Home Burudani TAMASHA LA MUZIKI LA SUNWAVES 2021 KUFANYIKA DONGWE,ZANZIBAR

TAMASHA LA MUZIKI LA SUNWAVES 2021 KUFANYIKA DONGWE,ZANZIBAR

0
……………………………………………………………
NA ANDREW CHALE, ZANZIBAR.
TAMASHA kubwa la Kimataifa la muziki linalofanyika kila mwaka katika fukwe nchini Romania la Sunwaves linatarajiwa kufanyika kwa mara ya kwanza kuanzia 17-21 Juni mwaka huu katika ufukwe wa Dongwe, Unguja-Zanzibar.
Mwandaaji wa tamasha hilo, Bw. John Borzea raia wa Romania, amesema maandalizi ya tamasha yanaendelea vizuri huku tiketi zikiendelea kuuzwa kwa njia ya mtandao duniani kote na pia  tiketi zitauzwa getini kila siku ya tamasha.
“Muziki mzuri na wa Kimataifa utakaochanganywa kisasa jukwaani utaacha simulizi kwa kila atakaefika kwa tamasha lengo ni kukonga nyoyo za watu kupitia muziki mzuri ndani ya Sunweves”. Alisema John Borzea.
John Borzea aliongeza katika tamasha hilo, kutakuwa na majukwaa mawili ya burudani, wasanii zaidi ya 40 kutoka Romania na Mataifa mengine Duniani kote wataamsha shangwe la nguvu kwa mara ya kwanza katika kisiwa cha Zanzibar.
“Hadi sasa maandalizi yanaendelea vizuri, wasanii na watu maarufu tayari wapo kwenye listi ya tamasha ya Sunwaves wakiwemo; Dj maarufu wa Kimataifa, Black Coffee, Msanii wa Romania, Dan Andrei, Mwanadada Alexandra kutoka Romania, Msanii Hoctor kutoka Mexican, Mahony, Ricardo Villarobos, Marco Carola, Priku, Joey Daniel, Loco Dice, Dubifire, Emi, Mihigh, Sepp, Themba, Yaya, Rhadoo, Raresh,Petre Inspirescu, Nu Zau, Neverdogs, Arapu, G76, Cap, Direct, Kozo, Herodot, Maher Daniel, Gescu na wengine wengi. 
Kwa upande wao Jumuiya ya watembeza watalii Zanzibar [ZATO], kupitia kwa Mwenyekiti wake, Bw. Hassan Ali Mzee amesema wamelipokea kwa mikono miwili kwani linatarajia kuongeza Watalii na kuiingizia fedha nyingi nchi kwa wageni watakaofika kupata burudani na kuendelea kukuza uchumi kupitia Utalii.
“Tamasha hili linafanyika kwenye fukwe kila mwaka nchini Romania, kwa mara ya kwanza safari hii wanalileta Zanzibar hii ni fursa ya kipekee kwetu kwani linafaida zake za kiuchumi na tunataka liwe endelevu kwa kufanyika hapahapa Zanzibar. 
Tuendelee kuliunga mkono kwani wageni watakaofika watalala mahoteli na pia kununua bidhaa zetu. Ambapo linatarajiwa kuleta wageni zaidi ya 3000, watakaoshiriki tamasha hilo kutoka Duniani kote”. Alisema Hassan Ali Mzee.
Aliongeza kuwa: “Wakati wa tamasha Sunwaves siku nzima kwa maana masaa 24 watu watapata burudani ya muziki bila kupumzika .. yaani mchana kutwa usiku kutwa ni burudani ya muziki tu kwenye fukwe. Bidhaa mbalimbali vyakula na vinywaji pia vitakuwepo kila anayependa burudani anakaribishwa raia wote ukiweza kulipia kiingilio tu”. Alimalizia Hassan Ali Mzee.
Tamasha la Sunwaves lilianzishwa maalum mwaka 2007 likiwa na wazo la kuunganisha Jamii kupitia muziki wa kisasa kwa kuburudisha na kuuheshimu ambapo kwa Romania, ni tamasha la kwanza kubwa la kila mwaka huku kizingatia usalama wa Mazingira kwa kulinda fukwe.