Waziri wa Ardhi Mh. William Lukuvi akiwa katika picha na pamoja na Waimbaji wa Muziki wa Injili wa Mkoa wa Iringa (Iringa Gospel Stars) bungeni
Waziri wa habari, Utamaduni,Sanaa na Michezo Mh. Innocent Bashungwa akiwa katika picha ya pamoja na Waimbaji wa Muziki wa Injili wa Mkoa wa Iringa (Iringa Gospel Stars)
Mwandishi wetu, Dodoma
Waimbaji wa Muziki wa Injili wa Mkoa wa Iringa (Iringa Gospel Stars) wamefanya ziara Bungeni mjini Dodoma na kupata nafasi ya kuzungumza na Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Mh Innocent Bashungwa.
Iringa Gospel Stars walifanya ziara ya kujifunza jana baada ya kupata mwaliko toka kwa Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Iringa, Ritha Kabati.
Pia, wanamuziki hao walipata nafasi ya kuonana na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mh William Lukuvi.
Akizungumza na waimbaji hao, Waziri Bashungwa aliahidi kushirikiana nao katika kukuza sekta ya muziki kwa kuhakikisha wasanii hasa wachanga wanaendelewa kupewa elimu kuhusu matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii.
“Nafahamu mnahitaji elimu hiyo, nitazungumza na Basata pamoja na Cosota kuona namna gani watasaidia kuwapatia elimu ili mnufaike na kazi zenu,” amesema Bashungwa na kuongeza;
“Hata hivyo safari hii bajeti yetu ieongezeka kwa hiyo tumshukuru Rais wetu, Mh Samia Suluhu Hassan kwa kusaidia ongezeko kwenye bajeti yetu, kazi inaendelea.”
Awali Mwenyekiti wa Iringa Gospel Stars, Dkt Tumaini Msowoya alimuomba Waziri Bashungwa kupitia wizara yake kuwasaidia wasanii hasa wanaochipukia elimu kuhusu matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii na namna wanavyoweza kuuza kazi zao.
“Wengi hawajui namna gani mitanbdao ya kijamii inaweza kuwasaidia, mziki umehama kutoka kwenye CD mpaka kwenye simu za mkononi. Tunakuomba Mh Waziri kupitia wizara yako, kutoa elimu kwa hawa wasanii ili kukuza vipaji vyao na kunufaika na kazi zao,” amesema.