Msanii wa muziki wa Kizazi kipya (Bongo Flava), Nandy akitoka katika Ofisi za TTCL Kijitonyama Jijini Dar es Salaam mara baada ya hafla hiyo. |
*Ofa Kabambe kutolewa kwa watakao Rudi Nyumbani
Na Mwandishi Wetu
SHIRIKA la Mawasiliano Tanzania limesaini Makubaliano na Msanii wa Muziki wa Kizazi Kipya Faustina Charles Mfinanga alimaarufu Nandy yakuwa Mdhamini Mkuu wa Tamasha la Nandy Festival 2021.
Hafla ya makubaliano hayo ilifanyika katika ofisi za TTCL Kijitonyama jijini Dar es Salaam ambapo Uongozi wa EASTWAVE MARKETING ambao ndiyo waandaaji wa Tamasha la hilo waliomba TTCL kushirikiana nao katika kufanikisha tukio hilo kubwa katika Tasnia ya Muziki hapa nchini na Afrika kwa ujumla.
Akizingumza katika hafla hiyo Mkurugenzi wa Biashara kutoka TTCL Ndugu Vedastus Mwita alisema baada ya mchakato wa kibiashara kukamilika TTCL Corporation imekuwa Mdhamini Mkuu wa Tamasha la NANDY FESTIVAL 2021 ambapo, kuanzia sasa litaitwa TTCL Nandy Festival 2021- Watakaa tu.
Tamasha hili litafanyika katika Mikoa Kumi (10) ambayo ni pamoja na Dar es Salaam, Dodoma, Mwanza, Sumbawanga, Kigoma, Shinyanga, Kilimanjaro, Tanga, Arusha na Zanzibar huku matarajio yakiwa ni kwamba Wananchi wa Mikoa hiyo na visiwa vya Zanzibar watapata burudani ya muziki yenye ubora na kiwango cha Kimataifa.
Katika udhamini huo TTCL inatarajia kufikia wateja wake ambapo katika kunogesha tamasha hilo inatoa ofa kwa Wateja wapya ambao watasajili laini zao katika kipindi chote cha tamasha hilo. Amesema kila Mteja mpya atakuwa na uwezo wa kupiga simu mitandao yote dakika 50, kupata MB 150 na SMS 50 bure kwa siku saba.
“tunapenda kuwakaribisha zaidi wananchi wajitokeze kwa wingi kuchukua laini zetu sambamba na kuingia uwanjani ambapo Tamasha litakapokuwa linafanyika ili kuweza kunufaika na huduma kutoka TTCL ambako ndiko nyumbani “alisema Mwita.
Aliongeza kuwa ili kuongeza radha za Tamasha hili, Mashabiki na wapenzi wa Muziki wa Nandy watakaonunua tiketi kupitia T-PESA watapata punguzo maalum hivyo hawapaswi kubaki nyuma ni vyema wakachangamkia fursa hiyo adhimu ya kumuona Msanii wao mubashara katika maeneo yao.
Katika hatua nyingine Mwita alimpongeza Nandy kwa uthubutu wake wa kuanzisha Tamasha la kuwapa burudani mashabiki zake na wapenda burudani nchini na kwamba uthubutu huo ni ishara kuwa Wanawake kupitia sekta mbalimbali wanaouwezo mkubwa wa kuleta mageuzi makubwa kiuchumi, kijamii na kisiasa.
Kwa upande wake Moko Biashara ambaye ni Meneja wa Nandy alisema anaishukuru TTCL kwakukubali kuitika wito wa kumuunga mkono Nandy katika Tamasha lake na kwamba tamasha hilo litakuwa chachu kwa wateja wa TTCL ambapo pamoja na mambo mengine Wananchi wataweza kujisajili na kujipatia laini ya TTCL, watanunua bidhaa na kupata elimu kuhusu huduma na bidhaa zinazotolewa na Shirika hilo.
Naye Msanii Nandy amesema TTCL kujitoa na kuwa mdhamini mkuu si jambo dogo hivyo analishukuru shirika hilo kwakuona umuhimu wa kutumia Tamasha lake kuwarudisha Watanzania Nyumbani kupitia burudani atakayoitoa katika mikoa iliyoandaliwa.
Nandy aliviambia vyombo vya habari kuwa atahakikisha anafanya kazi kwa weledi mkubwa utakaosaidia TTCL kusajili wateja wengi zaidi wapya, kuuza bidhaa na kutoa elimu kuhusu mawasiliano kwa wananchi katika maeneo aliyopanga kutoa burudani.
“Mimi ni wahakikishie tu kwamba nitafanya kazi kwa uweledi wa hali ya juu na tumeishaonesha mfano katika Mkoa wa Kigoma ambapo si chini ya elfu kumi na nane ya mashabiki na wapenzi wa burudani waliingia katika tamasha letu na kupitia idadi hii tunayo matumaini ya kuwarudisha nyumbani waanze kutumia huduma zinazotolewa na TTCL,” alisema Nandy.
Tamasha hili linalobebwa na kauli mbiu ya TTCL Nandy FESTIVAL 2021, Watakaa tu, limeanza kwa mafanikio makubwa Mkoani Kigoma ambapo limewakutanisha mashabiki wengi na wapenda burudani mkoani humo na kuacha historia kutokana na Wasanii wakubwa nchini ambao wameshiriki katika Tamasha hilo.