha alizeti,” alisema Waziri Mkuu na akaongeza;
“Kikao hiki sio mwisho nitarudi tena Kwa tathmini kabla ya msimu kuanza ili kuangalia je tulijipanga kwenye kuhamasisha?, pembejeo zimefika kwa wakati? je tuko tayari kulima?, tumeandaa ekari ngapi kwa kilimo hiki? ili tuone kama tutafikia shabaha yetu,” alisema kupitia kampeni hiyo ya Twende Tukalime Alizeti ina Faida.