Afisa Lishe Mtafiti Bi.Maria Ngilisho akiwasilisha mada katika Semina kwa waandishi wa habari iliyofanyika katika ofisi za Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC) leo Jijini Dar es Salaam. Afisa Lishe Mtafiti Mwandamizi Bi.Julieth Shineakiwasilisha mada katika Semina kwa waandishi wa habari iliyofanyika katika ofisi za Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC) leo Jijini Dar es Salaam.
Afisa Lishe Mtafiti Bi.Elizabeth Lyimo akiwasilisha mada katika Semina kwa waandishi wa habari iliyofanyika katika ofisi za Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC) leo Jijini Dar es Salaam.
Wanahabari wakifuatilia semina iliyofanyika katika ofisi za Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC) leo Jijini Dar es Salaam.
(PICHA ZOTE NA EMMANUEL MBATILO)
***********************
NA EMMANUEL MBATILO
Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC) yashauri utumiaji wa lishe bora kwa watoto na watu wazima ili kuepuka magonjwa mbalimbali yasiyo ya kuambukiza ambayo yamekuwa tishio Duniani.
Akizungumza katika semina kwa waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam,Afisa Lishe Mtafiti Bi.Maria Ngilisho amesema ulaji wa vyakula vyenye mafuta mengi hasa yenye asili ya wanyama huchangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la lehema mwilini.
“Kiasi kikubwa cha lehemu mwilini husababisha mkusanyiko wa mafuta katika mishipa ya damu hivyo kuzuia damu kupita kwa urahisi.Vyakula vyenye lehemu nyingi ni nyama, mayai, jibini na maziwa yasiyotolewa mafuta, maini, moyo, firigisi na figo”. Amesema Bi.Maria.
Aidha Bi.Maria amesema unywaji maji safi, salama na ya kutosha ni sehemu ya mlo kwani yana umuhimu kiafya hivyo inashauriwa kunywa maji safi na salama angalau lita moja na nusu kwa siku.
Nae Afisa Lishe Mtafiti Mwandamizi Bi.Julieth Shine amesema kuwa ulaji unaoshauriwa kwa mtu mwenye shinikizo kubwa la damu ni pamoja na kuepuka vyakula vyenye chumvi nyingi na vile vilivyosindikwa kwa chumvi hivyo unatakiwa kutumia viungo mbalimbali kuongeza ladha ya chakula kwa mfano tangawizi, ndimu, vitunguu saumu na mdalasini.