Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma alipotembelea mradi wa ujenzi wa ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga katika eneo la Kiamili.Mradi huo unatarajia kugharimu zaidi ya shilingi bilioni mbili hadi kukamilika
Mkuu wa Wilaya ya Mbinga Cosmas Nsenye akitoa maelezo kwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge kuhusu vijana walivyoshirikishwa kwenye mradi huo kufyatua matofali ambayo yanatumika kutekeleza mradi huo
Kikundi cha vijana wa Kigonsera ambacho kimeshirikishwa kwenye mradi wa jengo hilo kwa kufanyakazi ya ufyatuaji matofali ya kutekeleza mradi huo
……………………………………………………………
MKUU wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge ameupongeza uongozi wa Halmashauri ya Mbinga kuwashirikisha vijana katika mradi wa ujenzi ofisi za Halmashauri hiyo unaogharimu zaidi ya shilingi bilioni mbili.
RC Ibuge ametoa pongezi hizo baada ya kutembelea mradi wa jengo la Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo unaotekelezwa katika eneo la Kiamili Kata ya Mkako wilayani Mbinga.
R.C Ibuge ameridhishwa na maendeleo ya mradi huo unaojengwa na SUMA JKT,ambapo amepongeza jitihada mbalimbali zinazofanywa na uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga chini ya uongozi wa Mkurugenzi Mtendaji,Juma Mnwele.
Brigedia Jenerali Ibuge ameridhishwa na jitihada zinazofanywa kuwezesha jamii kupitia vikundi vya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu ikiwemo kikundi cha vijana cha Chipukizi ambacho kinajishughulisha na ufyatuaji wa tofali zinazotumika kwenye ujenzi wa jengo hilo la Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji.
Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Juma Mnwele akitoa taarifa ya ujenzi wa mradi huo,amesema hadi sasa zimeletwa shilingi bilioni moja na zaidi ya shilingi milioni 400 hadi sasa zimetumika kwa ajili ya hatua za awali za utekelezaji wa mradi huo ikiwemo ununuzi wa vifaa mbalimbali vya ujenzi.
“Tumemkabidhi mradi SUMA JKT kuanzia Juni 2 mwaka huu,kwa kuanzia tumemlipa shilingi milioni 78,tunaridhika na utekelezaji wa mradi huu,vijana wameshirikishwa kikamilifu katika mradi huu’’,alisema Mnwele.
Hata hivyo Mkurugenzi huyo wa Halmashauri ya Mbinga amesema Kikundi cha Chipukizi kilichopo Kata ya Kigonsera mwaka huu 2021 kimenufaika kwa kupatiwa mkopo wa shilingi Milioni 22.
Amesema kikundi hicho ambacho kinashiriki kwenye mradi huo,ni miongoni kwa vikundi vingine zaidi ya 20 ambavyo vimewezeshwa mikopo yenye thamani ya zaidi ya shilingi Milioni 330 ikiwa ni asilimia 10 ya fedha za mapato ya ndani kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga kwa mwaka wa fedha 2020/2021hadi 2021/2022.