Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiangalia mashine maalum ya kuoteshea alizeti, wakati wa mkutano na wadau wa zao la alizeti, katika ukumbi Catholic Social Hall, Juni 13, 2021, mkoani Singida. Wa kwanza kushoto ni Waziri wa Kilimo Prof. Adolf Mkenda.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akipewa maelezo kutoka kwa Meneja wa Wakulima Wadogo Edwin Shio kuhusu mbegu ya zao la alizeti, wakati alipotembelea mabanda, kwenye mkutano na wadau wa zao la alizeti, uliyofanyika katika ukumbi Catholic Social Hall, Juni 13, 2021, mkoani Singida.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza jambo na Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Crop Bioscience Solution Limited Wilfred Mushobozi, wakati alipotembelea mabanda, kwenye mkutano na wadau wa zao la alizeti, uliyofanyika katika ukumbi Catholic Social Hall, Juni 13, 2021, mkoani Singida.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiangalia mafuta yanayotokana na zao la alizeti kutoka kwa kampuni ya Singida Fresh Oil Mill, wakati alipotembelea mabanda, kwenye mkutano na wadau wa zao la alizeti, uliyofanyika katika ukumbi Catholic Social Hall, Juni 13, 2021, mkoani Singida. Wa kwanza kushoto ni Waziri wa Kilimo Prof. Adolf Mkenda.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza na wadau wa zao la alizeti katika ukumbi Catholic Social Hall, Juni 13, 2021, Mkoani Singida.
Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu
……………………………………………………………………..
*Asema lengo ni kuhakikisha nchi inaondokana na uagizaji wa mafuta ya kula
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Wakuu wa Mikoa, Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri, Maafisa Kilimo na Maafisa Ushirika nchini washirikiane katika kusimamia kilimo cha zao la alizeti kuhakikisha nchi inaondokana na utegemezi wa kuagiza mafuta ya kula kutoka nje.
“Lengo la Serikali ni kuongeza uzalishaji na tija kwa kuimarisha utafiti, huduma za ugani, upatikanaji wa mbegu bora na viuatilifu, kuongeza matumizi ya zana bora za kilimo, kuwajengea uwezo wazalishaji kuhusu kanuni za kilimo bora, kuanzisha mfumo imara wa ugharamiaji wa mazao ya mafuta kwa kushirikisha taasisi za fedha.”
Ametoa agizo hilo leo (Jumapili, Juni 13, 2021) wakati akizungumza na wadau wa zao la alizeti katika mkutano uliofanyika kwenye ukumbi wa Kituo cha Mafunzo ya Kanisa Katoliki, Mkoani Singida. Amesema hakuna sababu ya kuagiza mafuta ya kula kutoka nje kwa sababu nchi ina ardhi nzuri pamoja na nguvu kazi ya kutosha.
“Ni matarajio ya Serikali kuwa mikakati hiyo itawezesha kuongeza uzalishaji kutoka wastani wa tani 649,437 hadi tani 1,500,000 za alizeti zitakazochangia upatikanaji wa mafuta kwa takribani tani 300,000 ifikapo 2025. Pia Serikali imeendelea kuwekeza katika taasisi zinazohusika na utafiti na uzalishaji wa mbegu ili kuongeza tija.”
Waziri Mkuu amesema mahitaji ya mafuta ya kula nchini yanakadiriwa kuwa ni tani 650,000 na uzalishaji wa ndani ni wastani wa tani 290,000 sawa na asilimia 45 ya mahitaji kwa mwaka. Nchi hulazimika kuagiza wastani wa tani 360,000 hadi tani 400,000 kwa mwaka kufidia upungufu huo.
Amesema uagizaji wa mafuta ya kula kutoka nje kwa mwaka hugharimu takribani sh. bilioni 474. “Fedha hizi ni nyingi kama tungelikuwa tunajitosheleza katika uzalishaji wa mafuta hapa nchini, zingeokolewa na kuelekezwa kwenye maeneo mengine ikiwemo uboreshaji na utoaji wa huduma za afya, elimu na miundombinu.”
Waziri Mkuu amesema kutokana na umuhimu wa mafuta ya kula, Serikali imeweka mkakati wa kuongeza uzalishaji wa mazao ya mafuta yakiwemo ya chikichiki, alizeti, pamba, karanga na ufuta ili kujitosheleza na kuondokana na uagizaji wa mafuta kutoka nje ya nchi.
Amesema awali Serikali ilianza kutekeleza mikakati ya kuendeleza zao la michikichi kwa kuweka nguvu katika Mkoa wa Kigoma kwa kuanzisha kituo maalum cha Utafiti wa Mchikichi cha Kihinga.
“Kupitia utafiti huo, tumeanza kuona matokeo makubwa ya uzalishaji wa miche bora yenye uwezo wa kuzalisha mafuta kiasi cha wastani wa tani 5 kwa hekta ikilinganishwa na aina ya michikichi ya zamani iliyopo sasa inayozalisha wastani wa mafuta ya mawese tani 1.6 kwa hekta.”
Pia, Waziri Mkuu amesema Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi imeamua kulipatia uzito unaostahili zao la alizeti kwa kuwaunganisha wadau na kuanzisha kampeni ya kilimo bora cha alizeti pamoja na kuhamasisha viwanda vya kukamua mafuta kwa kuboresha teknolojia kwa viwanda vilivyopo na kuanzisha viwanda vipya kulingana na mahitaji.
Waziri Mkuu ameielekeza Wizara ya Kilimo iendelee kuwatambua wadau wanaowekeza kwenye zao la alizeti katika uzalishaji, viwanda na masoko na kuwaunganisha na wakulima na taasisi nyingine zikiwemo taasisi za fedha ili kuwa na uhakika wa upatikanaji wa mitaji, masoko na malighafi kwa ajili ya viwanda vya mafuta.
“Wizara ya Kilimo, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha kuwa uzalishaji wa mazao ya mafuta hususan zao la alizeti unasimamiwa kikamilifu kwa kuweka mfumo thabiti wa usimamizi na ufuatiliaji katika ngazi zote.”
Kadhalika, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwahamasisha wananchi kulima zao la alizeti ili waweze kujiongezea kipato. “Kama unataka utajiri wa haraka ndani ya miezi mitatu, minne lima alizeti kwa sababu kilimo chake si kigumu. Kwa hiyo ukitaka fedha ya haraka, nzuri na ya uhakika na yenye faida kubwa lima alizeti”
Kwa upande wake, Waziri wa Kilimo Profesa Adolf Mkenda amesema Serikali imeweka mkakati wa kuboresha huduma za ugani kwa kuongeza bajeti ili kuhakikisha wakulima wa zao la alizeti wanalima kilimo bora na kuongeza tija kwenye uzalishaji.
“Tumechagua mikoa mitatu ya Dodoma, Singida na Simiyu kwa kuanzia kwa sababu ni mikoa ambayo inalima mazao mbalimbali kwa ajili ya uzalishaji wa mafuta, ila kampeni hii ni ya nchi nzima na mikakati itakayowekwa ni kwa mikoa yote”